Mtoto wa mkulima ameanza kupoteza imani


Godlisten Malisa's picture

Na Godlisten Malisa - Imechapwa 11 August 2009

Printer-friendly version

NAANZA kuhofu kwamba Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ameanza kufuta ile imani ambayo Watanzania wengi walikuwa wamempa baada ya kujitambulisha kama mtoto wa mkulima, mara tu baada ya kuteuliwa kushikwa wadhifa huo Februari mwaka jana.

Katika siku za karibuni na hasa kufuatia utaratibu wa kujibu maswali ya papo kwa papo bungeni, waziri mkuu ameonyesha kushindwa kujibu hoja za msingi na badala yake anatoa maelezo ya kumkingia mtu anayetuhumiwa kutenda uovu.

Pinda ambaye ingali kwenye kumbukumbu kwamba alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) chini ya uongozi wa Benjamin Mkapa, ameulizwa swali linalohusu tuhuma za ufisadi zinazomkabali rais mstaafu huyo.

Hata hivyo, badala ya kujibu hoja hii ya ufisadi dhidi ya Mkapa, Pinda amempaka mafuta Mkapa. Tatizo ni kwamba ametumia mafuta yaliyokosa vikolezo hivyo, hayana mvuto. Naona hoja alizozitumia zimekosa mantiki.

Pinda anasema haoni ufisadi wa Mkapa kwa kuwa eti kiongozi huyo mstaafu hamiliki akaunti ya fedha nje ya nchi wala hana ndege zinazoruka. Utetezi huo umekosa mantiki na pia kwa hoja alizotoa, waziri mkuu anaonyesha kujaribu kukwepa hoja kwani Mkapa hatuhumiwi kwa kuwa na akaunti ya fedha nje ya nchi wala kumiliki ndege.

Hata Mkapa angekuwa na vyote hivyo, bado isingekuwa kitu kigezo cha kumfanya atuhumiwe kwa ufisadi. Suala lingekuwa je, mali hizo amezipata kwa njia halali?

Bila haya Waziri Mkuu anajaribu kujenga hoja nyingine dhaifu kuwa Mkapa ni mwadilifu, mcha Mungu na hadi leo anapendwa na kutambulika kama kiongozi mwadilifu.

Hii si hoja hata kidogo. Hoja hapa ni kwamba Mkapa anatuhumiwa kwa matumizi mabaya ya ofisi ya umma, ambayo ni Ikulu, na kutapanya mali za umma pamoja na kujilimbikizia baadhi ya mali hizo kupitia kampuni aliyoanzisha na mkewe akiwa Ikulu, ya ANBEM.

Mali hizo ni pamoja na mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira.

Pinda anapaswa kutambua kuwa suala la mgodi wa Kiwira kama amejimilikisha kiharamu, halina uhusiano wowote na iwapo Mkapa anakwenda au haendi kanisani, anasali au hasali rozali, ni mkarismatiki au la. Kutumia maneno kama haya ni kujaribu kukwepa hoja ya msingi ya tuhuma.

Mwanazuoni yeyote atakubaliana nami kuwa hivi karibuni Pinda ameonekana kushikilia kwa dhati ule msingi au utamaduni uliozolekea wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuendekeza kulindana. Kama si hivyo, Pinda atawezaje kumtuhumu bosi wake wa zamani na mwenyekiti wake mstaafu wa chama ambaye ndiye aliyemuinua kisiasa?

Kwa vyovyote vile Mkapa alipokuwa madarakani kama rais, Pinda alikuwa akipokea na kutekeleza maagizo yake.

Pinda alionesha imani kubwa kwa wananchi alipoteuliwa baada ya kujiuzulu uwaziri mkuu Edward Lowassa aliyetuhumiwa kwa ufisadi. Lakini imani hiyo kidogokidogo ameanza mwenyewe kuipoteza kutokana na kushindwa kujibu hoja za msingi bungeni au kwa kuzijibu jujuu.

Ila ni vizuri waziri mkuu akakumbuka kuwa wananchi hawana roho ya chuma hivyo si ajabu wakamkumbuka Lowassa kuliko yeye maana waswahili husema "Heri mwendawazimu uliyemzoea kuliko kichaa mpya."

0
Your rating: None Average: 2.7 (3 votes)
Soma zaidi kuhusu: