Msimu wa mashushu huu hapa


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 28 July 2010

Printer-friendly version

MSIMU wa mashushushu umewadia. Ni uzushi mtupu. Ni kupakazia. Ni utapeli uliokaangwa kwa mafuta masalia; chakula chake kina harufu sabini. Sasa mlaji ajue anakula nini?

Jibu ni kuacha kula chakula hicho cha harufu nyingi. Jibu ni kuwa kuku wa kienyeji: kujiparuria. Kujitafutia. Kujisikilizia. Kufikiri na siyo kutembeza bakuli la kuomba maoni.

Kwa siku nane sasa, tangu itangazwe kuwa Dk. Willibrod Slaa atagombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeoeo (CHADEMA), mashushushu wametoka usingizini.

Wameibua mbinu za kupaka matope, kulegeza mishipa ya wapambanaji, kukatisha tamaa na kuanzisha mijadala mfu ili kufunika nguvu mpya katika upinzani dhidi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Tayari wamesema Dk. Slaa ni chaguo la Kanisa Katoliki na kwamba kanisa hilo limeapa kumsaidia hadi anaingia ikulu. Kwa sasa tuuite uzushi, lakini uzushi elekezi. Tuendelee.

Siyo mara ya kwanza mashushushu, kwa kujituma au kwa kutumiwa na watawala, kuunda na kusambaza uzushi wa viwango hivyo. Wametumia mawakala maalum kwa njia ya mijadala katika mabasi, mabaa, masoko na vijiwe.

Wametumia vyombo vya habari na mimbari za makanisa na misikiti; wamepenya vikundi vya asasi mbalimbali za kijamii vikiwemo vya madhehebu mbalimbali. Wamepanda mbegu yao ambayo matunda yake ni chuki, uhasama na mgawanyiko.

Historia inatukumbusha yaliyotokea mara baada ya Watanzania zaidi ya 3,000 kukusanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam, 11 - 12 Juni 1991 na kuunda "Kamati ya Kitaifa Kupigania Mageuzi ya Mfumo wa Katiba" (National Committee for Constitutional Reform-NCCR).

Kwa siku mbili mfululizo, wananchi waliweka hoja zao wazi wakitaka kuwepo mfumo wa vyama vingi nchini na kuondokana na ukiritimba wa kisiasa.

Mashushushu walikuwepo. Walijaa kibao! Walishuhudia utulivu na jinsi hoja zilizvyojengwa. Kilichofuatia ni uzushi kuwa Kamati ya Mageuzi ni ya "Wahaya."

Hili liliposhindikana wakadai kuwa Watanzania hawana ujasiri kama huu ulioonyeshwa Diamond Jubilee, kwa hiyo watakuwa "wametumwa na serikali" kufanya hayo.

Mbegu ya mageuzi ilipomea na kuanza kukua na vyama vingi vikaanzishwa, mashushushu na viongozi wa serikali na CCM wakazunguka nchi nzima wakihubiri kuwa wale wanaotaka kuondoa ukiritimba wa kisiasa "wametumwa na mabeberu."

Wakati Mabere Marando na timu yake (akiwemo mwandishi wa makala hii), walipokamilisha mzunguko wa pili nchi nzima, kuelimisha wananchi juu ya haki yao ya kuchagua wanayemtaka na kukataa wasiyemtaka, mashushushu wakaeneza kuwa Marando alikuwa "ametumwa."

Hakika tulikuwa tumekaa pamoja na kumtuma Marando na wenzake, kupeleka ujumbe nchi nzima. Lakini mashushushu walioegemea zaidi upande wa serikali, wakijidai kuwa na "uchungu" na Kamati na baadaye NCCR-Mageuzi, walivumisha kuwa chama hicho kilikuwa sehemu ya serikali.

Ujio wa Augustine Mrema, aliyepata umaarufu kupitia chama kilichokuwa kimejengeka kwa uthabiti; kikiheshimika kwa demokrasi yake ya ndani, ulikiacha chama hoi.

Baada ya kushindwa urais, kushindwa kuendelea kuwa mbunge Temeke; kushindwa kuwafukuza viongozi aliowakuta na asiowataka au aliowaogopa na kushindwa kuhimili kishindo cha wengi, naye alianza kutukana wenzake kuwa "wametumwa na serikali kummaliza."

Waliomwona Mrema akicheza ngoma na kutupiwa visenti kwenye Mkutano Mkuu wa CCM wiki mbili zilizopita; huku akitetea chama hicho kuliko makada wake, watakuwa wamegundua kuwa hakuwa mwanamageuzi bali alikuzwa na mfumo unaoendeshwa na vitaarifa dhalili vya kishushushu.

Twende mbele. Watawala walipoona Chama cha Wananchi (CUF) kinaenea kote kisiwani Pemba; kinang'ata Unguja na kinaanza kuenea Tanzania Bara, wakasambaza sumu kuwa chama hicho ni cha "Kiislamu." Wakahubiri usiku na mchana mpaka wakaamini uzushi wao wenyewe.

Sumu hiyo imemwagwa nchi nzima; hata pale ambako wabunge wa chama hicho walikuwa waumini wa madhehebu mengine. Shabaha ni kupaka chama matope na kukiondolea hadhi ya uwakilishi kitaifa na miongoni mwa waumini wa madhehebu mengine.

Watawala walipoona CHADEMA inaanza kuibuka, baada ya ukimya wa miaka kadhaa ikijiandaa na kujiimarisha, wakasambaza kupitia mashushushu wao, kuwa chama hicho ni cha kikabila.

Mikutano ya hadhara ya CCM wakati wa kampeni za uchaguzi hujaa kejeli na madai kuwa CHADEMA ni chama cha familia moja.

Hayo yote yanafanywa hata baada ya kuona kuwa wanachama, viongozi na wabunge wa CHADEMA siyo wa familia moja. Ni kejeli. Ni uzushi unaosambazwa na mashushushu wa watawala ili kujenga sura isiyokubalika mbele ya wananchi.

Leo, CHADEMA wanasema wanamteua Dk. Slaa kuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muugano wa Tanzania. Tayari wametokea wa kudai kuwa ni pendekezo na chaguo la Kanisa Katoliki.

Lengo la madai na uvumi mkali kuhusu ukatoliki wa Dk. Slaa ni kwamba wasio Wakatoliki wajitenge naye. Waamini wa madhehebu mengine wajitenge na mgombea.

Huku ndiko kupakazia tulikozoea. Mara hii kunaweza kushindwa, tena kwa kishindo, kwa kuwa mteule wa CHADEMA yuko mbali sana na vineno, majungu na fitina za mashushushu na wanaowatuma.

Dk. Slaa ana nguvu ya kipekee katika jamii ya Tanzania. Umakini wake unamweka nje kabisa ya duara la majungu. Uthabiti wake wa kauli, unaoambatana na uchunguzi mwanana, unamtofautisha - angalau kwa kiasi ambacho tumeona hadi sasa - na mafarisayo hekaluni.
Kwake yeye, kutamka fisadi hakuhitaji dini. Kudhihirisha wizi uliotokea benki au wizarani, hakuendani na imani. Kugundua kuwa rais alisaini kitu ambacho siyo sheria iliyotungwa na bunge, hakuhusiani na madhehebu.

Imani ya CHADEMA na wananchi kwa Dk. Slaa haitokani na dini au madhehebu yake. Inatokana na kujali kwake. Ujuzi wake. Juhudi zake na nia yake katika kuleta mabadiliko.

Msomaji mmoja (simu: 0715 596929) ameniandikia, "Wakati ni huu. Nguvu za pamoja zinahitajika kuing'oa CCM madarakani. Tumieni busara na hekima; bila jazba - muongee kwa kina na CUF, tuungane Bara."

Ni ujumbe mwanana. Hataki kufuta CCM. Anataka ishindwe ili nayo ionje nafasi ya mpinzani. Inawezekana.

Dk. Slaa ana uwezo wa kuongoza wananchi na kuwafikisha mahali hapo. Tutaona wengi wa kuunga mkono safari hii - kuanzia wazazi, wanafunzi, wasomi, wafanyakazi, waumini na wasio waumini.

Hata viongozi wa madhehebu mbalimbali wanajua kuwa kuunga mkono safari ya ukombozi duniani ni kuandaa ukombozi wa mbinguni. Ni kazi ya kila mmoja.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: