Mugabe na Ardhi, Kikwete na EPA


Stanislaus Kirobo's picture

Na Stanislaus Kirobo - Imechapwa 26 March 2008

Printer-friendly version

ANGALAU nawasifu Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe na Mkuu wa jeshi la polisi nchini humo, Augustine Chihuri, waliotamka kwamba upinzani hauwezi kuachiwa nchi kutawala.

Mugabe amenukuliwa katika mkutano wake wa kampeni Jumamosi iliyopita akisema, "wapinzani wasahau kutawala mimi nikiwa hai."

Kwa upande wake, Chihuri amesema, "sitaruhusu upinzani kutawala hapa. Hawa ni vibaraka tu wa nchi za Magharibi."

Namsifu Mugabe kwa kuwa wazi katika hilo, ukilinganisha na viongozi wengine wa Afrika ambao hujigamba kusimamia demokrasia wakati wanafanya kinyume.

Kauli hizi zinaashiria kwamba hakuna uchaguzi huru na wa haki nchini humo. Kwani ni huyo huyo Chihuri aliyewahi kutamka katika uchaguzi uliyopita angejiuzulu wadhifa wake iwapo upinzani, chini ya chama cha Movement for Democratic Change (MDC) kinachoongozwa na Morgan Tzvangirai ungeshinda.

Lakini si Zimbabwe peke yake yenye kuchafua demokrasia katika bara la Afrika. Zipo nyingi nyingine.

Katika hali ya kawaida ni vigumu kuzitambua nchi hizi, lakini angalia tu ifikapo wakati wa uchaguzi zinavyoweza kujibainisha.

Naweza kusema kwa uhakika kwamba ni Afrika Kusini pekee, pengine labda na Botswana, ndiyo nchi angalau demokrasia inaweza kukidhi tafsiri yake halisi.

Kama nilivyosema, ni bora Mugabe ambaye kamwe hafichi azma yake ya kufinya demokrasia ili kubaki madarakani.

Wapo viongozi wengine hutoa kauli za kinafiki kwamba katika nchi zao uchaguzi unafanyika kwa njia huru, haki na kwa kuzingatia misingi ya demokrasia.

Lakini tulioyashuhudia nchini Kenya, Ethiopia 2005, Uganda 2006, Zambia 2006, Congo (DRC) 2005, Malawi 2004, Madagascar 2001 na Ivory Coast 2000 yanadhihirisha kwamba viongozi wetu wananena, bila kutenda.

Chaguzi zote hizi zililalamikiwa kwa kutokuwa huru na haki, kuanzia maandalizi yake, uandikishaji wa wapiga kura, uteuzi na uthibitishwaji wa wagombea; utumiaji mbaya wa fedha katika kampeni hasa kwa vyama tawala haukuweza kuelezeka.

Baadhi ya chaguzi hizo zilileta machafuko makubwa ikiwamo mauaji. Mfano halisi ni Ivory Coast, Ethiopia, DRC, Kenya na Madagascar.

Hata Tanzania, ni miongoni mwa nchi zinazokiuka wazi wazi kanuni za uendeshaji wa chaguzi zake, mapungufu ambayo yanaifanya demokrasia yetu kukosa uwanja ulio sawa.

Na hakuna sehemu ya nchi iliyoathirika sana katika chaguzi za ovyo kama Zanzibar. Chaguzi zake zote zimekuwa zikiporwa na chama kilicho madarakani kuanzia ule wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995.

Hali hii imezusha mgogoro mkubwa wa kisiasa visiwani humo hadi umwagaji mkubwa wa damu uliotokea Januari 26-27, 2001 baada ya upinzani kukataa matokeo ya uchaguzi wa 2000.

Pengine kuna kitu kimoja ambacho kina kila dalili za kutaka kuibuka na kukisuta chama tawala-Chama Cha Mapinduzi, kuhusu kutokuwapo kwa haki katika uchaguzi hasa uliopita.

Katika sakata la ufisadi linaloendelea kuchunguzwa, dalili zimeanza kuonyesha kuwapo kwa uchotaji haramu wa mabilioni ya mapesa kutoka Benki Kuu (BoT) kupitia Akaunti ya Madeni ya nje (EPA) uliofanyika kati ya 2005 na 2006.

Kuna taarifa kwamba baadhi ya fedha zilizochotwa zilitumika katika kampeni za chama hicho kwa njia ya watu wa kati.

Yaani hawa ni wale wale waliochota "walipewa sharti moja kwamba wapeleke baadhi ya mabilioni katika kampeni kuisaidia CCM."

Kuna kila dalili kwamba hayo yalifanyika. Kwanza ni kutokana na matumizi ya kampeni ya chama hicho kuwa makubwa mno, na watu walishangaa wapi CCM imepata fedha zote hizo.

Wenye macho walijua mapema kuwa mamilioni yale hayakupatikana kwa njia halali. Maana kama yangekuwa yamepatikana kwa njia halali, CCM isingeweza kuyatapanya kiasi kile.

Kutokana na hali hiyo, sakata la EPA linaiweka katika hali ngumu sana serikali ya Rais Jakaya Kikwete iliyojitosa au iliyoshinikizwa na wafadhili, wapinzani na vyombo vya habari kulichunguza.

Swali linalokuja mara moja ni je, iwapo ni hivyo, itawezekana kwa serikali ya CCM kujianika yenyewe mbele ya wananchi, kwa kusema kwamba ni kweli baadhi ya pesa za EPA ziliingia katika kampeni zake?

Mara moja wapinzani na wananchi wengine watapata nguvu na kusema, "Siku zote tumekuwa tukisema kuwa ushindi wa CCM siyo wa halali."

Hilo likitokea, jambo moja la wazi litakaloashiria ni mwisho wa CCM, ingawa mwisho huo, inavyoonekana, hauwezi kuepukika, kutokana na jinsi siku zinavyokwenda.

Kila kukicha wananchi wanazidi kuhoji kauli za viongozi wa chama tawala na hivyo kukataa kuendelea kuburuzwa.

Tukirudi huko Zimbabwe, kitu kikubwa anachokitumia Mugabe katika "kuhalalisha" ushindi wake katika kila uchaguzi ni ajenda aliyonayo mkononi, yaani lile suala la ardhi.

Suala jingine ni lile la ukombozi wa nchi na vita iliyopiganwa kuikomboa Zimbabwe, ingawa hili halina nguvu sana sasa hivi kutokana na ukweli kwamba Wazimbabwe wengi ambao wamo katika upinzani pia walishiriki vita ya ukombozi.

Ni kweli suala la ardhi hutumiwa sana na Mugabe katika kampeni kama vile kuwaambia wapinzani kwamba wao wako upande wa Wazungu walowezi, au tuseme Wazungu hao wako upande wao, kwa hivyo wao ni vibaraka.

Inawezekana kuwa Wazungu wako upande wa upinzani na hupewa msaada mkubwa, lakini kuna hoja pia kwamba Mugabe hulitumia suala hilo wakati wa uchaguzi tu kujipatia kuungwa mkono.

Baada ya ushindi basi halishughulikii kabisa suala hilo na kungojea hadi uchaguzi mwingine. Limekuwa ni suala lisiloisha, tangu aingie madarakani mwaka 1980.

Wadadisi wengine wa masuala haya wanasema kuwa suala la ardhi linamfanya Mugabe kupata sababu ya kushindwa kuyashughulikia masuala mengine ya uchumi wa nchi hiyo ambao umekuwa unazorota na kuwafanya wananchi kuwa masikini kupindukia.

Wadadisi hao wanasema kuwa usomi wa kiongozi huyo (ana digrii 6) umeshindwa kumpa busara ya kuweza kulishughulikia suala la ardhi, badala yake amekuwa akitawaliwa na jazba.

Hutumia historia kama vile damu ilivyomwagika katika kupata uhuru na jinsi Wazungu walivyoendelea kutawala uchumi.

Hapa kwetu hali ya namna hiyo, kwa kiasi kikubwa iko Visiwani ambako watawala walio madarakani wamekuwa wakisema kuwa hawatatoa nchi kwa wapinzani kwa njia ya vipande vya karatasi (kura).

Hii inatokana na Mapinduzi ya mwaka 1964 yaliyoung'oa utawala wa Kisultani, na hivyo wao tu kujiona ndiyo wanaostahili kutawala milele.

Hali hii imesababisha kukwama kwa mambo mengi ya maendeleo na kuongeza umasikini.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: