Mtandao wa JK wadaiwa kuchota mabilioni BoT


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 11 June 2008

Printer-friendly version
Mkapa ashika kichwa, alalama
Makampuni yaliota kama uyoga
Rais  Jakaya Kikwete

MSULULU wa makampuni yaliyokwapua mabilioni ya shilingi kutoka Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) ya Benki Kuu (BoT), unadaiwa kunufaisha kampeni za Rais Jakaya Kikwete, MwanaHALISI limeelezwa.

Taarifa zilizopatikana jijini Dar es Salaam wiki hii zimeeleza kuwa makampuni hayo, yaliyoanzishwa kwa kasi, yalilenga kujinufaisha, lakini pia kubeba mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), jukumu ambalo lilifanikiwa.

Mtoa habari wa ndani aliliambia mwanaHALISI kuwa mpango wa kuotesha makampuni kama uyoga, na kufanikiwa kuchota Sh. 133 bilioni, ulibuniwa na baadhi ya viongozi wa mtandao wa Kikwete baada ya kuona kwamba hawakuwa na fedha za kuendesha kampeni.

Imeelezwa kwamba mpango huo ulipata baraka za aliyekuwa rais, Benjamin Mkapa baada ya kukutana na wanamtandao na kujadiliana nao juu ya mapungufu yao na jinsi ya kupata fedha.

"Baada ya Mkapa kukataa mapendekezo ya baadhi ya viongozi wenzake ndani ya chama na kuamua kuwa Jakaya Kikwete ndiye alikuwa anahitajika kugombea, mzigo wa kupata fedha za kuendesha kampeni ulikuwa umemwangukia," ameeleza mtoa habari.

Kuna madai kwamba Mkapa alikubaliana na wanamtandao juu ya kupata fedha na kuwaelekeza kwa Gavana wa BoT, Daudi Ballali ambako uliandaliwa mpango mzima wa kupata fedha kwa njia ya kuuziana madeni katika akaunti ya EPA.

Mfumuko wa taarifa kuhusu jinsi fedha zilivyopatikana unatokana na baadhi ya wanamtandao kutoridhika kwa kuachwa nje ya duara la madaraka na bila kuona uwezekano wa mabadiliko katika miaka miwili na nusu ya utawala wa Kikwete.

Hii ni mara ya kwanza kwa tuhuma nzito namna hii kutolewa dhidi ya mtandao wa Kikwete ingawa baadhi ya wanamtandao mmojammoja wamekuwa wakitajwa kwenye orodha ya "mafisadi" iliyotangazwa na vyama vya upinzani tarehe 15 Septemba mwaka jana.

Kifo cha Ballali ambacho kilitanguliwa na usiri mkubwa wa serikali juu ya mahali alipo, afya yake na iwapo anahitajika kujibu hoja juu ya mabilioni ya shilingi yaliyokwapuliwa, kinachukuliwa kuwa msiba mkubwa kwa waliotaka kujua zaidi mtandao wa wizi ndani ya BoT.

Kwa mujibu wa kalenda ya matukio, uteuzi wa mgombea ndani ya CCM ulifanyika Mei 2005 na kampeni zilianza Agosti mwaka huo. Ingawa mtoa habari hakusema ni lini hasa wanamtandao walikutana na Mkapa, inasadikika kuwa ilikuwa siku chache kabla kampeni kuanza.

Kulingana na taarifa ya maodita wa Delloite & Touche wa Afrika Kusini, waliokagua hesabu za akaunti ya EPA kabla ya kunyang'anywa kazi hiyo, makampuni 12 yaliingia makubaliano kati ya tarehe 10 Oktoba na tarehe 3 Novemba 2005.

Makampuni mengine matano (5) yaliingia makubaliano siku moja, tarehe 19 Oktoba 2005 wakati mengine manne (4) yaliingia makubaliano tarehe 18 Oktoba mwaka huohuo. Mikataba yote ilisainiwa mbele ya kamishena wa kiapo B.M. Sanze.

Ni kasi hii iliyowastua maodita wa Delloite & Touche, kuwafanya watilie mashaka makubaliano hayo kufanyika haraka kiasi hicho; na katika ripoti yao kueleza waziwazi kuwa kulikuwa na chembechembe za udanganyifu.

Kilichowastua zaidi maodita ni kuona makubaliano yote yanasainiwa Dar es Salaam na hata marekebisho yaliyohusu kampuni iliyosemekana kuwa Ulaya, yalifanywa katika siku mbili tu.

Barua ya tarehe 4 Septemba 2006 kwenda kwa Ballali, ikiwa imesainiwa na Samuel Sithole aliyekuwa kiongozi wa maodita, inatilia mashaka kasi ya kutia saini mikataba na kusema ingekuwa vema kuchunguza katika Idara ya Uhamiaji kuona kama kweli wenye makampuni walisafiri kutoka Ulaya hadi Dar es Salaam katika muda mfupi namna hiyo.

Wasiwasi mkubwa ulionyeshwa kwa kampuni ya Kagoda Agriculture Limited ambayo ilionyesha kuwa nchini Ujerumani wanalipa kwa kutumia fedha za Euro lakini BoT ikawasahihisha na kuwaambia waweke Deutshe Marks.

Mshangao wa maodita wa Delloite & Touche unatokana na kuona kuwa sahihisho hilo lililohusu Kagoda na ambalo lilihitaji watu kwenda Ujerumani au kutoka Ujerumani kuja nchini lilifanywa katika saa 48 tu.

Vyama vya upinzani na watu binafsi wamekuwa wakidai kuwa fedha zilizokwapuliwa BoT zilitumika katika uchaguzi mkuu wa 2005 na kwamba Timu ya Rais ya Kufuatilia makampuni yaliyohusika katika wizi huo ni "kiini macho."

Katika hatua nyingine, taarifa zimemnukuu kiongozi wa juu katika CCM akisema, "Hatuwezi kuendelea kuchota BoT." Alikuwa akijibu hoja iliyotolewa na mmoja wa viongozi wa Kamati Kuu (CC) kwamba Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) itafute fedha, hata kuomba BoT ili kuendesha kikao cha NEC kilichokuwa kifanyike Dodoma mwezi uliopita.

Kikao cha NEC kinatafuta kujadili hoja zilizowasilishwa na Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu kwenye kikao kilichopita ambacho kilifanyika Butiama, mkoani Mara, mwishoni mwa Machi.

CCM ilionyesha nguvu na ufahari wa aina yake wakati wa uchaguzi mkuu wa 2005 ambapo nchi nzima ilifurika fulana, kapelo, khanga, mabango, vipeperushi, matangazo katika magazeti, redio na televisheni na magari ya chama na mengine binafsi ya kifahari yaliyokuwa yakipishana kama siafu.

"Nakwambia, hakuna awezaye kuthibitisha kuwa fedha hizi zilikuwa za chama. Kwanza hatukuwa na fedha za kufaya kufuru ya aina hii," ameeleza mmoja wa viongozi waandamizi wa CCM.

Kiongozi huyo alisema kulikuwa na vurugu ndani ya chama wakati wa uchaguzi. "Kulikuwa na makao makuu mawili – Ofisi ndogo ya Mtaa wa Lumumba na Upanga ambayo yalikuwa makao ya mtandao; kulikuwa na sekretariati mbili na maelekezo kutoka kambi mbili, kabla na baada ya Kikwete kupitishwa kuwa mgombea," ameeleza mtoa habari.

Hata hivyo MwanaHALISI limeelezwa kuwa siyo viongozi wote ndani ya CCM wanajua mpango wa kukwapua fedha kutoka BoT.

Kiongozi mmoja ameliambia gazeti hili, kwa kutaka ajina lake lisitajwe, kuwa kuna wakati kiasi kilichochukuliwa benki kilimstua hata Mkapa.

"Walipomwambia kuwa Sh. 133 bilioni ndizo zimechukuliwa kutoka BoT, Mkapa alistuka, akashika kichwa kwa mikono miwili na kuuliza, ?Fedha zote hizo za nini?" ameeleza mtoa habari.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: