Muafaka sasa Seif kuongoza Zanzibar


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 27 October 2010

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

ZIKIWA zimebaki siku tatu tu kuingia siku ya upigaji kura, tarehe 31 Oktoba, mazingira ya kwenye uwanja wa ushindani yanaonyesha Chama cha Wananchi (CUF) kina nafasi kubwa ya kuunda serikali.

CUF, chama ambacho kinaamini kimekuwa kikiporwa ushindi tangu mwaka 1995, kina nguzo nyingi; mojawapo ni umma wenye morali ya kuleta mabadiliko ulio nyuma yake.

Mwaka 1995, Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ilimtangaza Dk. Salmin Amour Juma wa Chama cha Mapinduzi (CCM), kuwa rais.

Alimzidi mshindani wake Maalim Seif Shariff Hamad wa Chama cha Wananchi (CUF), kwa asilimia 0.2 tu. Matokeo hayo yalisababisha tafrani na kuibua mgogoro wa kisiasa.

CUF walijiaminisha kuwa walishinda, lakini baada ya dola kuingilia, tume ilibadilisha matokeo na kumtangaza Dk. Salmin kuwa mshindi.

Dk. Salmin alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari, mara baada ya kutangazwa kuwa rais, alisema ushindi ni ushindi tu hata ukiwa wa goli moja.

Alisema ataunda serikali kutokana na chama chake tu. Kuna taarifa kuwa walioidhinisha “wizi” wa kura, walikuwa wamependekeza iundwe serikali ya mseto.

Uchaguzi wa 2000 ulivurugwa na dola kwa mbinu ya kufuta matokeo ya majimbo 17 ya Mkoa wa Mjini Magharibi kwa kisingizio kwamba eti kulikuwa na ucheleweshaji vifaa uliosababisha watu kushindwa kupiga kura. CCM ilimsimamisha Amani Abeid Karume kushindana na Maalim Seif.

Uchaguzi ulifutwa baada ya vikosi vya ulinzi na usalama, bila ya shaka vilivyotumwa na watawala wa CCM, kuvamia vituo vya uchaguzi na kupora masanduku ya kura kutoka kwa maofisa wa tume pamoja na mawakala wa vyama vilivyoshiriki uchaguzi.

CUF ilisusia uchaguzi wa marudio uliotangazwa baadaye na hapo njia ikawa nyeupe kwa CCM kubaki madarakani; kwani ilitangazwa ndio mshindi. Madai ya CUF kutaka uchaguzi mpya yaliishia kwa gharika iliyoacha doa kubwa katika sifa nzuri ya Tanzania kuwa “kisiwa cha amani.”

Dola ilidhibiti maandamano ya umma yaliyoitishwa na CUF nchi nzima, 27 Januari 2001 na udhibiti ulipokamilika, makumi ya wananchi walikuwa tayari wameuliwa na askari wa vikosi mbalimbali vya serikali.

Serikali ya Rais Benjamin Mkapa iliendesha uchunguzi chini ya tume ya Brigedia Hashim Mbita na kuthibitisha watu 30 waliuawa katika maandamano hayo yaliyofanyika pia mikoa ya Tanzania Bara, ukiwemo Dar es Salaam.

Katika uchaguzi uliopita wa 2005, takwimu zilionyesha mapema kuwa CUF ilishinda. Lakini baada ya dola kutunisha misuli kwa mara nyingine, kwa nia ya kulinda watawala wa CCM, Karume alitangazwa tena mshindi.

Umma ulikasirikia hali hiyo na kundi kubwa la wafuasi wa CUF lililokuwa limekusanyika makao makuu ya chama Mtendeni, likajikuta limezingirwa na vikosi vya ulinzi na usalama kwa kusudi la kuwazuia kutoka barabarani kufanya maandamano.

Baada ya siku mbili, huku taasisi za ndani ya nchi na zile za kimataifa zikilalamikia uvunjaji wa haki za binadamu na demokrasia, walinzi waliondolewa na sherehe ya kuapisha rais Karume ikatekelezwa.

Uchaguzi wa keshokutwa unafanyika chini ya mazingira mazuri ya kisiasa; hali iliyofuatia kufikiwa kwa maridhiano kati ya vyama vikuu kiushindani.

Maridhiano yaliidhinishwa na Baraza la Wawakilishi na kutungiwa sheria iliyowezesha katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kubadilishwa ili kuruhusu mfumo wa serikali ya umoja wa kitaifa. Serikali ya Umoja wa Kitaifa itaundwa mara tu baada ya uchaguzi huu.

Sasa wachambuzi wa siasa wanaamini kwa mazingira yaliyopo, kuna uwezekano mkubwa Zanzibar kuwa na uchaguzi wa kwanza ulio huru na wa haki na ambao umefanyika kwa uwazi. Kwa mazingira hayohayo, CCM itakosa nafasi ya kuendelea kushika hatamu za uongozi wa serikali.

Mazingira yanaleta imani kwamba kila mtu atapiga kura moja, tofauti na chaguzi zilizopita paliposhuhudiwa makundi ya wananchi waliopewa ulinzi na dola kuingia vituoni na kupiga kura watakazo kwa mtindo wa kuhamahama vituo.

Kulikuwa na kambi nyingi za vijana wa CCM ambao kutokana na ukorofi na uharamia wao walipachikwa jina la Janjaweed, mfano wa wanamgambo wa nchini Sudan wanaopambana na umma wa eneo la kusini unaodai haki ya kujitawala.

Safari hii hakuna “kambi za kishetani” zilizokuwa nguzo ya ushindi wa CCM. Hazipo. Ndio maana kampeni za uchaguzi zimekuwa za salama na utulivu mkubwa ambao haujapata kutokea tangu dola ya Zanzibar ilipojiasisi.

Sehemu kubwa ya wapiga kura mara hii ni vijana. Hili ni kundi linalotaka mabadiliko ili kupata maisha bora na yenye neema, kinyume na ilivyo. Hawa vijana wamechoka kugandishwa.

Ni kama walivyochoka wazee wao kuona maisha yanazidi kuwa magumu kutokana na sera za serikali iliyoko madarakani kutotoa matunda yanayowagusa hata wao.

Chanzo kikubwa cha sera zisizozaa matunda ni uongozi mbaya ambao hata kama haukufikia kuitwa “utawala wa mkono wa chuma,” angalau ulikuwa na mfanano wa kiasi fulani.

Uongozi huu ulichochea chuki na hasama miongoni mwa wananchi. Walioheshimu utawala wa CCM na kuishi kutokana nao, wakaonekana ndio watu; waliopendelea upinzani wakachukuliwa kuwa ni mamluki wasiostahili hata haki zao za msingi.

Vijana na wazee wanautazama uchaguzi huu kwa mategemeo makubwa ya kuleta mabadiliko; na kwamba wakiipoteza nafasi hii, watakuwa wamekosa kila kitu; wataililia milele.

Wachambuzi wanaamini kuwa ile sauti na sukumo wa mabadiliko, ndio utakaoiingiza CUF na mgombea wake wa urais, Maalim Seif, kwenye kilele cha utawala wa Zanzibar.

Hivi sasa CCM ni dhaifu kuliko wakati mwingine wowote; si Zanzibar peke yake, hata Tanzania Bara ambako nako kundi la vijana limechemka na kutaka mabadiliko.

Udhaifu wa CCM uko kwa namna mbili. Kwanza, kimeshindwa kutafsiri sera zake katika kuwapatia Watanzania maendeleo yanayotumainiwa kulingana na wakati uliopo. Sera zenyewe hazitekelezeki, na ni kutokana na uongozi mbaya usio na usimamizi makini.

Pili, ni mgawanyiko mkubwa ndani ya chama hiki kilichotokana na mifupa ya ASP (Afro-Shirazi Party cha Zanzibar) na TANU (Tanganyika African National Union) cha iliyokuwa Tanganyika.

Mgawanyiko kwa CCM umetokana na mambo mengi, lakini makuu ni mienendo ya uhafidhina kwa wakongwe wake; ufisadi wa kutumia fedha na mabavu na vuguvugu jipya la vijana wanaotaka kukijenga chama.

Matokeo ya kura za maoni za utafutaji wa wagombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi huu ni ushahidi wa hayo. Fedha nyingi zilitumika kwa kila aliyekuwa anatumaini kuteuliwa kugombea ubunge, uwakilishi na udiwani.

Si vizuri kusahau kutaja nguvu moja iliyochangia CCM kuonekana ni chama kilichokwisha kifikra na kidhamira. Hii ni nguvu ya upinzani.

Kambi hii, licha ya kugawanyika kwake, imejitutumua na kujieleza vizuri kwa umma, ikitumia udhaifu wa watawala kujenga hoja makini na matokeo yaliyoanza kuonekana tangu kikao cha bajeti cha mwaka 2007, yanathibitishwa katika kipindi hiki cha kampeni.

Kwa Zanzibar, makundi ya wenyewe kwa wenyewe yameimarika mno. Mbio za nani awe rais zimekimaliza chama. Hata hatua ya kumteua daktari wa sayansi ya atomiki, Mohamed Gharib Bilal kuwa mgombea mwenza wa Jakaya Kikwete, hakujatibu majeraha.

Kampeni ya daktari wa binadamu nchini, Ali Mohamed Shein imekuwa ngumu kweli. hata mwenyewe anajua kuwa halazimiki kupumbazwa na wingi wa vijana wanaofika kwenye mikutano yake.

Vijana wenyewe wanasema wazi kuwa wanafuata starehe na kwa sababu hawana gharama yoyote kufuatilia kampeni ya CCM – magari bure, posho ya angalau Sh. 2,000 wanapata; hata kama mkutano unafanyika kijiji cha mbali – wapo kwa mzo.

Huu ni udhaifu unaotoa nguvu kubwa kwa CUF na mgombea wake. Na ni hali hiyo basi, inayotoa ishara kuwa wakati wa Maalim Seif kushika hatamu za uongozi wa serikali mpya itakayokuwa ya Umoja wa Kitaifa, sasa umefika.

Kampeni ya CUF imesifiwa na wengi hata wanadiplomasia niliopata kukutana nao. Imetungwa vizuri ikatungika; imepangwa vema ikapangika; inaelezwa vizuri inaelezeka; na ilani ya uchaguzi ya CUF imeandaliwa chini ya uzoefu wa matokeo ya uongozi mbaya ulioiharibu jamii ya Wazanzibari.

Ambaye hajathibitisha hili, atumie siku tatu za mwisho za kampeni. Hudhuria mkutano wa Dk. Shein. Sikiliza wanaopanda jukwaani. Muangalie Dk. Shein akipanda jukwaa. Tazama pembeni mwa mkutano kunaendelea nini.

Utaweza kugundua yafuatayo: Umati unafuata shangwe ya nyimbo na burudani jukwaani. Hotuba zikianza unapunguka. Makundi ya vijana yanajisogeza pembeni na kubarizi.

Wakati Dk. Shein anahutubia, tayari watu wanakutwa wanatangatanga maeneo ya karibu na mkutano; hawasikilizi anachokisema mgombea. Hali ni ngumu kwa CCM na Shein wake.

Hali ni tofauti upande wa mikutano ya Maalim Seif. Vijana hawataki wala hawafanyi mzaha. Wanasikiliza kwa makini.

Nijana wanafuatilia hata hotuba ya mpiga debe yeyote wa Maalim Seif; akiwemo kijana machachari Issa Kheir Hussein, mwalimu wa ki-Tumbatu anayevuna ujuzi mkubwa akiwa begani kwa Maalim Seif.

Ukweli ni kwamba Maalim Seif hajachoka wala hajachusha wanaomzingatia. Ndio maana Ismail Jussa, kijana aliyemlea sana kisiasa, alipotangaza kuandaliwa kwa keki ya sherehe ya siku ya kuzaliwa kwa mgombea wa CUF, akitimiza miaka 67, mvumo mkubwa ulisikika uwanja wa Ijitimai ya zamani, Mwanakwerekwe.

Akaikata keki, akalishwa na mama Awena, mwalimu makini licha ya ukimya wake; akakatiwa akalishwa na wanawe. Sherehe kubwa na hadharani ya namna ile.

Pale ni jimboni kwa Shamsi Vuai Nahodha, kijana aliyetunukiwa uwaziri kiongozi lakini akiishia na kumsimanga mteuzi wake kwa kumwita “dereva mtatanishi.”

Ukipima haya, huna haja ya kushangaa iwapo kura zaidi ya asilimia 70 zitahesabiwa kwa Maalim Seif Shariff Hamad. Inshaallah yatakuwa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: