Mteketa: Tatizo CCM tunaoneana haya


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 14 December 2011

Printer-friendly version

“SIKUWAZA kama ningekuwa mbunge. Kutokana na unafiki, majungu, wivu na fitina zilizojikita kwenye ulingo wa kisiasa, binafsi sikufikiria kwamba ninaweza kujitumbukiza katika ulingo huu wa kisiasa. Ni kwa sababu, kwenye siasa kila mtu anapanga mkakati wa kumharibia mwenzake.

“Lakini ni fitina hizo zilizoninufaisha baada ya baadhi ya watu kunishawishi kuingia kwenye kinyang’anyiro cha ubunge mwaka 2010 na hatimaye nikafanikiwa kushinda.”

Ndivyo anavyoeleza Abdul Rajab Mteketa, mbunge wa Kilombero kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM). Katika mahojiano yake wiki hii, pamoja na mambo mengine Mteketa anasema, “Sasa nimeweza kufahamu mengi na kuelewa mengi pia kuhusu siasa.”

Anasema mwaka mmoja wa ubunge wake, amejifunza mambo mengi ikiwamo kazi nzito ambayo mbunge anayo.

Miongoni mwa anayotaja, ni baadhi ya wananchi hasa kutoka kwenye jimbo la mbunge husika, kuweka matarajio yao yote ya maisha kwa mbunge wao. Kutokana na hali hiyo, Mteketa anajitambulisha kuwa ni miongoni wabunge wanaounga mkono hoja ya ongezeko la posho za vikao vya Bunge kutoka Sh. 70,000 hadi Sh. 200,000.

Anasema “Ni muhimu na ni vema fedha za posho kwa wabunge zikaongezeka. Nichukue nafasi hii, kumuomba mheshimiwa Rais (Jakaya Kikwete) aidhinishe haraka posho hizi.”

Anadai tofauti na watu wanavyofikiria, sehemu kubwa ya fedha za posho wanazolipwa wabunge zinatumika kusaidia jamii; mbunge hubaki na kiasi kidogo sana kwenye fedha hizo.

“Wanaopinga posho hizi, ni wale wanafiki. Watu wanashindwa kuelewa, kuwa ni vigumu kwa mbunge kuishi kwa Sh. 70,000 pale Dodoma. Spika (Anne Makinda) anajua namna ambavyo wabunge wake wanavyohangaika, ndiyo maana anapambana kuhakikisha fedha hizi zinalipwa,” anaeleza.

Anasema, “Nyumba ya kulala yenye hadhi ya mbunge unaweza kukuta ni Sh. 50,000 hapohapo kuna kula, usafiri wa ndani, kumbuka kuna kumlipa dereva ili apate kula na malazi, yote hiyo ni gharama wakati posho ni Sh. 70,000.”

Mbunge huyo ambaye ni mara yake ya kwanza kuingia bungeni anasema kiasi hicho cha fedha, hakitoshi na kwamba sharti serikali ikiongeze ili wabunge waweze kutenda kazi zao vyema.

“Wanaobeza posho hizi hawana nia njema na wabunge. Hawa wanataka wabunge wawe masikini. Hili ni jambo ambalo haliwezi kukubalika,” anasema.

Anasema, “Bahati mbaya sana baadhi ya wanaopinga posho hizi ni wabunge wenzetu, wengine wanatoka ndani ya chama tawala. Huu ni unafiki na hauwezi kuvumiliwa.”

Alipoulizwa kama mshahara wake wa ubunge hauwezi kusaidia kuziba mabonde kwa pale palipopungua, Mteketa alijibu, “…jamani wabunge wenu hatuna kitu.” Anahoji, “Unadhani tunalipwa fedha nyingi? Hapana!”

Akizungumzia upatikanaji wa ajira, Mteketa anasema pamoja na matatizo yaliyopo, ni muhimu serikali ikajikita katika kutafuta ajira mpya; serikali ijitahidi kukusanya kodi ili iweze kujiendesha kwa ufanisi.

“Kwa Mheshimiwa kama Kardinali Pengo (Mwadhama), nadhani angeanza kuweka utaratibu wa kulipa kodi na kuhamasisha mashirika mengine ya dini kulipa kodi kama kweli tunataka kuwaonea huruma wananchi,” anasema na kuongeza:

“Pengo amezungumzia umuhimu wa kuwa na Katiba inayohitajika na Watanzania wote kwa wakati, lakini alikemea kile anachokiita ‘ubinafsi wa wabunge’ kwa namna wanavyotaka kujiongezea posho kwa kile kinachoitwa maisha magumu kwa waheshimiwa hao wanapokuwa Dodoma.

“Viongozi wa dini zote wana msamaha wa kodi, na hili pia linawaumiza wananchi maana watu wasiangalie tu posho za wabunge. Viongozi wa dini wana misamaha na wanaingiza magari ya kifahari mpaka unashangaa, leo posho za wabunge imekuwa sababu?”

Kwa upande wa pili wa shilingi, anasema chama chake cha CCM, kimetawaliwa na urafiki unaosababisha unafiki wa kuoneana haya kwa tuhuma nzito za kifisadi.

“Serikali iwe makini inavyofanya kazi. Waliochuma fedha za nchi isivyo halali warudishe. Kuna ufisadi kwenye madini, watuhumiwa wanajulikana, tumeona hapa mikataba mibovu ya gesi na rada, Richmond. Fedha nyingi inapotelea huko na watu wanashindwa kuchukua hatua,” anasisitiza mbunge huyo akielezea mianya inayopoteza mapato ya Serikali.

Anasema mbunge ana kazi kubwa na si vema akalala na njaa. “Waone tu wamevaa suti. Wengi wetu hawana fedha kama wabunge wa Burundi na Kenya ambako wana maslahi zaidi. Sisi kaposho kidogo tu, kelele nyingi.”

Anasema fedha inayoibwa kwenye mikataba ni nyingi na kwamba posho hiyo ni kama kumhamasisha mbunge kufanya kazi kama anavyopewa ama mfanyakazi wa kawaida au kocha wa timu, nyumba, gari na mshahara mzuri.

Anasema: “Wabunge wengi choka mbaya. Leo hii tukienda bungeni na kupiga kura ya siri juu ya posho, naamini asilimia zaidi ya 90 watasema tunataka kuongezewa. Ukipata kidogo unagawana na wapiga kura, hakuna kitu.”

Mteketa anaonya kwa baadhi ya watoa hoja juu ya posho hizo akisema: “Tusipotoshe wananchi. Tuache malumbano kwani kama ni suala la ubadhilifu, basi uangaliwe zaidi huko kwenye halmashauri zetu na ofisi za umma.

“Tatizo CCM tunaoneana haya, tunalindana, wanaogopa kuumbuana. Imefika wakati sheria ichukua mkondo wake.” Akielezea majukumu jimboni kwake, Mteketa anasema hadi sasa amezunguka theluthi mbili ya jimbo lake kukagua shughuli mbalimbali za maendeleo tangu achukue jimbo mwishoni mwa mwaka jana.

“Jimbo la Kilombero ni kubwa, lina zaidi ya wakazi 400,000. Idadi hiyo ya watu ni sifa tosha kuligawa jimbo hili,” anasema Mteketa ambaye ni mchezaji wa zamani wa klabu za Simba na Yanga.

Kwa kipindi cha mwaka huu tu, Mteketa anatamba kwamba amehamasisha michezo hasa soka na netiboli kwa kutoa jezi za soka 40 na mipira 35 katika kata 23 za jimbo hilo. Pia ametoa jezi kwa timu nne za netiboli.

Anadai kwamba ametoa shuka 350 katika hospitali za Ifakara, Kibaoni na Mlimba huku akiboresha mitaa na miundombinu katika mji wa Ifakara.

Katika hilo la miundombinu, anakwenda mbali akisema kwamba kabla ya 2015 kuna uwezekano wa kujengwa kwa daraja mto Kilombero kwa sababu mchoro wake umekamilika. Daraja hilo linaunganisha wilaya za Kilombero na Ulanga.

“Fedha Sh 5 bilioni zipo kwa ajili ya mradi. Daraja hili litasaidia kuongeza kasi ya uwekezaji maana tafiti zinaonyesha kuwa jimbo langu lina uwezo wa kuzalisha mchele na kulisha nchi nzima na kuuza wa ziada,” anatamba.

Upande wa maji, kwa kushirikiana na wananchi wamejenga visima viwili na kufufua visima vyote katika kata za Ifarakara wakitumia kampuni ya MSABI- yaani Maji Safi Boresha Ifakara.

“Kampuni hii inachimba visima kwa bei nafuu sana. Kisima kimoja Sh 250,000 na wananchi wanatoa mchango wa chakula, kokoto, mchanga na kuteka maji,” anasema mbunge huyo.

Kwa upande wa elimu, Mteketa anasema kwamba ndani ya jimbo lake kuna uhaba mkubwa wa madawati huku akifurahia uamuzi wa mkuu wa mkoa mpya wa Morogoro, Joel Bendera kuridhia kuvunwa kwa miti ili kupata magogo ya kuchongwa madawati.

“Lakini, vilevile kwenye elimu tumeanza taratibu za mwanzo kabisa kuomba majengo ya shule ya sekondari ya Michipi…haya yaliyoachwa na Wacuba  kugeuzwa kuwa chuo kikuu, ni majengo mazuri na yakikarabatiwa yatakuwa msaada mkubwa kwetu katika kuboresha elimu,” anasema.

Abdul Rajab Mteketa alizaliwa mwaka 1960, Ifakara, wilayani Kilombero, mkoani Morogoro. Ameona na ana watoto.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: