Msekwa, Mukama barua za mafisadi haziandikiki?


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 27 April 2011

Printer-friendly version
Tafakuri

SITAKI kuaamini kwamba wiki tatu tu baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutamba kuwa kimefanikiwa kujivua gamba kufuatia kujiuzulu kwa Kamati Kuu na sekretarieti ya chama hicho mjini Dodoma, sasa watendaji wake wameanza kujawa na hofu.

Woga huu umeenea na kusambazwa hata na makada wa ndani ya CCM kwamba maamuzi ya kuwapa viongozi wenye tuhuma za ufisadi siku 90 wajitoe ndani ya chama hicho kwa maana ya kuachia nyadhifa zao ni mambo yasiyotekelezeka.

Habari ambazo ziliripotiwa na baadhi ya magazeti wiki iliyopita zikiwakariri viongozi watatu wa sekretariati, yaani Katibu Mkuu, Wilson Mukama; Naibu Katibu Mkuu Bara, John Chiligati na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, kwamba hawajui majaliwa ya kuandikiwa barua za kutaka watuhumiwa ufisadi wapime uzito, zinaanza kujenga picha ya hofu kwa watendaji hao kwamba huenda hakuna kitakachofanyika.

Lakini kibaya na kigumu zaidi ni kauli ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Pius Msekwa, ambaye pamoja na kujijengea heshima yake kubwa nchini kwa miaka mingi, anaanza kuonekana kama uzee unamtesa kwa kukosa busara katika kauli zake juu ya yote yanayotendeka ndani ya CCM.

Msekwa, kama viongozi wa sekretarieti walioulizwa hatima ya mafisadi na kama zimeandikwa barua za kuwataka wapime uzito kisha wajiengue kwenye uongozi, aligeuka mbogo. Alitaka vyombo vya habari eti visichokonoe habari hiyo kwa kuwa ni mambo ya ndani ya CCM.

Msekwa kwa maana hiyo alitumia ukali kukwepa kueleza barua hizo zimeandikwa au zitaandikwa lini. Kauli ya Msekwa ilionyesha dhadhiri kukerwa na vyombo vya habari kufuatilia utekelezaji wa maazimio ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM ambayo kwa mbwembwe za kutosha kabisa Msekwa, alitumia maazimio hayo kuyaweka wazi kwenye mkutano wa hadhara ambao ulifanyika mjini Dodoma kwa wanachama wa CCM kwa nia ya kuitambulisha Sekretarieti mpya.

Si hivyo tu,  Msekwa alinukuliwa na vyanzo vya habari kwamba katika kikao cha Kamati Kuu kujadili ajenda za kwenda NEC, suala la ufisadi lilipoibuka na mwenyekiti Jakaya Kikwete kutaka kujua  wanaotuhumiwa hasa ni nani, kwa kuwa tuhuma hizo zimekijeruhi mno chama hicho, ndiye alitaja majina.

Msekwa alinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari kwamba ndiye alimweleza mwenyekiti wake kuwa wanaotajwatajwa na wananchi na hata wanachama wa CCM, na akirejea taarifa alizopata wakati akiwa kwenye kamati ya kutibu mpasuko ndani ya CCM iliyoongozwa na Mzee Ali Hassan Mwinyi, ni Edward Lowassa akishikamanishwa na Richmond; Andrew Chenge akishikamanishwa na rada na Rostam Aziz akishikamanishwa na Dowans na Kagoda.

Taarifa zilizovuja zilisema kwamba pamoja na utetezi dhaifu uliokuwa umetolewa na wajumbe kama Sophia Simba, kwamba tuhuma za ufisadi ni porojo tu kwani hata hao wanaotuhumiwa kama Chenge walikwisha kusafishwa na makachero wa Shirika la Makosa Makubwa ya Jinai la Uingereza (SFO), Kikwete alikuwa mbogo na kutaka sasa wasonge mbele hatua moja zaidi.

Kabla ya mwenyekiti kusema ni hatua gani ya mbele zaidi ilikuwa inatarajiwa, habari zilivuja kuwa mjumbe mmoja, Abdulrahaman Kinana, alipendekeza wajumbe wa CC na sekretarieti wajiuzulu ili kumpa mwenyekiti fursa ya kuteua upya wajumbe ambao anaamini watamsaidia kutekeleza majukumu yake kwa kuwa waliopo tayari walikuwa wamechafuka mno kwa tuhuma.

Ninafanya marejeo haya ili kujenga hoja kwamba Msekwa anafahamu vilivyo chimbuko la CCM kujivua gamba, lakini pia anafahamu walivyoparurana ndani ya vikao; kikubwa zaidi anajua jinsi alivyotumia ripoti ya mkutano wa CC ya hoja ya haja ya kufanya mageuzi ndani ya CCM, akisoma kwa kituo suala la rushwa.

Kwa kuwa Msekwa aliona fahari, kujawa na hisia za ukada na kuona kuwa kuweka hadharani msimamo wa NEC juu ya rushwa na ufisadi kwa wanachama wake kwenye mkutano wa hadhara na hasa juu ya hatua za kuchukuliwa dhidi ya watuhumiwa wote wa ufisadi, hatuoni anakwazika nini sasa anapotafutwa na vyombo vya habari kuzungumzia suala lile lile alilokuwa amelizungumzia kwa hisia kali. Nongwa inatoka wapi? Kulioni Msekwa?

Lakini pia ni vema Msekwa akajua kuwa mambo ya CCM si ya viongozi, ni mambo ya umma, hiki ni chama tawala, maamuzi yake yanaathiri moja kwa moja serikali na wananchi wote, wawe wanachama au la.

CCM haiwezi asilani kujifanya kuwa ni chama binafsi, si kampuni ya mtu ni taasisi ya umma, ni chama kinachounda serikali, Msekwa lazima aelewe hili, hatuwezi kumnyamazia.

Hata hivyo, baada ya kutangazwa kwa siku 90 kwa makada wa CCM wenye tuhuma kali za ufisadi wapime wenyewe uzito wa tuhuma zao na kisha wajiengue kwenye uongozi, watu walijawa na hisia mchanganyiko.

Wapo walioona kuwa muda huo ni kama njia ya ‘funika kombe mwanaharamu apite’ wengine wakisema ni kosa la kiufundi, kwa sababu kama kulikuwa na ushahidi mahususi wa kuwaangamiza makada hao, hakukuwa na sababu ya kutoa muda wote huo, wangewashughulikia kwenye mkutano wa NEC.

Kwa kufanya hivyo, akina Msekwa, Mukama, Chiligati na Nape wasingekuwa na kibarua cha kupita nchi nzima kutangaza kwamba wameanza kujivua magamba kwani tayari yangekuwa yanaonekana wazi, watu wametoswa.

  Lakini kwa kuwa hadi sasa hakuna aliyetoswa kwa maana halisi ya kutoswa, na hasa tukijaribu kutazama hali ya mambo inavyozidi kugeuka kila uchao, ni haki na halali kuanza kujenga fikra kwamba hao waliodaiwa kuwa ni mafisadi wanatisha, wanaogopesha akina Msekwa, Mukama, Chiligati na Nape ndiyo maana takribani wiki tatu hakuna anayeweza kusema lolote la maana kuhusu barua hizo.

  Kelele zimekwisha kuanza kupigwa kwamba mambo yamegeuka. Akiwa mgeni rasmi kwenye tamasha la nyimbo za injili Jumapili ya Pasaka katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Rais Kikwete alisema  “… waliokuwa wananikazania kauli ya kuvua gamba sasa wamenigeuka.”

Ingawa Rais hakwenda mbali kufafanua nani hasa wamemgeuka, akiishia tu kuwashukuru viongozi wa dini kwa kumtia moyo na kumuunga mkono katika mapambano dhidi ya ufisadi, hizi ni dalili kwamba moto uliowashwa Dodoma sasa unazidi kufifia kwa kuwa ndani ya CCM kwenyewe na pengine hata serikalini, ufisadi umeota mizizi kuliko inavyoweza kuelezwa kwa maneno matupu.

Katika kikao kilichopita cha CC ilithibitisha kwamba ufisadi umekuwa tishio la uhai wa chama hicho; kimepoteza mvuto kwa wananchi kwa sababu ya ufisadi, na kimepoteza kura nyingi kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka jana kwa  sababu ya ufisadi, lakini pia kimeonyesha dhahiri kuwa kinaondosheka madarakani kwa sababu ya ufisadi.

Kwa mwelekeo huu, ni dhahiri ufisadi ni ugonjwa unaohitaji tiba kutoka nje ya CCM, inavyoelekea CCM haiwezi kujitibu yenyewe. Tusubiri tuone.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: