Muda wa SMZ kufedheheka unakaribia


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 05 May 2010

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

TUME ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imeshatangaza kuwa uchaguzi mkuu wa Zanzibar; utakaohusisha kuchagua rais, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na madiwani, utafanyika tarehe 31 Oktoba.

Lakini tume yenyewe imeanza kubanwa koo iwajibike ipasavyo. Hata ikipiga kelele kwamba haijui wapi walipo watu kadhaa ambao walishiriki uchaguzi wa mwaka 2005, inatakiwa iwasake ili iwaandikishe.

Katika taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wake, Khatibu Mwinchande, hivi karibuni, ZEC imesema imeandikisha watu 382,958 Zanzibar (Unguja na Pemba) idadi ambayo ni asilimia 75.5 ya makadirio. Ilikadiria kuandikisha watu 550,000.

Sasa wakuu wa tume wanalalamika kuwa idadi hiyo ni ndogo kwani kuna upungufu wa watu 124,267 ambao inasema hawakuandikishwa.

Tume ilianza uandikishaji wapiga kura wa kujumuishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura (DKWK) la Zanzibar mwezi Julai mwaka jana. Awamu ya pili ya uandikishaji inaendelea katika baadhi ya majimbo na itakamilika tarehe 9 Mei.

Iwapo uandikishaji umekamilika katika majimbo mengi Zanzibar – baki majimbo machache ambayo tume inaendelea na awamu ya pili – lakini idadi hiyo ya watu hawakuandikishwa, nini maana yake?

Maana yake ni kwamba watu hao wako nje ya daftari na kwa hivyo siku ya kupiga kura ikifika, hawatapata nafasi ya kutumia haki yao ya kikatiba ya kupiga kura kwa ajili ya kuchagua viongozi wanaowataka.

Taarifa yake imeonyesha kwamba imeandikisha watu 271,601 (asilimia 77.5) kisiwani Unguja na watu 111,357 (asilimia 71) kisiwani Pemba.

Kwa hivyo, kulingana na makadirio iliyoyafanya kabla haijapita kwenye majimbo kuanza kazi ya uandikishaji, watu 78,906 kwa Unguja na 45,361 kwa Pemba wamekosa kuandikishwa.

Kumbe Tume ilikadiria kuandikisha wapiga kura 550,000. Ninaamini makadirio haya yalifanywa kitaalamu kwa kuzingatia takwimu zilizopo kwa Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Lakini uandikishaji ulipoanza tu kulianza kutolewa kauli za kuitisha tume kwamba kamwe haitaweza kuandikisha kwa mujibu wa makadirio yake.

Mpaka wakati naandika makala hii, Mohamed Juma Ame, Mkurugenzi wa Idara ya Usajili na Kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi, hajafuta kauli yake hiyo.

Huyu ni ofisa mwandamizi katika serikali ambaye katika nchi inayofuata misingi ya utawala bora, angetarajiwa kuisaidia Tume ya Uchaguzi kufanikisha matarajio yake.

Kauli yake ilikuwa ni kitisho kwa wakuu na watendaji wengine wa Tume ya Uchaguzi. Pengine hawakutetereka. Lakini hawakutoa kauli yoyote kuhusu tamko la Mohamed bali walikuwa wanasisitiza wataandikisha kwa mujibu wa sheria.

Hadharani na mara kadhaa, Mohamed alikuwa anasema tume haitafikia idadi hiyo ya watu kwa sababu kwa mfumo waliouweka katika kutoa vitambulisho, hakutakuwa na upandikizaji wapiga kura.

Alisema kwa mfumo wanaotumia kusajili na kutoa vitambulisho, yale yaliyotekelezwa na wanasiasa wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, hayatawezekana.

Nilimsikia akieleza hayo ukumbi wa hoteli ya Mazsons, mjini Zanzibar na ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam, kulipofanyika mijadala kuhusu matatizo yaliyokuwa yakitokea katika uandikishaji.

Katika ripoti ya tume baada ya uchaguzi wa mwaka 2005, ilielezwa kwamba watu wapatao 3,000 walibainika kuandikishwa zaidi ya mara moja.

Na bado wahalifu hao hawajafunguliwa mashitaka mahakamani na kisingizio kimekuwa kwamba tume ilipopeleka orodha yao kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) wa Zanzibar haikutoa maelezo ya kutosha kuwezesha kuwatambua.

DPP, Othman Masoud Othman, aliwahi kueleza mara nyingi suala hilo kwamba ni vigumu kuwashitaki kwani hakuna vielelezo vya watu hao.

Mpira ukatupwa kwa tume ambayo iliwaandikisha kwa kuwa ilipaswa kupeleka vielelezo hivyo zikiwemo picha zao.

Kwa vile watu hao tumeambiwa waliandikishwa, lazima wanajulikana kwa majina matatu kama ulivyo utaratibu; vituo vipi waliandikishwa na lini? Lazima namba za shahada walizopewa na picha zao itakuwa zipo tu.

Si walipofika vituoni walitaja yote hayo? Zitakosekanaje kumbukumbu zao? Ni ushetani tu kuelezwa eti haijulikani wapatikaneje.

Taarifa kamili za watu hao zipo, sema tu suala la kuwakamata na kuwashitaki mahakamani, litafichua yasiyotakiwa kuwekwa hadharani na watawala, Chama Cha Mapinduzi (CCM). Kwa kujua vizuri hilo, chama na serikali wanaona kuwashitaki haina maslahi kwao.

Ukweli ni kwamba mazingira yaliyokuwepo wakati wa uandikishaji wapiga kura, haikuwa rahisi vyama vya upinzani kupenyeza watu wasiostahili. Kama ulivyokuwa upigaji kura, uandikishaji ulidhibitiwa na vyombo vya dola.

Wakati wa uandikishaji wapiga kura, tulikuwa tunashuhudia magari ya baadhi ya viongozi wa CCM na ya vikosi vya ulinzi vya SMZ yakipeleka watu vituoni wakiwemo watoto wadogo ili waandikishwe.

Matukio kama hayo yalitokea siku ya upigaji kura mengine mbele ya macho ya watazamaji wa ndani na nje ya nchi.

Watu hao baada ya kushushwa vituoni, waliingizwa ndani kwa misururu na chini ya ulinzi wa vyombo vya dola na walipiga kura. Wapo waliokuja kusimulia kwa majivuno kwamba walipiga hadi kura kumi mtu mmoja.

Nataka niamini Mohamed anaposema wanasiasa walipandikiza wapiga kura, hakukosea. Tatizo lake ni kwamba hakutaja ni wanasiasa wepi?

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Mwinchande anasema kwa kushirikiana na Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), wanatafiti ili kubaini sababu za kushindwa kuandikisha watu wengi.

Hiki ni kitendawili. Kwanza, naona tume ingepata majibu rahisi kwa kujadiliana na Mohamed, yule aliyetamka kuwa haitaweza kuandikisha watu kwa idadi iliyokadiria.

Lakini pili, tume iliwahi kukusanya takwimu za watu waliokuwa wanajitokeza vituoni ili kuandikishwa lakini wakakosa haki hiyo kwa kutokuwa na kitambulisho. Hiki kinatolewa na ofisi ambayo Mohamed ndiye mkurugenzi wake.

Hivi si ni dhahiri kuwa tume ilikwazwa kuandikisha kimatarajio kwa sababu zoezi la utoaji vitambulisho limekuwa na mizengwe mingi na watu wangali wanaendelea kulalamika kunyimwa haki?

Nilidhani angekuwa chanzo kikuu cha kushirikishwa katika utafiti ambao Tume imeahidi kuufanya pamoja na UNDP.

Hapa akili ya kawaida inakubali kwamba watu wengi walikuwa hawana kitambulisho ambacho kulingana na sheria ya uchaguzi, ni sharti ili mtu aandikishwe.

Tatu, bila ya ubishi wa kishetani, inaeleweka wazi kuwa kuna idadi nzuri ya watu walionyimwa kitambulisho kwa sababu za kisiasa tu. Wanadhaniwa hawatachagua CCM.

Yalitokea jimbo la Magogoni lilipofanya uchaguzi mdogo wa mwakilishi Mei mwaka jana. Wengi walinyimwa kupiga kura kwa kukosa kitambulisho.

Jimbo kama la Mji Mkongwe lililokuwa na wapiga kura zaidi ya 13,000 mwaka 2005, leo limekuja na wapiga kura 7,372 tu. Wako wapi watu zaidi ya 6,000?

Ama itakuwa kweli kulikuwa na upandikizaji wapiga kura kama alivyosema Mohamed, au kwa makusudi ya kukidhi matakwa ya kisiasa, wamenyimwa kitambulisho na ofisi yake.

Katika jimbo hili ambalo ndilo ngome kuu ya Chama cha Wananchi (CUF) Unguja, nilikuta viongozi wa upinzani wameshikilia yapata fomu 1,000 za rufaa za watu walionyimwa vitambulisho.

Wengi wao ni vijana waliotimiza umri wa miaka 18 kati ya mwaka 2005 na sasa.

Muda wa serikali kufedheheka kiulimwengu unazidi kukaribia.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: