Mtatiro: Nitarejesha makali ya CUF


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 22 December 2010

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii

MIONGONI mwa wanasiasa vijana waliopo nchini kwa sasa, Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro, ana historia ya kipekee.

Katika umri wa miaka 28 alionao, tayari amekutana na masaibu mazito kutoka serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM); amewekwa gerezani, amekuwa kiongozi wa wanafunzi wote wa vyuo vikuu nchini na ameachishwa shule takribani mara sita kwa sababu ya kutetea haki za wanafunzi wenzake.

Hivi sasa ameweka historia mpya ya kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF, mwanasiasa kijana zaidi katika historia ya chama hicho kuwahi kushika nafasi ya juu tangu kianzishwe takribani miaka 18 iliyopita.

Je, aliitarajia nafasi hiyo; Mtatiro anajibu, “Kwa kweli nilishtuka kidogo wakati chama kilipotangaza kunipa unaibu katibu mkuu. Ndani ya chama chetu kuna wanasiasa wakomavu na wenye uwezo ambao wangeweza kushika wadhifa huu bila ya matatizo yoyote.

“Hata hivyo, hiyo haimaanishi kwamba nimepewa viatu vikubwa kuliko miguu yangu. Ninaimudu nafasi hii na Watanzania wasubiri kuona nguvu ya CUF katika kipindi kifupi kijacho,” anaeleza kwa kujiamini katika mazungumzo na MwanaHALISI ofisini kwake jijini Dar es Salaam wiki hii.

Anasema huu ni wakati wa vijana kushika hatamu ya harakati za kisiasa duniani kote na uamuzi huo wa chama chake umeonyesha namna kilivyo na imani na vijana kama kundi la jamii lenye ushawishi mkubwa.

Mtatiro anasema ingawa alifuatwa na vyama vingi mara baada ya kuhitimu masomo yake ya Chuo Kikuu miaka miwili iliyopita, lakini aliamua kujiunga na CUF baada ya kuridhika na mwenendo wake.

“Mimi sikutaka kujiunga na vyama kwa kufuata mkumbo. Niliamua kwa makusudi kabisa kufuatilia kwa karibu mienendo ya vyama vyote vya siasa vilivyopo nchini ili nijiunge na kile kinachoendana na mitazamo yangu ya kisiasa.

“Sikutaka kujiunga na chama ambacho maamuzi hufanywa na wachache. Chama ambacho kitanifurahisha kuwa mwanachama wake lakini kisitimize malengo yangu. Nikaona CUF ndiyo chenyewe na nikajiunga nacho,” anasema.

Mwanasiasa huyu anaamini kuwa uongozi ni kipaji ambacho mtu huwa anazaliwa nacho na ndiyo maana wengi wa viongozi mbalimbali wa kitaifa waliopo sasa wana historia ya kuwa viongozi tangu wangali shuleni.

“Chukulia kwa mfano mimi, tangu nianze shule nimekuwa kiongozi kuanzia shule ya msingi. Mwaka wa kwanza wa masomo yangu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) nikawa mbunge.

“Baadaye nikawa Waziri wa Mikopo wa Serikali ya Wanafunzi UDSM (DARUSO) kabla ya baadaye kuwa Waziri Mkuu wa serikali hiyo.

“Mwishowe nikaja kuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Nchini (TAHLISO), nafasi iliyoniwezesha kuwa kiongozi wa wanafunzi karibu laki moja nchini kote.

“Huwezi ukawa kiongozi  wa wanafunzi nchini ambao kimsingi wana uelewa mkubwa na wapembuzi wa mambo kuliko wananchi wa kawaida na halafu ukashindwa kuwa kiongozi wa chama,” anasema.

Hata hivyo, Mtatitiro ambaye kabla ya wadhifa wake wa sasa alikuwa Mkurugenzi wa Masuala ya Haki za Binadamu wa CUF, anasema kuna tofauti ndogo baina ya uongozi wa wanafunzi na ule wa vyama vya siasa.

“Tofauti kubwa ipo kwenye aina ya watu unaowaongoza. Kwenye vyuo vikuu, unahitaji kueleza kidogo tu na ukaeleweka. Kwa wananchi unahitaji kueleza tena na tena ili ueleweke. Uelewa uko tofauti,” anasema.

Akizungumzia changamoto zilizoko mbele yake, Mtatiro amesema huwa anaumizwa sana na propaganda zilizoenezwa kuihusisha CUF na uislamu na kusema wananchi wanahitaji kueleweshwa zaidi.

“Hakuna udini wowote CUF. Mimi hapa ni mkristo na nimepewa wadhifa huu huku nikiwa na mwaka mmoja tu ndani ya chama. Mwenyekiti wangu, Profesa Ibrahim Lipumba, amechaguliwa kwa sababu ya uwezo wake na si dini yake.

“Hata Maalim Seif ni Katibu Mkuu kwa sababu ya uwezo wake. Huu udini ni propaganda tu ya CCM na vyombo vyake vya propaganda ndiyo vimeueneza.

“Cha ajabu ni kwamba, CCM iliyokuwa ikieneza propaganda hizi chafu za udini, yenyewe ilikuwa na viongozi wa juu watatu wa dini moja. Lakini yenyewe haikusema ni udini, ila kwa CUF ni nongwa,” anasema.

Kuhusu majukumu yake, Mtatiro anasema anataraji kuimarisha mahusiano baina ya CUF na vyombo vya habari, aliyosema hayakuwa mazuri kwa vile dola iliona CCM haiwezi kukaa madarakani iwapo chama chake na waandishi wa habari watafanya kazi pamoja.

“Vyombo vya habari vina nguvu sana lakini kwa bahati mbaya CUF haijafaidika sana na nguvu hiyo, na hiyo ni kwa sababu mfumo ulitaka iwe hivyo. Nitajitahidi kulibadili hilo kwani kwa sasa wananchi na mfumo nao unabadilika,” anasema.

Katika kipindi cha mwaka mmoja ujao, Mtatiro anasema ataelekeza nguvu zake nyingi kwenye suala zima la mabadiliko ya Katiba, anayosema ndiyo kiini cha matatizo yote yanayoikumba nchi kwa sasa.

Anasema CUF kitafanya kila iwezalo kuhakikisha serikali inasikiliza kilio cha wananchi kutaka Katiba mpya; ambayo itatengenezwa kwa matakwa yao na kwa maslahi ya taifa.

“Na niseme mapema kuwa katika hili, kama noma na iwe noma. Nitafanya chochote kile ambacho chama changu na wananchi wataniagiza kufanya. Ni lazima katiba mpya itengenezwe katika mazingira ya amani na si lazima watu wauawe kwanza kama Kenya ndipo serikali idai ni sikivu,” anasema.

Mtatiro alizaliwa mwaka 1982 katika kijiji cha Kiabakari, Musoma Vijijini katika familia ya watoto 14 wa Mzee Charles Marwa na Mama Paschalia Nyamtondo.

Alipata elimu ya msingi katika shule ya Kiabakari na sekondari ya awali aliipata katika shule ya Kiagata huku akipata masomo ya kidato cha tano na sita katika shule ya Ifakara maarufu kwa jina la Machipi.

Alipata shahada yake ya kwanza katika ualimu na elimu ya siasa na utawala UDSM kati ya mwaka 2004 hadi 2008 ambako ndiko hasa alikopata misukosuko na uzoefu wa siasa za kitaifa.

“Nilifukuzwa chuo kikuu na kurejeshwa takribani mara sita kwa sababu ya kuhusika katika kila suala lililohusu wanafunzi.

“Kwa wanaokumbuka, ni wakati wa kipindi changu cha uongozi ndipo wanafunzi walipoandamana kwa ajili ya kupinga kupanda kwa bei ya bidhaa muhimu pamoja na nauli.

“Niliongoza pia maandamano kupinga mauaji yaliyotokana na uchaguzi mkuu wa Kenya wa mwaka 2007. Haya si mambo ambayo wanafunzi wa Tanzania hupenda sana kujihusisha nayo lakini chini yangu walijihusisha sana,” anasema.

Mtatiro ambaye bado hajaoa, hupenda kujisomea, kuangalia filamu za kijasusi na kufanya mazoezi katika wakati wake wa mapumziko.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: