Mtanzania anachukuliwaje?


editor's picture

Na editor - Imechapwa 02 November 2011

Printer-friendly version

MIGOGORO ya ardhi inaongezeka nchini. Wananchi wanajikuta hawana haki ya kutumia ardhi ndani ya nchi yao huru.

Wanatishiwa maisha, wanapigwa na mwishowe, wanafukuzwa kwenye maeneo waliyohamia kwa miaka hata 30. Utamaduni mbaya kabisa.

Hofu yao inazidi kuwa kubwa kutokana na kauli za viongozi wakuu hasahasa rais wa jamhuri na waziri mkuu ambao, waziwazi wanasikika wakitetea wawekezaji, wakiwemo wagani, badala ya kusaidia raia wanaowaongoza.

Alipokuwa akizindua Ukanda wa Uwekezaji wa Ziwa Tanganyika, wiki iliyopita, Rais Jakaya Kikwete alisema wawekezaji wasiguswe. Wanahitajika kwa ajili ya kukuza uchumi.

Rais akahimiza wananchi wa Tanzania wasiogope wawekezaji wala kuwatishia usalama wao. Washirikiane nao maana wamekuja kusaidia nchi yao.

Rais na Waziri Mkuu Mizengo Pinda sasa wapo mkabala mmoja na wawekezaji. Kauli zao kwa wananchi hazivutii; haziwalengi wao moja kwa moja na nafasi yao ya haki ya kufaidi matunda ya uhuru nchi kwao.

Kuna mgogoro wa ardhi Bonde la Kiru wilayani Babati; mgogoro kwenye mashamba ya Kapunga, Mbarali; na ule wa Loliondo haujafa.

Wiki mbili zilizopita, wakazi wa eneo la Kunduchi Mtongani, mkoani Dar es Salaam, walishuhudia makazi yao yanavunjwavunjwa na wanajeshi wa serikali.

Siku chache zilizopita, Watanzania wameshuhudia mgogoro mwingine wa kipuuzi eneo la kijijini Njedengwa, katika manispaa ya mji wa Dodoma.

Taarifa za Njedengwa zinasema mwekezaji anayetakiwa na serikali alituma watu wa miraba minne na magreda nyuma yao ili kuvunjavunja makazi ya wananchi. Hapo ilikuwa ni alfajiri ya mungu watu wakiwa wamelala.

Bila aibu, Polisi waliobeba silaha wamesimamia operesheni ya kutimua wananchi kutoka vitandani mwao kwa vipigo na kuwatoa nje ili “wamiliki” wasawazishe eneo lao.

Operesheni ikaendeshwa huku mabaunsa wakipondaponda raia kama siafu. Kisa nini? Wananchi wanaishi katika eneo wasilolimiki. Mwenyewe nani? Mwekezaji anayetaka kujenga shule ya vidudu.

Matukio yote haya yanajenga taswira kwamba Serikali ya Tanzania imeshindwa kusimamia haki za wananchi bali imeamua kula sahani moja na wenye fedha.

Utamaduni wa kudharau wananchi haufai. Ni muhimu viongozi wa ngazi zote watambue kuwa wananchi wakichoka watachukia. Serikali inapopalilia chuki, itahimili matokeo yake?

Yapasa iamue sasa kuwa katika mipango yake yote, lazima izingatie kaulimbiu mpya – “mwananchi kwanza.”

0
No votes yet