Mressa kumvaa Mhita Kondoa Kaskazini


Nicoline John's picture

Na Nicoline John - Imechapwa 29 September 2009

Printer-friendly version
Ana kwa Ana

FRANK Mumba Mressa (30) ni miongoni mwa wa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliojiingiza katika harakati za kuwania ubunge jimbo la Kondoa Kaskazini, mkoani Dodoma katika uchaguzi mkuu wa mwaka kesho.

Mressa ni ofisa katika Benki ya CRDB tawi la Lumumba, Dar es Salaam.

Mbunge wa sasa wa jimbo la Kondoa Kaskazini ni Zabein Muhita. Aliingia bungeni kupitia sanduku la kura mwaka 2005 kwa kumshinda Halidi Suru, ambaye alikuwa mbunge wa jimbo hilo kwa muda wa miaka 10 kati ya mwaka 1995 hadi 2005.

Halidi naye alichukua kiti hicho kutoka kwa Balozi Mustapha Nyang'anyi, aliyeongoza jimbo hilo kwa muda wa miaka 25. Nyanganyi ni miongoni mwa wanachama wa CCM wanaotajwa kutaka kuwania tena nafasi hiyo katika uchaguzi ujao.

Wengine wanaotajwa mbali na Nyanganyi, Mressa na mbunge wa sasa Muhita, ni Edwin Sanda na Rajabu Msii.

Katika mahojiano yake na MwanaHALISI wiki hii, Mressa anasema ameamua kujitosa katika kinyang'anyiro hicho kutokana na kile alichoita, "Muhita kushindwa kazi."

Anasema uamuzi wake wa kuwania ubunge wa jimbo hilo umetokana na sababu mbili kubwa. Moja, ni kuombwa na baadhi ya wazee, vijana na wanawake wa jimbo hilo, na pili ni uchungu alionao kwa wananchi wanaoishi katika jimbo hilo.

"Nimeamua kugombea baada ya kuombwa na wazee na baadhi ya vijana. Hawa ndio walionisukuma kutaka nigombee nafasi hii. Wameniomba nijitose katika uchaguzi wa mwaka kesho," anasema.

Anasema; "Mimi nikiwa kada ninayekitakia mema chama changu, nikiwa kijana mwenye uchungu na wananchi wenzangu na taifa langu, sikuona sababu ya kukataa ombi la wazee wangu."

Anasema kwa muda wa miaka 30 jimbo la Kondoa limeongozwa na watu wasiokuwa na uchungu wa maendeleo na uzalendo kwa taifa lao. Ndiyo maana mpaka sasa, wilaya ya Kondoa haijaweza kuunganishwa kwa barabara za lami na mikoa mingine inayopakana na wilaya hiyo kama vile Dodoma, Singida na Arusha.

"Miaka 30 Kondoa hakuna barabara. Hakuna shule za uhakika, hakuna maji, hakuna zahanati za kutosha.

"Shule nyingi zilizopo hazina walimu wa kutosha wala vitabu vya kufundishia. Haya yote yanafanyika kutokana na wananchi kutokuwa na wawakilishi wanaojali shida zao; wenye uwezo wa kujenga hoja na kuwatetea," anasema Mressa.

Alipoulizwa kama ana ‘ubavu' wa kushindana na wanasiasa wakongwe, Mressa haraka alijibu; "Nina ubavu. Nimejiandaa vya kutosha, si kujaribu, bali nimejiandaa kushinda."

Mressa anasema kinachompa nguvu ya kujitapa kuwa anakwenda kushinda, ni uamuzi wa Hamashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), kubadili mfumo wa kupatikana wagombea kupitia chama hicho.

Hivi sasa wagombea wa nafasi za ubunge na udiwani kupitia CCM watapigiwa kura na wanachama wote wa CCM kupitia mikutano mikuu ya kata.

"Mfumo huu mpya wa uchaguzi ni mzuri na unaweza kuzuia vitendo vya rushwa vinavyotawala chaguzi zetu. Hii ni kutokana na wanachama wengi kushirikishwa, jambo ambalo linaweza kuwapa ugumu wa kushinda mabingwa wa kununua kura," anasema.

Mressa anasema kuwa mfumo wa zamani wa kura za maoni za CCM ulikuwa unatoa nafasi kwa watu wachache, na ulijenga vitendo vingi vya rushwa kuchangia kupatikana kwa viongozi wasio na sifa.

Anasema; "Hivi sasa kuna wapiga kura wengi ambao huwezi kuwahonga, hivyo kila mtu atatumia haki yake ya kikatiba na sio rushwa ili kuweza kupata uongozi."

Kada huyo kijana anasema ni muhimu kwa chama chake kuweka ulinzi maalum katika utoaji wa kadi za uanachama ili kuthibiti wimbi la wagombea wanaotumia mwanya kusambaza kadi kwa wanachama mamluki.

Kwamba ugawaji wa kadi za CCM bila kufuata mpangilio ni rushwa na kama mwanachama yeyote akipatikana na kadi hizo ashitakiwe mahakamani na azuiwe kuingia katika uchaguzi.

Anataka wananchi wasikubali kudanganywa kwa fedha kidogo na kuwafanya wachague watu wasiokuwa na uwezo, wanaotafuta maslahi binafsi.

Kuhusu siasa anasema ni mchezo wa kuigiza kutokana na kubadilika kwa upepo mara kwa mara, hasa wagombea wanapojipitisha kwa wanachama kujinadi na kutoa ahadi za uongo.

Pamoja na kuombwa na watu anasema anafaa kuwa kiongozi kwani amewahi kuwa makamu wa rais wa serikali ya wanafunzi ya Chuo Kikuu cha Mzumbe, kilichopo mkoani Morogoro.

Hivi sasa yuko tayari kuwatumikia wananchi katika shughuli zao, kwa kuwa ana uwezo wa kujituma na ameishi Kondoa, amesoma huko na anayafahamu mazingira.

Anafahamu jinsi wazazi wake wanavyotembea umbali mrefu kutafuta huduma muhimu kama vile maji. "Mimi ninafahamu vizuri mazingira ya kwetu kwa kuwa nilikuwa natembea kutafuta huduma hiyo tangu zamani."

Changamoto anayoitoa kwa wanachama ni kwamba wawe makini na kuchagua watu wenye uwezo mkubwa na moyo wa kujituma.

Anasema tayari CCM kina malengo yake na wanaotaka kuingia ndani yake lazima wawe na malengo kwa ajili ya wananchi na si maslahi binafsi.

"Sishangai kuona watu wameanza kuonyesha nia ya kugombea mapema kwa sababu ni njia ya kujitangaza ili watu waamue ni yupi watakaye mchagua.

"Japo tunatambua jimbo lina mbunge ambaye ni Mhita (Zabein) lakini tuna haki pia kujitangaza ili watu watujue," anasema Mressa.

Frank Mressa alizaliwa katika kijiji cha Kandaga wilaya ya Kondoa, mkoani Dodoma, mwaka 1979.

Alipata elimu yake katika Shule ya Msingi Kandaga, iliyopo kata ya Masange, Kondoa.

Alipata elimu yake ya kidato cha kwanza hadi cha nne katika Shule ya Sekondari ya Jitegemee, Dar es Salaam, na baadaye alipata elimu ya kidato cha tano na cha sita katika Shule ya Sekondari ya Makongo.

Alijiunga na Chuo Kikuu cha Mzumbe kwa masomo ya biashara na utawala, ambako alihitimu shahada ya kwanza mwaka 2004.

Ana mke aitwaye Leticia.

Pamoja na kuwa mmoja wa maofisa wa benki ya CRDB, sasa ni mwanafunzi wa shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Pia anafanya kazi zake binafsi kama mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Orange Investment. Pia ni ofisa mtendaji mkuu wa Mumba Ostrich Farm, ambayo malengo yake ni kuongeza ajira ya watu zaidi ya 100 katika wilaya ya Kondoa.

Hupendelea kucheza mpira wa miguu. Ni kiongozi wa timu yake ya Kijitonyama Chipukizi, ya Dar es Salaam.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: