Msilale, CCM hawajaanza kugombana leo


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 30 March 2011

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

JUZI, wakati nikiwa maeneo ya jirani na Mlimani City jijini Dar es Salaam, nilikuwa na mazungumzo marefu na mmoja wa viongozi wa upinzani nchini.

Kiongozi huyo alikuwa na imani kwamba kwa namna mambo yanavyokwenda ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa sasa, ni wazi kuwa ni suala la muda tu kabla chama hicho kupasuka na upinzani kushika madaraka.

Kwa hiyo, wapo baadhi ya wapinzani ambao sasa wameanza kugawana vyeo (na mimi alinipa cha kwangu kama nitataka) eti kwa vile “CCM Kwisha Sasa.”

Nikamwambia aache kuota ndoto za mchana na badala yake aamke na kuanza kuchapa kazi. CCM inaweza kujinusuru kupasuka milele na itakapopasuka, pengine si katika wakati mimi na yeye tutakuwa hai.

Nikamkumbusha ya mgogoro baina ya Oscar Salathiel Kambona na Mwalimu Nyerere. Ukiondoa Nyerere, Kambona ndiye aliyekuwa mwanasiasa anayependwa na watu kuliko wengine wote nchini wakati huo. Hata staili yake ya kunyoa nywele ilikuwa ikiigwa na wananchi.

Kwa sasa, hakuna kiongozi hapa nchini anayependwa na wananchi kwa namna ambavyo Watanganyika walimpenda Kambona.

Hata hivyo, Nyerere na Kambona walitofautiana. Kwanza ilikuwa ni hatua ya Nyerere kutangaza kuwa Tanganyika itakuwa nchi ya chama kimoja cha siasa, hatua aliyoipinga Kambona.

Wakatofautiana tena wakati wa mkakati wa vijiji vya ujamaa. Nyerere na mzee Rashid Kawawa wakitaka vianzishwe haraka na nchi nzima wakati Kambona akitaka vianzishwe vichache kwanza ili vitumike kama kipimo kabla ya kuvieneza nchi nzima. Kambona akashindwa tena.

Wakahitilafiana zaidi mwaka 1967 wakati wa Azimio la Arusha. Kambona hakuwa mjamaa na alipendelea mfumo wa ubepari. Wakabishana sana katika mikutano yao binafsi na katika vikao rasmi. Ubishani ukageuka uhasama mpaka akaamua kukimbilia Uingereza na chama tawala cha TANU kikaingia katika mgogoro mkubwa.

Ulikuwa mgogoro mkubwa. Kambona alikuwa pia Katibu Mkuu wa chama hicho na hapa unazungumzia vita kati ya Mwenyekiti na Katibu Mkuu wa chama. Tena vita vyenyewe vikitokana na tofauti za kiitikadi na si masuala binafsi.

Kama mtu ataitazana CCM ya sasa (ambayo ni mtoto wa TANU), atabaini kuwa hakuna mwana CCM mwenye nguvu kwa umma kuliko alivyokuwa Kambona.

Kama CCM, wakati huo TANU, iliweza kuvuka kikwazo hicho na ikaendelea kutawala hadi leo, sidhani kama migogoro inayoibuka sasa (UVCCM Vs Sumaye na kina Samuel Sitta Vs kina Rostam Aziz), inaweza kuwa kiashiria cha chama hicho kupasuka na kuondolewa madarakani.

Mwaka 1968, TANU ilipata msukosuko mwingine mkubwa. Wabunge wake wanane wakiongozwa na Joseph Kasella Bantu na Elly Anangisye, walifukuzwa chamani. Kosa lao lilikuwa ni kuhoji nani ana nguvu kati ya Bunge na chama tawala.

Aliyekuwa Waziri Mdogo katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Richard Wambura, alizungumza bungeni na kupasua wazi kuwa chama kiko juu ya Bunge kwa vile wabunge wote wameingia bungeni kwa tiketi ya chama. “Wanaohoji wakome mara moja,” alisema.

Hatimaye kina Kasella Bantu wakatimuliwa kwenye chama. CCM ikatetemeshwa kwa sababu wabunge hao walikuwa wanaungwa mkono sana lakini bado CCM imeendelea kuwapo hadi leo na kubaki madarakani.

Na katika siku za karibuni, watu wamekuwa wakizungumzia matukio ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na rais Kikwete, kupinga hadharani mambo ya Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, kuhusu ubomoaji wa nyumba za wananchi waliojenga kwenye hifadhi ya barabara.

Lakini jambo kama hili limewahi kutokea katika enzi ya Mwalimu Nyerere. Miaka ya 1970 wakati wa kile kilichoitwa Operesheni Maduka, Kawawa alidaiwa kuvunja maduka mengi ya watu binafsi ili kila kitu kiuzwe kwenye maduka ya ushirika.

Wananchi wakalalamika na ndipo Nyerere alipoibuka na kusema: “Kiongozi yeyote anayefunga maduka ya watu binafsi kwa nguvu na kusababisha usumbufu kwa watu wasipate mahitaji; ni adui wa Ujamaa. Maduka binafsi yatakufa kifo cha kawaida vitakapotokea vyama vya ushirika makini na vyenye nguvu, vitakavyosimamiwa vizuri.”

Wakati ule hakuna aliyesema kuwa ule ulikuwa mwisho wa CCM kwa vile Nyerere ameonekana kumpinga hadharani Kawawa ambaye alikuwa waziri wake mtiifu. Pamoja na hilo, CCM iliendelea kuwapo na ipo hadi leo pamoja na kauli hizo mbili tofauti za viongozi.

Tumewahi pia kushuhudia taharuki iliyotokea wakati Horace Kolimba, mmoja wa makada maarufu wa CCM, aliposema katika miaka ya 1990 kuwa chama hicho hakina dira wala mwelekeo.

Yalikuwapo mambo ya makundi kama vile G55 miongoni mwa wabunge wa CCM na wanachama wao kuhusu kuundwa kwa serikali ya Tanganyika ndani ya muungano. Hata hivyo, changamoto hiyo haikuivunja CCM.

Kimsingi, katika kila muongo mmoja, CCM imekuwa na kawaida ya kuingia katika mgogoro kutokana na tofauti miongoni mwa viongozi au wanachama wake. Lakini mara zote, tofauti hizo humalizwa salama.

Kinachofanya sasa mambo yaonekane makubwa ni uhuru na wingi wa vyombo vya habari. Nikiri hapa kuwa pamoja na kasoro nyingine zote ambazo Kikwete anazo, serikali yake imejitahidi kwenye kuacha vyombo vya habari na watu wawe huru kujieleza kuliko katika wakati mwingine wowote tangu uhuru.

Ukitaka kujua namna kujieleza kulivyozimwa katika miaka ya nyuma, chukua mfano wa mwaka 1969. Daisy Sykes, binti wa mmoja wa waasisi wa harakati za Uhuru nchini, Abdulwahid Sykes, alitaka kuandika kitabu kuhusu historia ya baba yake.

Binti alikuwa amekasirishwa na ukweli kuwa kifo cha baba yake, kilichotokea 12 Oktoba 1968, hakikupewa uzito uliostahili na magazeti ya chama na serikali; UHURU na Nationalist yaliyokuwa chini ya uhariri wa Benjamin Mkapa.

Kwa mujibu wa kitabu cha Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes (1924-1968) cha Mohamed Said (Bwana MSA), serikali ilikataa ombi la binti huyo. Huko ndiko tulikotoka na ndiyo maana hatukusikia sana malumbano na ubishani kama tunavyouona sasa.

Ninaamini haya tunayoyaona leo yanatokana tu na aina ya uongozi na mfumo wa kidunia uliopo kwa sasa na si kwa sababu CCM imelegea kuliko kawaida.

Ushauri wangu kwa vyama vya siasa ni kuhakikisha vinaendelea na kazi ya siasa ili kujiongezea wanachama na kuonyesha uhalali wao wa kupewa madaraka.

Vinginevyo, vitakuwa sawa na ule mfano wa fisi aliyekuwa akimfuata mwanadamu kwa nyuma, akidhani mikono yake itadondoka chini ili apate chakula. Haikutokea.

www.ezekielkamwaga.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: