Muda wa kampeni wayoyoma, hadhi ya ahadi yapungua


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 29 September 2010

Printer-friendly version
Gumzo

SIKU 40 za kampeni zimemalizika. Wagombea watatu wanaonekana kuwa washindani wakuu katika mbio za urais – Dk. Willibrod Slaa, Profesa Ibrahim Lipumba na Jakaya Kikwete.

Lakini aliyenogesha kampeni hadi sasa ni Kikwete, mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyeamua kujinadi kwa staili ya kumwaga lundo la ahadi. Kila anapopita, anaahidi hiki au kile. Hawezi kuondoka bila kumwaga ahadi.

Mpaka sasa, tayari ametoa ahadi ya kutekeleza miradi mikubwa 32 katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Nyingi ya ahadi hizo zinaonekana wazi kuwa hazitekelezeki.

Baadhi ya aliyoahidi yanahitaji utashi mkubwa wa kisiasa kutoka nje ya mfumo wa chama chake. Miradi mingine inahitaji wataalamu wenye ujuzi na mabilioni ya shilingi kuitekeleza.

Kwa mfano, Kikwete ameahidi kuunganisha shule zote za sekondari nchini katika mtandao wa mawasiliano (itaneti). Anasema hilo atalifanya ndani ya kipindi hiki cha mwaka huu wa fedha.

Hakuishia hapo. Ameahidi kuipatia kila shule ya sekondari walimu wanne wenye ujuzi na uwezo katika masuala ya itaneti. Nchi nzima ina shule zaidi ya 4,000 za sekondari.

Hivyo basi, ili kufanikisha ahadi hii, Kikwete atalazimika kuajiri walimu wapya 16,000. Atalazimika kusomesha walimu wapya ili kukidhi mahitaji hayo. Je, hilo linawezekana? Jibu liko wazi. Hataweza.

Kwanza, kabla ya Kikwete kuahidi pepo kwa waliohai, ni vema angeangalia kwanza kile kinachoitwa, “Malengo ya Elimu ya Msingi,” kama kinaweza kutekelezwa na serikali yake.

Mwaka mmoja baada ya Kikwete kuingia madarakani, serikali yake iliweka kile kilichoitwa, “Mpango wa elimu ya msingi.”

Mkakati huu unapatikana katika kitabu kiitwacho, “Muhtasari wa Sayansi kwa shule za msingi.” Kimetolewa na serikali mwaka 2006.

Katika andishi lake, serikali inasema, “…Elimu ya msingi inayohitajika kwa Watanzania kwa maendeleo ya sasa, ina madhumuni ya kuwapatia walengwa maarifa, stadi na mwelekeo unaohitajika kwa maendeleo ya taifa.”

Katika kufanikisha mkakati huu, serikali iliweka malengo kumi 18 na taarifa zinasema, iliahidi kutekeleza malengo hayo ndani ya miaka miwili ya kwanza.

Pamoja na mengine mengi, serikali iliahidi kumpatia kila mwanafunzi stadi za kusoma, kuandika, kuhesabu, ubunifu na kumwezesha kuwasiliana kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza.

Je, haya yamefanyika? Kama ndiyo, kwa kiwango gani? Kama bado, kwa nini yameshindikana? Nani aliyesababisha yaliyoahidiwa na kunakiliwa katika vitabu vya serikali kushindwa kutekelezwa? Je, wahusika wamechukuliwa hatua gani? Lini na wapi?

Ukiangalia suala hili kwa makini, utabaini haraka kuwa hakuna hata moja lililotekelezwa. Kati ya watoto 10 waliomaliza darasa la saba mwaka 2009, watatu walimaliza bila kujua kusoma na kuandika.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Mtandao wa elimu Tanzania katika wilaya 30 nchini, kati ya watoto kumi, wanaofanya mtihani wa darasa la saba, watatu wanamaliza shule bila kujua kusoma na kuandika.

Hapa hatuzungumzii kuandika Kiingereza, tunazungumzia kuandika Kiswahili. Hata katika Kiingereza, nako kuna mgogoro. Serikali haikufanikiwa kuondosha raia wake katika giza.

Je, hayo majigambo, kwamba serikali imeimarisha elimu na sasa inataka kuunganisha shule zote za sekondari katika mtandao wa intaneti yanatoka wapi?

Utafiti unaonyesha kwamba zaidi ya asilimia 80 ya watoto waliomaliza darasa la saba mwaka 2008, hawajui kuandika na kuzungumza Kiingereza?

Si hivyo tu. Zaidi ya asilimia 70 ya watoto waliomaliza darasa la saba mwaka 2009, hawakufaulu mitihani yao.

Kwamba wakati Mwalimu Nyerere anaondoka madarakani mwaka 1985, aliachia taifa hili urithi mkubwa wa elimu. Wakati huo, ilikuwa ni asilimia tisa tu ya watu wasiojua kusoma na kuandika.

Leo, miaka 25 baada ya Nyerere kuondoka madarakani, wasiojua kusoma na kuandika wameongezeka na kufikia asilimia 30.

Aidha, katika baadhi ya maeneo, hasa yale ya vijijini, baadhi ya wanaoitwa wanafunzi wa sekondari, hawajui kusoma na kuandika Kiswahili kwa ufasha. Hapa ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa kwa watoto waliopo Kidato cha Pili.

Utafiti uliohusisha kaya zaidi ya 20,000 na watoto zaidi ya 40,000 unaonesha kuwa kuna tatizo kubwa katika elimu nchini.

Kwa mfano, inatakiwa asilimia 100 ya watoto wanaoingia darasa la tatu, kuwa na stadi za kusoma na kuhesabu.

Lakini ukweli ni kuwa hadi wanapofika darasa la tatu, watoto saba kati ya 10 hawawezi kusoma Kiswahili cha msingi; watoto tisa kati ya 10 hawawezi kusoma Kiingereza cha msingi, na watoto wanane kati ya 10 hawawezi kufanya hesabu za msingi.

Tatizo hili limekuwa kubwa zaidi katika maeneo ya vijijini ambapo Kikwete amelundika hicho anachoita, “Shule za kata.”

Kikwete analijua hili? Chama chake kinajua hili? Wanajua kwamba watoto wetu wanakwenda shule, si kujifunza, bali wanakwenda kukulia huko tu?

Wanajua kuwa shule zilizopo ni “jahanamu la maisha yao?” Wanafahamu kwamba zinazoitwa shule ni vijiwe vya watoto kukulia na pengine kuvutia bangi?

Bila shaka anajua. Ndiyo maana yeye na wakubwa wenzake katika chama na serikali, hawapeleki watoto wao katika shule hizi.

Hata hayo majengo ambayo serikali inayaita shule, mengi yako hoi. Wataalamu wa ujenzi wanasema, asilimia 70 ya majengo ya shule yaliyopo sasa, yataanza kuanguka baada miaka 10 toka yajengwe – miaka sita iliyopita.

Kisa: Ni kwa kuwa yamejengwa chini ya viwango. Waliohusika kuingiza taifa katika majanga ya vifo vya watoto wetu kwa kujenga majengo hafifu wanafahamika, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa dhidi yao.

Hata Kikwete hawezi kujibu kwa ufasaha, kwamba waliotafuna fedha za shule kwa kujenga majengo yasiyo na viwango wamechukuliwa hatua gani.

Anajua kuwa hakuna hatua zilizochukuliwa dhidi yao. Anajua kuwa baadhi ya makandarasi waliohusika katika utapeli huu, wamepitishwa na chama chake kugombea ubunge na udiwani.

Wengine ndio wafadhili wa kampeni zake za kutaka kuendelea kuwa madarakani. Baadhi yao wanafahamika hata kwa majina.

Hata pale ambapo baadhi ya wenzake katika chama wanamueleza mgombea huyo ametafuna fedha za walipa kodi, yeye ametia pamba masikio.

Wengi wao amewapitisha kugombea uongozi na sasa analazimika kuwaombea kura. Majengo yaliyoachwa na mkoloni miaka 100 iliyopita, bado yanadunda.

Mfano hai ni jengo la shule ya sekondari Pugu na lile la sekondari ya Tabora. Pamoja na kutotunzwa vizuri na serikali, lakini hakuna dalili za kuanguka katika miaka 10 ijayo.

Sasa katika mazingira haya, Kikwete anapata wapi ubavu wa kusema kwamba serikali yake, tena katika mwaka huu wa bajeti, itaingiza shule zote katika mtandao wa intaneti?

Tatizo kubwa la Kikwete na chama chake ni kutojua nini kifanyike sasa na kipi kitendeke baadaye.

Ndiyo maana katika mwaka huu wa fedha 2010/2011, serikali inatarajiwa kutumia Sh. 11.1 trilioni. Ni ongezeko la Sh. 1.6 trilioni zaidi ya bajeti ya mwaka jana.

Hata hivyo, nyongeza ya Sh. 1.6 trilioni kwenye bajeti ya mwaka huu ina umuhimu kidogo kwa kuwa kilicholipua bajeti ni kushuka kwa thamanai ya shilingi.

Lakini kwa mujibu wa mwelekeo wa bajeti, serikali imetenga Sh. 3.2 trilioni tu kwa ajili ya maendeleo. Kiasi kilichobaki cha Sh. 7.9 trilioni kimetengwa kwa matumizi ya kawaida.

Kikwete na serikali yake wanalaumiwa na wahisani kwa kutofanya vizuri au kuzembea katika kukusanya kodi.

Hata mikopo imepungua, jambo ambalo linathibitisha kuwa kinachoahidiwa kutekelezwa hakiwezi kufanyika.

Kiwango hicho cha mikopo kimepungua kutoka dola 840 milioni hadi dola 534 milioni.

Ni kutokana na pigo hilo, serikali ililazimika kukopa Sh. 983.7 bilioni kutoka kwa mabenki ya biashara ya ndani kwa masharti ya kibiashara, jambo ambalo limezidi kuteteresha uchumi.

Misamaha ya kodi nayo imeongezeka. Angalia wanaoitwa wawekezaji katika sekta ya madini wanavyopeta. Kikwete ameshindwa kusikiliza kilio cha wananchi, kwamba misamaha hii inakandamiza uchumi wa taifa.

Kwa mfano, wawekezaji katika sekta ya madini hawalipi kodi ya mafuta wanayotumia. Lakini migodi inapata faida kubwa na inapanuka kibiashara.

Jingine ambalo litayeyusha ahadi za Kikwete ni mfumuko wa bei na kushuka kwa thamani ya shilingi. Kwa mfano, wakati wa bajeti mwaka jana thamani ya dola ilikuwa Sh. 1,250. Leo ni zaidi ya Sh. 1,500.

Kutokana na hali hiyo, Kikwete aache kukimbilia kuunganisha shule kwenye mtandao wa intaneti, ashughulikie matatizo makubwa yaliyopo nchini.

Kwa mfano, aanze kwa kushughulikia tatizo la watoto kumaliza shule bila kujua kusoma na kuandika.

Aachane na majigambo ya kushangilia majengo mapya na idadi kubwa ya watoto wanaoandikishwa. Kuandikishwa kwa watoto wengi hakiwezi kuwa kigezo cha mafanikio katika elimu.

Ishughulikie tatizo la kuwapo idadi kubwa ya watoto wanamaliza elimu ya msingi bila kujua kusoma wala kuhesabu.

Inabidi serikali ijikite zaidi katika kuangalia kinachotokea shuleni badala ya kulisha wananchi takwimu. Hata bajeti inayopelekwa katika elimu haikidhi mahitaji.

Kikwete anajua kuwa kila mzazi au mlezi, anapeleka mtoto shule siyo kuvaa sare tu, bali kupata maarifa. Kama thamani ya elimu inaangaliwa kwa wingi wa watoto darasani, basi Kikwete na chama chake watakuwa wanasherehekea ndoa za waathirika wa kansa. Haitadumu.

Tatizo kubwa la serikali ya Kikwete, ni kutopea katika matumizi yasiyo ya lazima. Hata kampeni zake za urais, zinathibitisha hili.

Angalia Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha uliokwisha. Matumizi makubwa ya serikali yako kwenye malipo ya posho, masurufu ya safari za nje na ununuzi na utunzaji wa magari ya kifahari ya serikali.

Katika hali ambayo haijaweza kuelezwa hata na serikali yenyewe, kiasi cha fedha kilichopangwa kutumika kwa ajili ya matumizi ya kawaida, kimezidi kile kinachokusanywa na serikali yenyewe.

Hii ina maana kwamba serikali italazimika kutumia hata fedha za mikopo, misaada kutoka kwa wafadhili na michango mingine ya wahisani kugharamia matumizi yake ya kawaida.

Je, serikali inayotafuna kama mchwa, itaweza kutekeleza miradi hii anayoahidi? Je, kuna miradi mingapi iliyoahidiwa ambayo itaishia njiani?

Wengine wanasema Kikwete ameamua kuja na lundo hili la ahadi, si kwa sababu ana dhamira ya dhati ya kutekeleza kile anachoahidi. Anachotafuta ni yeye kushinda. Akishinda, basi.

Kikwete anajua kwamba yeye hatagombea tena urais. Hivyo, hakuna anayeweza kumuuliza na hata kumhoji.

Wala hajali yule atakayekuja baada ya yeye kumaliza kipindi chake. Hajipi muda wa kutafiti, kwamba hiki anachokiahidi sasa, kisipotekelezwa kitakuwa kitanzi kingine kwa chama chake.

Ni hatari zaidi pale yeye na chama chake watakaposhindwa. CCM yaweza kufa moja kwa moja.

Bali Mungu apishe mbali. CCM inastahili kubaki hai; ikae pembeni na kushuhudia jinsi chama kingine kinavyoweza kuunda na kuendesha serikali isiyo na ufisadi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: