Msajili wa mahakama kuu katika kashifa


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 18 May 2011

Printer-friendly version

UONGOZI wa Mahakama ya Rufaa Tanzania unatuhumiwa kutowatendea haki wafanyakazi wake.

Katika waraka maalum unaodaiwa kuandikwa na wafanyakazi hao, wametishia “kuchoma moto majengo ya mahakama” iwapo hawatasikilizwa.

Katika andishi linaloonyesha kuwa waraka wa wanaojiita wafanyakazi wa ngazi ya chini, wametoa siku 21 kwa Jaji Mkuu, Othman Chande kumuondoa Msajili wa Mahakama hiyo, Francis Mutungi.

Waraka umenukuu malalamiko ya wafanyakazi wa idara hiyo ukisema, uongozi wa Mutungi umekuwa ukiwagawa wafanyakazi kitabaka.

Katika waraka wao uliosheheni malalamiko, wafanyakazi wanamueleza jaji mkuu kuwa ndani ya mahakama “kumekithiri dhuluma, uonevu, ulaghai na uasherati.”

Wanawake wanaotajwa kufanya uasherati na vigogo hao (majina tunahifadhi), ni kutoka idara ya uhasibu, ofisi ya msajili wa mahakama na ofisi ya jaji mkuu.

Waraka huo wenye kurasa 17 umeanza kwa nukuu ya Jaji Jackson Robert, aliyewahi kuwa jaji mkuu wa Marekani na umeishia kwa nukuu ya Mwongozo wa TANU wa mwaka 1971.

“Kuna matabaka makuu mawili ndani ya jengo la Mahakama ya Rufaa (ukiondoa majaji na wakurugenzi) ambayo yameegemea katika upande wa malipo, ujira na mengineyo,” wanasema wafanyakazi katika waraka wao huo.

Wanasema, “Matabaka hayo hayasababishwi na aina ya kazi anayofanya mtu au kada na ieleweke kuwa hatuna lengo kusema kuna unyanyasaji wa ajira. Ni tabaka la chini na tabaka la juu ambayo yamegawanyika sehemu mbili. Matabaka baina ya vitendo na matabaka baina ya watumishi wenyewe.”

Katika waraka huo, ambao hauna saini, wafanyakazi wanamtuhumu Mutungi, pamoja na wafanyakazi wa idara ya uhasibu kuwa wamegubikwa na ufisadi.

Wamemtaka jaji mkuu kumwondoa Mutungi kwenye wadhifa wake ndani ya siku 21 na kuonya kuwa akiendelea kuwepo, “ataondolewa kwa nguvu.”

“Sisi ndio tunafungua milango, tunawaendesha, tunakaa na funguo za ofisi, tunawanunulia chakula na kuwahudumia; kwa uhuru tulionao, tunaweza kujua mengi mpaka sasa tunauwezo kuchoma majengo ya mahakama ndani ya nusu saa popote yalipo na kuwaua majaji wote kwa dakika saba bila ya kujali mahali walipo,” unasema waraka.

Katika ukurasa wa mwisho, wafanyakazi wanasema, “Tumeonewa kiasi cha kutosha, sambamba na kunyonywa, kupuuzwa, hivyo tunataka mapinduzi ya kuondoa unyonge ili tusionewe, tusinyonywe tena wala tusipuuzwe tena.”

Waraka umesambazwa kwa vyombo vya habari pamoja na Jaji Kiongozi, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Waziri wa Sheria na Katiba. Pia umenakiliwa kwa Mhasibu wa Mahakama, Fanuel Tibuza na Mkuu wa Mafunzo na Kompyuta, Essaba Machumu.

Wafanyakazi wanadai mshahara wa Sh. 150,000 na posho ya Sh. 90,000 kwa mwezi na wanadai hawana mazingira mengine yanayowawezesha kupata fedha nje ya malipo hayo.

“Mzunguko wa malipo kwa mlinzi (kwa mfano), ukiondoa mshahara wa Sh. 150,000 kwa mlinzi aliyesoma, hakuna malipo yoyote zaidi ya posho, yaani elfu tisini kwa mwezi.

“Mtu huyu hana hoja nyingine ya kujenga ili apate pesa angalau hata Sh. 1,000 nyingine, zaidi ya posho tu na mshahara ambao kwa sababu ya madeni wengi wao tunadaiwa mikopo benki mbalimbali,” waraka unaeleza.

Kada nyingine ya watumishi wa chini inajumuisha wahudumu wa ofisi na makarani ambao baadhi, wanafikia hatua ya kugoma kuhamia ofisi za majaji, maktaba au kwa msajili wanakodai kuna “iziki.”

Kadhalika, waraka unadai matabaka kati watumishi wenyewe wa tabaka la chini, pia kuna tabaka kulingana na aina ya ofisi ambayo mhudumu anafanyia.

Wanatoa mfano: Wahudumu wanaofanya kazi katika ofisi za uhasibu hasa kwa “chifu” – Mhasibu Mkuu (CA) na wale wanaofanya kazi katika ofisi kama store (PMU), DAP, AU na RCA au SDR-CA wako tofauti na hawapendi kuhamishwa kwa sababu ya unafuu uliopo.

Wakimtuhumu Tibuza, wanadai pamoja na idara yake ya uhasibu, hatoi kipaumbele katika kushughulikia madai ya fedha za wafanyakazi wa kada hiyo, badala yake anaangalia wale wa ngazi za juu tu.

“Inakuaje majalada ya malipo ya Jaji Mkuu, Majaji wa Mahakama ya Rufaa, Msajili na Mkurugenzi hushughulikiwa haraka zaidi kuliko malipo ya wahudumu, makarani na walinzi, wakati wote wanafanya kazi katika idara moja,” wanahoji.

Katika waraka wao, wameorodhesha safari za viongozi walizodai kuwa ni hewa na kwamba ni “sehemu ya ufisadi” mahakamani.

Waraka unataja mapendekezo 13 wakitaka yafanyiwe kazi wakiamini kuwa ndipo usawa katika utendaji miongoni mwa wafanyakazi utarejeshwa.

Baadhi ya mapendekezo hayo ni kuendelea kwa utaratibu wa kila mtumishi kulipwa mshahara kulingana na elimu yake; kufutwa kwa utaratibu wa kila kitengo kuomba posho ya wafanyakazi wake na badala yake litumike jalada moja kwa watumishi wote.

Jaji Mutungi alipoulizwa kuhusu tuhuma hizo, alikiri kuzifahamu lakini alitoa maelezo mafupi: “Ninachoweza kusema kwa sasa habari hizo si kweli. Mamlaka husika zinaufanyia kazi (waraka huo). Ahsante.”

Mhasibu aitwaye Tibuza hakupatikana, lakini mmoja wa wasaidizi wake katika idara ya uhasibu ambaye aliomba jina lifichwe, alithibitisha kuuona waraka huo ambao “umesambaa hadi mikoani.”

Ofisa huyo wa idara ya uhasibu katika mahakama ya rufaa alisema: “Nadhani hao watoa taarifa walio-over look taarifa za kiuhasibu. Unajua kwa nini? Haiwezekani mtu wa idara ya uhasibu akaenda safari kama ya Mwanza kwa wiki moja akalipwa Sh. milioni nane.

“ Hilo haliwezekani kwa sababu za wadhifa wake, posho na siku zilizoripotiwa. Wewe unaona safari ya wiki kwa ofisa wa kawaida akalipwa Sh. milioni nane? Hilo haliwezekani.

“Madai mengine ya kijinga, kwenye huo waraka mwingine anadai eti sambusa na vipande vya viazi vinavyobaki kwenye semina au washa kuwa na zamu ya kuganwa,” ameeleza.

Kitu kingine ambacho alisema hakiwezekani kabisa ni kwamba hata siku moja haiwezekani jaji na mlinzi wakapata posho sawa.

Cha kuchekesha zaidi eti mlinzi au mhudumu naye anadai safari. Ya kwenda wapi na anakwenda kufanya nini? Majaji wanakwenda kusimamia kesi, huyo mhudumu naye aende akafanye nini?´amehoji ofisa huyo.

Mkuu wa kitengo cha kompyuta, Machumu alipoulizwa alisema anasikitika kwa kuwa anahisi madai yaliyotolewa si ya kweli.

“Sipendi kumsingizia mtu. Akili ni nywele na kila mtu ana zake. Ndugu mwandishi, madai hayo ni uongo na watu wanashindwa kumuogopa Mungu,” alisema Machumu.

Machumu amesema kuna wizara na idara za serikali zimebinafsisha vitengo vya uhudumu na ulinzi, lakini, jaji mkuu mstaafu, Agustino Ramadhani, alikataa kwa upande wa mahakama, hivyo ajira zao kuendelea.

“Lakini leo hii, haohao watumishi waandike waraka wa kumshutumu? Sijui! Tusubiri tuone baadaye,” alisema.

Gazeti hili limeshindwa kumpata Jaji Mkuu Chande wala Jaji Kiongozi Fakih Jundu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: