Mtoto wa Kikwete azua tafrani


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 03 March 2010

Printer-friendly version
Avunja mkutano wa UV-CCM
Ridhiwani Kikwete

MTOTO wa Rais Jakaya Kikwete, Ridhiwani Kikwete anatuhumiwa kuvunja mkutano wa mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UV-CCM), Masauni Yusuph Masauni, MwanaHALISI imeelezwa.

Taarifa zinasema Ridhiwani aligoma kutoka katika mkutano wa Masauni na wenyeviti wa mikoa wa umoja huo.

Lakini Ridhiwani alipoongea na gazeti hili, alikana kuvunja kikao chochote cha mwenyekiti wake.

“Kwamba nilikuwa Moshi ni sahihi. Nilihudhuria mkutano wa kuchangisha fedha za UV-CCM. Basi. Muda wangu mwingi nilikuwa chumbani mwangu. Wanaosema nilizozana na mwenyekiti wangu; wana mpango wa kutugombanisha,” alieleza.

Lakini taarifa zinasema baada ya kuibuka kutoelewana katika mkutano wa kusimika makamanda, mwenyekiti aliitisha mkutano wa ghafla asubuhi ya Jumapili ulioshirikisha wenyeviti wote wa mikoa 20 ya Tanzania Bara wa jumuiya hiyo.

Lakini mtoa habari amesema mkutano huo ulivunjika kabla ya kuanza kutokana na kile kilichodaiwa kuwa “uliingiliwa na watu wasiohusika.”

Gazeti hili limefahamishwa kuwa mwenyekiti Masauni alikataa kuendesha mkutano huo kwa sababu Ridhiwani aling’ang’ania kuwepo kikaoni.

Ilikuwa baada ya Ridhwani kukataa kutoka nje ya ukumbi, mkutano wa wenyeviti ulivunjika, ameeleza mtoa taarifa.

Kwa mujibu wa mtoa taarifa, sekeseke hilo lilianza baada ya Masauni, ambaye imeelezwa alikuwa njiani kwenda mkoani Manyara, kutinga mjini Moshi ghafla.

Mwenyekiti huyo anadaiwa kuvamia sherehe za kusimika makamanda wa vijana wa mkoa wa Kilimanjaro ambako mgeni rasmi alikuwa makamu wake, Benno Malisa.

Mtoa taarifa anasema mara baada ya kuingia Moshi, Masauni alikwenda moja kwa moja uwanja wa Manyama ambako sherehe hizo zilikuwa zinafanyika.

Ni mkutanoni hapo ambako itifaki zinadaiwa kugongana. Wakati Masauni alitaka kusimika makamanda, uvumi wa chinichini ulianza ukiwa ishara za kupinga kushiriki kwake kwani hakuwa amealikwa kwa shughuli hiyo.

Mtoa taarifa anasema alikuwa Malissa, Naibu Katibu Mkuu wa UV-CCM Tanzania Zanzibar, Mohammed Nassoro Moyo na Ridhiwani ambao walimzuia Masauni kusimika makamanda.

Hata hivyo, taarifa zinasema mivutano ndani ya jumuiya hiyo inatokana na makundi yaliyogoma kuzika tofauti zilizotokana na uchaguzi mkuu ndani ya UV-CCM.

“Nakuambia, mivutano imeenea kote Tanzania Bara na Zanzibar, ambako kundi lililobeba Malisa na lile la Masauni hayapikiki chungu kimoja,” ameeleza mtoa taarifa.

Taarifa zinasema makundi yaliyogoma kuzika tofauti zilizotokea wakati wa uchaguzi mkuu yameimarika kwa sura mpya inayoonyesha kuwagawa viongozi wa ngazi ya juu.

Siyo siri kwamba mivutano imedhihirika Tanzania Bara ambako kuna kundi linalobeba makamu mwenyekiti (Benno Malisa) na Visiwani ambako Mwenyekiti Masauni ameonekana kutoelewana na wenzake.

Wachambuzi wa siasa za ndani ya CCM wanaona kuwa ugomvi huu unatokana na mikakati ya kila kundi kulenga matakwa maalum wakati wa uchaguzi mkuu ujao.

Maoni ya wachunguzi yanaonyesha kuwa nguvu kubwa ya maamuzi katika UV-CCM ipo kwa Malissa ambaye inaelezwa kuwa anashirikiana zaidi na Ridhiwani Kikwete.

Taarifa zimesema kundi la Malissa na Ridhiwani linataka kuendesha mambo linavyoona, hata ikibidi, kwa kutomhusisha mwenyekiti Masauni.

Bali Masauni alipoulizwa juu ya uhusiano wa ukinzani na kutohusishwa, alijibu haraka, “Hapana. Siyo kweli. Hakuna kitu kinachotendeka bila mimi kujua.”

Alipoulizwa kwa nini alivamia kikao ambako hakuwa amealikwa kuwa mgeni rasmi, Masauni alijibu kwa utulivu, “Mimi ndiye niliyepaswa kuwa mgeni rasmi.”

Lakini pia Masauni anavutana na naibu katibu mkuu wake Zanzibar, Mohammed Nassor Moyo.

Imeelezwa kuwa tofauti na migongano kati ya wawili hao imejikita katika mikakati ya makundi ya kichama ya kutafuta mrithi wa Rais Amani Abeid Karume.

Hata hivyo Masauni ametajwa kunyemelea ubunge wa jimbo la Kikwajuni, Unguja ambako pia Naibu Katibu mkuu wa CCM Zanzibar, Saleh Ramadhan Ferouz ananuia kugombea.

Katika kinyang’anyiro hicho, Ferouz anaungwa mkono na Moyo. Tayari Masauni na Moyo wamepatanishwa kuhusu suala hili. Hii ilikuwa kwenye mkutano wa uchaguzi wa Chipukizi mjini Morogoro mwishoni mwa mwaka jana.

“Huu mvutano ni mkubwa sana. Wengine wanaita hasa ‘mgogoro wa kimaslahi.’ Viongozi wamegawanyika,” ameeleza mtoa taarifa.

Kutokana na mgongano miongoni mwa viongozi wa UV-CCM ambao umejikita katika kambi, kuna uwezekano mkubwa hali hiyo kuathiri CCM na hata kusababisha kutota katika uchaguzi mkuu wa Oktoba.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: