Msitu wa Pande kama Msitu wa Ngong


Nyaronyo Kicheere's picture

Na Nyaronyo Kicheere - Imechapwa 04 July 2012

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

KULE Kenya kuna eneo maarufu sana linaloitwa Msitu wa Ngong. Msitu huu ulipata umaarufu hapo awali kwa ufugaji na ufundishaji wa farasi wa kushiriki katika mashindano ya mbio na michezo mbalimbali inayoshirikisha farasi.

Umaarufu huo ndio ulioleta msemo wa “anakwenda kasi kama farasi wa Ngong.” Baada ya uhuru wa Kenya mnamo mwaka 1963 Msitu wa Ngong ulibadilishwa matumizi na kuwa eneo la mateso na mauaji ya watu wanaoonekana hatari kwa utawala wa Jomo Kenyata na baadaye Daniel arap Moi.

Msitu wa Ngong ndiko ulikokutwa mwili wa mbunge wa Kiambuu, Joshua Mwangi Kariuki maarufu “JM” baada ya kutoonekana hadharani kwa siku tatu hivi. Msitu wa Ngong ndiko pia ilikoanguka ndege iliyoanguka na kusababisha vifo vya mawaziri George Saitoti na msaidizi wake aitwaye Ojode.

Katika miaka ya 1990 iligundulika kuwa mtu wa mwisho kuonekana pamoja na hayati Kariuki alikuwa Peter Kinyanjui au Mark Twist ambaye alihamia Tanzania kisirisiri akapata pasipoti ya Tanzania na kufanya kazi nyingi tu ya mwisho ikiwa Makamu Mwenyekiti wa Chama Soka Tanzania (FAT).

Hata hivyo, Kinyanjui alifanya makosa mwaka 1994 pale alipoingilia mambo ya klabu maarufu nchini ya Yanga, ambao kupitia kwa polisi namba wani wa wakati huo, Mzee wa Kiraracha, Augustine Lyatonga Mrema walimtimua nchini akarejeshwa kwao Kenya ambako eti serikali ilisema ilikuwa haimtafuti!

Yaani huyu ndiye mtu wa mwisho kuonekana na hayati Kariuki na hadi leo mauaji yake hayajatatuliwa kwa maana kwamba hajapatikana mtu aliyesababisha kifo chake, na bado serikali inasema haimtafuti? Lakini kabla hajaondoka yaelekea aliwafundisha Watanzania namna ya kutekeleza mambo kama yanayofanyika Msitu wa Ngong.

Mambo yasiyofaa kama yale ya Msitu wa Ngong ndiyo yanafanyika katika Msitu wa Pande uliopo nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam. Na hata Msitu wa Ngong upo nje kidogo ya jiji la Nairobi.

Inavyoelekea watesaji wa Watanzania hawakuhitimu kama wenzao wa Kenya. Wakenya wakimchukua au kumteka mtu, hupatikana baada ya siku tatu au nne katika Msitu wa Ngong akiwa maiti, hawamwachi akiwa hai akielezea jinsi alivyong’olewa meno na kunyofolewa kucha!

Kwa mara ya kwanza Msitu wa Pande kuvuma ilikuwa mwaka 2006 ilipoelezwa na polisi jinsi wafanyabiashara watatu na dereva wa teksi mmoja “walivyopambana na askari kwa kurushiana risasi na hatimaye watu wale wanne kuuawa”.

Kwa mujibu wa polisi, mapambano hayo yaliyotokea katika Msitu wa Pande, yalikuwa makali na yalidhihirisha jinsi polisi walivyo na shabaha maana kila mmoja alipigwa risasi kisogoni. Mapambano hayo pia yanaonyesha mbinu za medani za polisi wanavyoweza kumpiga risasi kisogoni, bila kukosea, mtu wanayepambana naye wakitazamana uso kwa uso.

Ukweli wafanyabiashara wale, walitekwa Sinza kisha wakaporwa fedha na madini halafu wakapelekwa katika msitu wa Pande ambako waliuawa kwa kupigwa risasi ili kupoteza ushahidi.

Huko ndiko mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka aliokotwa na wasamaria wema akiwa nyang’anyang’a, kapigika, hajitambui na hatambuliki.

Waliofanya shughuli ile ya kumpiga, kumg’oa meno na kumvunja mikono na mbavu hawakufanya kazi vizuri kwani walimwacha hai tofauti na inavyofanyika Kenya, na sasa Dk. Ulimboka amepata nafasi ya kudokeza kilichotokea kabla, wakati wa kipigo chenyewe na baada ya kipigo hicho.

Kulingana na taarifa za magazeti, redio na televisheni, Dk. Ulimboka anasema kuwa alipigiwa simu na mtu ambaye wamekuwa wakikutana naye katika mazungumzo ya kumaliza mgomo. Akiwa na rafiki yake Dk. Deo Michael wakaenda kukutana naye na kwamba wakati wanazungumza walifika watu wapatao watano wakidai wanamtaka yeye tu na wakaondoka naye kwa mikiki.

Huko akapigwa kwanza ndani ya gari na baadaye katika Msitu wa Pande, ambako ndiko alikokutwa asubuhi akiwa hoi bin taaban. Madaktari wenzake wanasema kavunjwa mbavu, mikono na taya. Pia kang’olewa meno mawili ya mbele na kunyofolewa kucha.

Sasa viongozi wanasema hawahusiki na tukio hilo lakini “waathirika” wanasema wanamjua mhusika. Hakuna anayemtaja mbele za watu mhusika huyo ni nani, lakini kwenye vijiwe, kila mtu anataja kuwa serikali inahusika na kwamba wahusika ni Kijitonyama.

Ukiuliza Kijitonyama ni nani, wanasema ni wenyewe hao hao serikali. Kiongozi wa nchi kasema serikali haihusiki lakini yaelekea raia hawamwamini na hawaiamini serikali kuwa haihusiki. Lakini mng’oaji meno, mvunjaji mbavu, mikono na mataya atakuwa nani na kwa nini?

Na kwa nini mtu mwenyewe anayevunjwa mikono, mbavu na taya ni yule tu mwenye ugomvi na serikali? Kama ni kweli waliompiga Dk. Ulimboka, wakamvunja taya, mikono, mbavu na wakamnyofoa kucha walikuwa wakimhoji eti “nani wanakutumia kuongoza migomo,” je, ni nani hao wapigaji?

Kitendo cha madaktari kukataa mchango wa serikali kwa ajili ya matibabu ya Dk. Ulimboka ni ishara tosha kuwa wanaamini serikali ndiyo inahusika katika kutoa kipigo kwa mwenzao. Swali ni, je, serikali itajinasuaje katika tuhuma hizi mbaya?

Dawa ni moja tu, Rais Jakaya Kikwete aunde tume huru kubainisha ukweli na kuhakikisha mtuhumiwa wa mateso kwa Dk. Ulimboka anapatikana na kufikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.

Bila kupatikana mtu huyo anayenyofoa watu kucha na kung’oa meno bila ganzi, serikali haitaaminika tena. Tukio hili limeipaka matope serikali na kuifanya ionekane ni ya watesaji wakubwa.

Tatizo letu ni kufanya mafunzo kwa Kiingereza wakati watu wenyewe hawajui Kiingereza na walimu wao pia hawajui Kiingereza. Watu walioiva nusunusu ndio hufanya kazi zao nusunusu.

Watu wangesoma kwa Kiswahili huku walimu wao nao wanakijua Kiswahili kikamilifu wangeiva katika mafunzo yao. Kadhalika wanafunzi kusoma kwa Kiingereza wakati walimu wao hawajui Kiingereza na wanafunzi ndio kabisa wanajua Kinyakyusa, Kisukuma, Kikurya na Kizaramo ndiyo chanzo cha elimu kushuka.

Hakuna tunachopatia katika matendo yetu kama Watanzania iwe kwenye uchumi, kwenye elimu, sekta ya habari, uchunguzi, utawala na hata kwenye utesaji tunaboronga na kuacha nyuma ushahidi kuwa mtesaji ni nani hata kama hakuna anayemteja mtesaji huyo wala kukiri kumfahamu.

Ushauri wa bure ni kwa kila mtu asiyeweza kuhimili kung’olewa meno na kunyofolewa kucha bila ganzi ajitoe kwenye kundi linalopingana na Jamhuri yasije kumkuta yaliyomkuta Dk. Ulimboka.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: