Mtihani wa vitambulisho bado unaitesa SMZ


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 24 March 2010

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar inakabiliwa na mtihani mgumu sana sasa. ni suala la kuhakikisha kila mtu mwenye haki kisheria ya kupata kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi anakipata.

Ni mtihani hasa kwa kuwa inatakiwa kila mtu mwenye haki kisheria aandikishwe kuwa mpiga kura kwa ajili ya kuja kushiriki kupiga kura katika uchaguzi mkuu ujao.

Mtihani wenyewe unakuja kwa kuwa wananchi bado wanalalamika kuwa wananyimwa kitambulisho hiki, ambacho ni kiingilio cha mtu kuandikishwa na kuingizwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura (DKWK).

Kuna mambo mawili: kwanza Rais Amani Abeid Karume amehakikishia wananchi hadharani kuwa uchaguzi hautafanyika mpaka kila mwenye haki awe ameandikishwa kwenye daftari hili.

Bali jambo la pili ni hatua ya Mkurugenzi wa Idara ya Usajili na Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, Mohamed Juma Ame, kukataa kuwepo malalamiko ya haki kutoka kwa wananchi kuwa wananyimwa vitambulisho.

Ningekuwa mimi rais, na pengine ndio maana siye, ningeshamuita Mohamed ofisini kwangu Ikulu; na kumuuliza “mbona kuna malalamiko mengi ya watu kunyimwa vitambulisho.”

Mohamed atajibu na kutoa maelezo ya kile anachokijua. Kwa msimamo wake kikazi, najua atanidanganya kwa sababu ni kama vile hasikilizi vilio vya wananchi isipokuwa anawabeza.

Tayari uzoefu wa majibu ya Mohamed unaonyesha atatoa maelezo mengi yakiandamana na takwimu zinazoonyesha ametoa vitambulisho kwa watu wote wanaostahili.

Takwimu zitakuwa tamtam. Lakini nikiwa rais nitamuuliza tena, “sasa wewe unasema watu wanaostahili wameshapata vitambulisho, hawa wanaolalamika wanatoka wapi?”

Nitamuuliza tena: Okay tuseme umeshatoa vitambulisho 550,000 Unguja na Pemba. Upo tayari tupite majimboni na orodha yako ya watu uliowapatia vitambulisho?

Kwa kumuuliza Mohamed swali hili la mwisho, rais, katika wingu hili la malalamiko ya wananchi wengi kunyimwa vitambulisho, unataka kutafuta hisia za ofisa wako uliyempa dhamana ya kutendea haki wananchi, kama ametenda haki kweli?

Nasema mimi si rais na huo si katika wadhifa ninaounyemelea maishani mwangu. Urais ni mtihani mkubwa unaoweza kunipelekesha vibaya mbele ya Mwenyezi Mungu. Siutaki ng’o. Wawanie wengine wenye ubavu.

Iwapo Mohamed atakuwa tayari kuzunguka majimboni, kulekule alikopelekea watendaji wake, wakapiga picha wananchi na kuwasajili ili wapatiwe vitambulisho – badala wilayani ambako wanahitaji angalau Sh. 5,000 kufika na kurudi makwao – naapa mchawi atapatikana katika suala hili linalozua utata mkubwa.

Kwa kuwa mimi si rais ambaye ningekuwa na mamlaka ya kumuagiza Mohamed, ninashauri tu kwa nafasi yangu kama mtu wa mawasiliano na umma.

Kwamba kazi ya utoaji vitambulisho kwa wananchi, isifanyiwe mzaha au kuzingatia mtizamo wa kisiasa wa mtu iwapo kweli viongozi wanataka kufuta historia ya mfumo wa utawala uliostawi zaidi kwa kunyima haki na kukandamiza wananchi wenye mtizamo wa upinzani.

Kwa kuwa si kazi ya mzaha na siasa, inatakiwa kufanywa kwa uadilifu mkubwa; bila ya kujengeka hata chembe ya chuki. Unaposikia watu wanalalamika na malalamiko yanaendelea, lazima kuna jambo.

Ni tatizo linalohitaji ufumbuzi. Tena ufumbuzi wa haki na kwa mujibu wa sheria iliyoanzisha kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi.

Inashangaza kuona Mohamed anadhani anaonewa au kusakamwa kila akisoma malalamiko ya watu ambao hawajapata vitambulisho. Akiona tu jina hili na la waandishi wachokonozi wengine, ananuna.

Huo si ufumbuzi. Anapaswa kujua kwamba ofisi yake ni ya umma si ya familia yake wala mtu mwingine yeyote. Ofisi ya umma inatakiwa kutoa huduma kihaki.

Ila kama anadhani anakabiliwa na msongo wa mawazo kwa sababu wapo watu wanaomvuta ili audhi wananchi bila sababu ya msingi, bora awataje hadharani ili waumbuke.

Anaweza kuendelea kusema ofisi yake imetoa vitambulisho laki tano na ushei, lakini kama inaendeleza urasimu mbaya unaokwamisha watu kupata vitambulisho, wale wanaoishia kwa masheha na kudhalilishwa, hajasaidia kitu.

Yeye hawezi kujua idadi ya wananchi. Ataijua watakapojitokeza vituoni. Alipoita watu mwaka 2005 alikosa waliokuwa hawakutimia umri wa miaka 18. Leo waliotimu umri ni wengi.

Si hivyo tu. Inashtua kusikia watu wanazo stakabadhi za uthibitisho wa kusajiliwa lakini wanaendelea kupigwa danadana kama vile wanafuatilia kesi mahakamani.

Mara “njoo wiki ijayo,” akirudi tena anaambiwa, “Wewe itabidi uende makao makuu.” Fikiria mtu amekuwa akifuatilia kitambulisho Gamba, mkoa wa Kaskazini Unguja, lakini unamtaka aende makao makuu Mazizini. Gharama hizi analipa nani?

Mtindo wa kusumbua wananchi ni aina ya uhuni. Haiwezekani ofisi ya umma ifanyie uhuni watu ambao ndio wanaolipa gharama za kuiendesha ofisi hiyo.

Lakini inashangaza kukuta makundi ya watoto wanakutwa wana vitambulisho na ukiwauliza wanasema, “tulipata baada ya kuandikishwa nyumbani kwa sheha.”

Ni ujinga mtupu mtu mzima na akili yake kuacha kazi ya kuzalisha mali akaenda kukusanya watoto na kuwapeleka kwa sheha ili waandikishwe na kupewa haki ambayo wazazi wao wamenyimwa kwa sababu tu wanahisiwa ni wafuasi wa upinzani.

Suala la vitambulisho ni kitanzi ambacho kinawazonga viongozi wa SMZ na hasa wakuu wa ofisi ya vitambulisho wakiongozwa na Mkurugenzi. Muda utaamua yupi mkweli kati ya ofisi na wananchi wanaolalamika.

Kura ya Maoni

Muswada wa kura ya maoni unatarajiwa kuwasilishwa katika mkutano wa Baraza la Wawakilishi unaoanza leo Jumatano.

Mapendekezo ya serikali katika muswada huo yanaonyesha kama vile kura inaandaliwa kwa malengo hasi, siyo ya kupeleka mbele dhamira ya maelewano iliyojengwa na viongozi wakuu wawili wa kisiasa, rais Karume na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad.

Pengine ni dhana yangu tu. Lakini taarifa ninazopata kuhusu jitihada za baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakiwemo wasaidizi wakuu wa Rais Karume, zinashawishi kuwa wanataka kuhakikisha kura inakataliwa.

Wanakataa nini? Wapo wanaotaka ufumbuzi wa mgogoro wa kisiasa Zanzibar usitatuliwe kwa kuanzia na kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa.

Wanataka ibaki vilevile ilivyo sasa kwamba chama kinachoshinda uchaguzi, na wao wanaamini hiki kitakuwa ni CCM tu vyovyote vile, kiunde serikali ya peke yake.

Wapinzani wa serikali ya umoja wa kitaifa iliyopendekezwa na kupitishwa na wajumbe wa baraza wa CCM na CUF walifikia hadi kutaka kumlaghai rais Jakaya Kikwete ambaye aliwatolea nje.

Nataka kuamini kwamba baraza likishapitisha muswada wa sheria ya kura ya maoni, itakapopigwa wakati wake ukifika, basi wananchi wapenda amani ya kweli, ndio watashinda.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: