Msekwa ‘mtegoni,’ nani atakayebakia?


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 24 August 2011

Printer-friendly version
Gumzo la Wiki

PIUS Msekwa, Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ametumbukizwa katika kashifa.

Kiongozi huyo, ambaye inadaiwa alijipa kazi ya kuwafukuza wenzake wanaoitwa “mafisadi ndani ya CCM, naye sasa ameanza kuitwa gamba.

Anatuhumiwa kutumia vibaya jina la Rais Jakaya Kikwete kuidhinisha, kinyume cha sheria, ujenzi wa hoteli ya kitalii yenye hadhi ya Nyota Tano katika mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro.

Anadaiwa pia kujipa “kazi za kiutendaji” – kama katika mamlaka ya bodi ya Ngorongoro, kinyume cha taratibu.

Anatuhumiwa pia kuvunja kwa makusudi, sheria ya hifadhi ya bonde la Ngorongoro, kwa kuruhusu ujenzi wa hoteli kwenye bonde hilo.

Aidha, Msekwa anadaiwa kuliingizia taifa hasara kwa uamuzi wake wa kuingilia kazi ya kitaalamu katika mamlaka ya hifadhi; na kushiriki katika uharibifu wa mazingira katika eneo la hifadhi.

Kwa mkondo huu, nani atakayeweza kubaki salama ndani ya CCM? Nani ataweza kumnyooshea kidole mwenzake? Je, atakuwa na nguvu ya kimamlaka ya kufukuza wengine wanaokabiliwa na tuhuma za ufisadi?”

Tuhuma dhidi ya Msekwa ziliibuliwa bungeni wiki iliyopita, wakati wa mjadala wa bajeti ya wizara ya nishati na madini. Aliyeanza kuvurumisha madai hayo, ni Mbunge wa CHADEMA katika jimbo la Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa.

Naye Mbunge wa Ngorongoro, Kaika Terere (CCM), alimtuhumu Msekwa, kupitia Bodi ya Hifadhi ya Ngorongoro, akisema “imetenda kazi zake kinyume cha sheria na katiba ya nchi.”

Aliitaka serikali kuivunja mara moja bodi ya mamlaka hiyo na kuiunda upya. Alionya bodi mpya itakayoundwa, isimhusishe Msekwa.

Alisema, “Si busara serikali kumhusisha Msekwa katika bodi mpya kutokana na aliyotendea taifa hili.”

Mpaka sasa, Msekwa hajaweza kujibu tuhuma zilizoelekezwa kwake. Badala yake, amenukuliwa na vyombo vya habari akisema, “hayo ni maneno ya kijinga na kipumbavu.” Safari hii hajasema “ni wivu wa kike!”

Lakini nani awezaye kusema tuhuma dhidi ya Msekwa ni upuuzi? Tuhuma zimetolewa mbele ya bunge. Zimeelezwa na wabunge, akiwamo Terere – mbunge wa eneo husika, ambaye ana ufahamu mkubwa wa madhara ya kutuhumu kiongozi mkuu wa chama, bila kuwapo uthibitisho.

Ni Terere anayefikia hatua ya kushangaa, “Kikwete ndiye ametoa amri ya kuuzwa eneo hili?

Anauliza, “Rais gani awezaye kubariki uuzaji huu?” Anasema, hata kama ni Kikwete aliyebariki uharibifu huo, yuko tayari kukabiliana naye. Huu ni ujumbe mzito unaotoka kwa mtu mwenye uchungu na anayejiamini.

Telele amesimama na kupigania wananchi wa wilaya ya Ngorongoro kwa miaka 10 sasa. Tarehe 6 Novemba 2009 aliwasilisha maelezo binafsi bungeni akitaka ufafanuzi kuhusu hujuma dhidi ya wananchi Loliondo.

Samwel Sitta ambaye wakati huo alikuwa spika wa Bunge, aliiamuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira iliyokuwa chini ya Job Ndugai, kwenda Loliondo kuchunguza madai ya Telele. Kamati ya Ndugai iliilinda serikali; ikaishia kuficha ukweli.

Madai yote dhidi ya Msekwa, hata hivyo, yamemesheheni vielelezo. Kuna barua iliyoandikwa na Msekwa mwenyewe kwenda kwa waziri wa maliasili na utalii, Ezekiel Maige inayoagiza serikali kumpa kibali cha ujenzi wa hoteli ya kitalii mwekezaji wa kigeni kwenye eneo la mamlaka ya hifadhi.

Maige amethibitisha hili. Amesema amepokea barua kutoka kwa Msekwa. Amekiri pia kutekeleza agizo lililomo katika barua hiyo bila kushirikisha watendaji wa wizara yake.

Maige amesema jambo hilo laweza kumuingiza katika mgogoro mkubwa wa kisheria iwapo mwekezaji aliyepewa eneo hilo awali ataamua kwenda mahakamani kupinga uamuzi wa kubatilisha maamuzi yaliyotokana na maagizo ya Msekwa.

Ni Rais Kikwete ambaye Novemba 2006, mara baada ya kuapishwa, alimteua Pius Msekwa, Spika wa zamani wa Bunge, kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.

Wachunguzi wa mambo wanasema uteuzi huo ulilenga kumpoza Msekwa baada ya wanamtandao wa Kikwete kumwondoa katika kiti cha spika na siyo kwamba  ulilenga kuboresha maliasili ya Ngorongoro.

Hata Msekwa mwenyewe hawezi kusema hivyo, kwa sababu anajua kuwa hana ujuzi wala utaalamu wa kusimamia kazi za hifadhi.

Taarifa zinasema Msekwa anapata posho ya Sh. 500,000 kila siku ambayo vikao vya bodi vinafanyika. Anapata gari na nyumba ya bure kila anapokuwa kwenye mikutano ya bodi huko Ngorongoro. Vikao vya bodi, kwa mujibu wa taratibu, vinafanyika mara tatu kwa mwaka.

Tuhuma nyingine dhidi ya Msekwa ni kwamba anafanya vikao “hata mara kumi” kwa mwaka na kwamba ameunda “kamati mbalimbali za ulaji” kuhalalisha matumizi ya fedha za umma.

Kutajwa kwa Msekwa ndani ya sakata hili, kunamuondoa moja kwa moja katika mamlaka ya kusimamia maadili na nidhamu ndani ya chama chake; angalau hadi hapo atakapokuwa amejiondoa kwenye tope hilo.

Katika hali ya kawaida, Msekwa akiwa makamu mwenyekiti wa chama ambacho mwenyekiti wake yuko ikulu, angepaswa kuwa anajenga chama badala ya kujihusisha na masuala ya Ngorongoro.

Kiongozi wa chama kinachokufa kila siku, alipaswa kutambua kwamba kazi yake kuu ni kuhakikisha uhai wa chama na kujibu mapigo ya wapinzani wake.

Katika mazingira ambamo mwenyekiti wa chama yuko ikulu kuendesha serikali, makamu mwenyekiti ndiye jicho la chama kwenye serikali.

Makamu mwenyekiti ndiye jicho la serikali kwa chama na ndiye jicho la rais kwa viongozi wenzake ndani ya chama.

Makamu mwenyekiti wa chama kilichopo iIkulu, ndiye mkono wa chama katika mambo ambayo yanamhusu mwenyekiti aliyeko ikulu.

Aidha, makamu mwenyekiti ndiye mwenyekiti wa kamati ndogo ya maadili – inayochambua na kuangalia mienendo ya viongozi na wanachama – mwenye jukumu la kumueleza mwenyekiti udhaifu wa kila kiongozi ndani ya chama.

Huyu ndiye mjenzi mkuu wa chama kwa niaba ya mwenyekiti. Ndiye anastahili kumueleza mwenyekiti nani mwanasiasa na nani msanii.

Akiwa kiongozi mwandamizi wa CCM, na huku akitambua kwamba serikali inayoongozwa na chama hicho nayo imepwaya, alipaswa kukipa makali chama chake, ili walau wananchi waliopoteza imani na serikali, wawe na imani na chama.

Kwa wadhifa alionao, na majukumu aliyojipa ya kusimamia nidhamu ya wenzake, Msekwa alipaswa kuwa mfano wa kuigwa ili kauli yake iwe na uzito wa kuwaaminisha mafisadi kwamba kazi inayofanywa na chama kuwaondoa ndani ya ulingo mkuu wa kisiasa, ina lengo jema la kusafisha chama na kukirejesha mikononi mwa wanachama.

Lakini katika mazingira ya sasa, ni “fisadi gani” anamwogopa au hata kumheshimu Msekwa? Fisadi gani anaweza kukemewa na Msekwa naye akatishika na kunywea?

Wakati hayo yakitendeka, kumbukumbu zinaonyesha kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alishajiapiza kwamba atahakikisha anafukuza mafisadi wote ndani ya chama, na akishawamaliza anaenda kuwang’oa walio serikalini.

Sasa, Nape ataweza kumshughulikia Msekwa anayetuhumiwa kufisidi hifadhi ya Ngorongoro? Au ataendelea kushikamana naye kuwanyoshea wengine kidole?

Mwingine ambaye yuko kwenye mtihani ni mwenyekiti Kikwete. Kama ana nia njema na mapambano haya, anatakiwa kuonyesha dhamira ya kweli.

Je, ataendelea kufanya kazi na Msekwa kwenye chama? Atapuuza tuhuma hizi na kumwacha aendelee kujihusisha na masuala ya Ngorongoro?

Je, iwapo ataamua kumuacha Msekwa akawashambulia wengine, yeye ataaminiwa na yeyote? Je, ataweza kukinusuru chama? Ataweza kujinusuru mwenyewe?

Kikwete aliyelundikiwa tuhuma dhidi ya akina Rostam Aziz, Edward Lowassa na Andrew Chenge, ataweza kusema haoni tuhuma dhidi ya Msekwa? Au atakubaliana na Msekwa kwamba tuhuma hizi ni ujinga?

Msekwa anajitoaje hapa? Anaandaaje kikao kijacho cha halmashauri kuu (NEC) ya CCM kujadili na kufukuza “magamba” ya CCM?

Je, yawezekana tuhuma dhidi ya Msekwa zimeletwa ili kumdhoofisha mbele ya kikao cha NEC cha kujadili “mafisadi ndani ya CCM?”

Kama jibu ni ndiyo, basi hazitakuwa na uzito. Kama jibu ni hapana, tutashuhudia patashika ya aina yake.

Bali Msekwa, akiwa mwanasheria, anajua vema kuwa ana haki ya kusikilizwa kabla ya kuhukumiwa. Mengine yote yanaweza kusemwa nje ya vikao.

Lakini ndani ya vikao, kila tuhuma sharti ithibitishwe na sharti Msekwa apate fursa ya kujitetea.

Ni utetezi huo ambao wananchi na wachunguzi wa mienendo ya CCM, wanasubiri kwa hamu. Je, Msekwa atafaulu kutupilia mbali “gunia la misumari” lililoko kichwani kwake?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: