Mukama anaakisi ya Yussuf Makamba


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 11 April 2012

Printer-friendly version

YAPO mengi yametokea nchini katika kipindi  cha wiki moja iliyopita. Haya ni pamoja na kuvuliwa ubunge kwa mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema; kifo cha msanii wa  filamu, Stephen Kanumba na Chama cha Demokarasia na Maendeleo (CHADEMA), kupitia mgombea wake, Joshua Nassari, kushinda uchaguzi mdogo wa kiti cha ubunge, Arumeru Mashariki.

Ukiyajumuisha matukio haya pamoja na yaliyojiri barani Afrika kwa wiki moja iliyopita, kama kifo cha Rais Bingu wa Mutharika wa Malawi na kuibuka kwa rais wa pili mwanamke Afrika, Joyce Banda ambaye amerithi nafasi ya Mutharika, uwanja wa mijadala umesisimka zaidi.

Pamoja na matukio haya makubwa ya kusisimua, bado mwangwi wa uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki ungali unatetemesha ngoma za masikio ya wengi hasa namna kampeni zilivyofanyika na kuibuka siasa za matusi ambazo zinaelekea kuungwa mkono na wakubwa wa chama tawala.

Mmoja wa waatu waliovunja rekodi ya kuporomosha matusi katika kampeni hizo ambaye hakika alistahili nishani ya matusi, ni Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde aka Kibajaji.

Huyu alivunja miiko ya uongozi, alikanyaga wadhifa wake na kwa hakika aliwatukana hata waliompigia kura kwani wamejikuta wakijiuliza maswali magumu kama kweli huyo ndiye aliyewaomba kura mwaka 2010 ili awawakilishe kwa hoja si katika bunge tu, bali kokote atakakokuwa akizungumza sauti za Wanamtera zisikike.

Watu wanajiuliza pamoja na uzee wa John Malecela, huyu ndiye mrithi wa jabali hili la siasa za Tanzania? Mwaka 2015 majibu yaweza kupatikana.

CCM ina mzizi kutoka mbali; kiliasisiwa na kujengwa juu ya misingi ya uadilifu, utu na kwa kweli kujitoa kwa ajili ya kutetea wanyonge; wakati wote hoja na ujenzi wa hoja ulitarajiwa kuwa ungekuwa msingi wa kuendelea kutawala kwa chama hiki chenye nasaba na Tanu. Tanu haikupigana vita ya kumwaga damu, ilijenga hoja katika kudai uhuru.

Kama Tanu miaka zaidi ya 55 iliyopita ilijiegemeza katika kujenga hoja, kusikiliza na kushawishi kwa hoja, haiwezekani leo miaka 50 baada ya uhuru kile chama kilichorithi mikoba yake kishindwe kuendeleza misingi hiyo.

Kama kimeshindwa basi kuna kila sababu ya kujiuliza maswali mengi, kubwa ni hili kama Lusinde ndiyo kizazi kipya na damu mpya ya viongozi waliopikwa ndani ya CCM, basi tunaweza kupata majibu kwa nini kama taifa tumekwama mkwamo mkubwa na mbaya.

Pengine hali hii isingesumbua sana kama matusi ya nguoni ambayo Lusinde aliyaporomosha kule Arumeru dhidi ya viongozi wa CHADEMA yangebakia kuwa yake binafsi, lakini kuna kila dalili yalibarikiwa na chama, kuanzia Arumeru kwenye kambi ya kampeni ya mgombea wa CCM, Sioi Sumari, hadi makao makuu ya chama.

Akizungumza na waandishi wa habari aliowaita wiki iliyopita, Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama, alizungumza mambo mengi, mojawapo ni swali aliloulizwa na waandishi juu ya kauli yake kuhusu matusi aliyoporomosha Lusinde kule Arumeru.

Mukama hakutafuna maneno, alisema  wazi kuwa haoni ubaya wowote wa matusi yale. Alijitetea kuwa Lusinde alikuwa akijibu mapigo dhidi ya CHADEMA!

Mukama si karani wa CCM, ni Katibu Mkuu wa CCM, si mhudumu, si mtu wa hivi hivi tu, ndiye mtendaji mkuu wa chama hicho, anapaswa kuongozwa na vitu vitatu; mosi, katiba ya chama; pili miongozo ya chama; na tatu kanuni za chama.

Haitarajiwi kiongozi wa aina ya Mukama, kwa hali yoyote ile, kuunga mkono matusi yanayotolewa kwa niaba ya chama chake, iwe hadharani au sirini.

Matusi ni kielelezo cha kuchoka kufikiri; ni kufilisika kifikra na kuamua kutafuta njia nyepesi ya kihuni ya kufurahisha umati.

Kama akina Lusinde wamebarikiwa na Mukama na kupewa hiyo anasa ya kuacha kufikiri na kuporomosha matusi, basi na sasa ijulikane wazi kwamba matatizo ya taifa hili chini ya uongozi wa CCM hakika hayana wa kuyasemea.

Kuna wakati napata tabu sana kuelewa kwa uhakika kazi ya chama tawala kama CCM ni nini kikishapitisha wagombea nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi mkuu.

Kwamba kinapata wenyeviti wa vijiji, vitongoji na mitaa, madiwani na mameya, wabunge na kushinda kiti cha urais, je, kina nguvu gani ya kuisimamia serikali kutekeleza majukumu yake? Kina ubavu huo?

Miaka ya nyuma ilikuwa ni rahisi zaidi kusikia tuhuma za rushwa zikitajwa ndani ya serikali, uvunjaji wa maadili ya uongozi ni jambo lililowezekana ndani ya serikali pia, lakini kwa hakika chama pamoja na ukweli kwamba kilikuwa kinaonekana kujaa watu wasiokuwa na uwezo, kwanza wa kifedha na hata kielemu, bado kilishikamana sana na misingi ya uadilifu.

Chama kilichukuliwa kama kioo, malalamiko dhidi ya serikali yalipelekwa kwenye chama, siku hizi chama kimegeuzwa kuwa kichaka cha watu waliopoteza dira na mwelekeo. Matusi ya Lusinde hayakuwa ya bahati mbaya, ni msimamo mpya na mwelekeo mpya wa chama.

Mukama anachukua mikoba ya aliyekuwa Katibu Mkuu kabla yake, Yusuf Makama, ambaye hakubariki tu matusi muda aliokalia kiti cha ukatibu mkuu wa CCM, bali aliwatafuta wahuni walioshindikana kutoka vyama vya upinzani na kuwapa nafasi ndani ya chama kama watendaji.

Kazi yao kubwa ilikuwa kuporomosha matusi dhidi ya vyama vya upinzani; kuendesha hila na kila aina ya ghilba. Hawa walijaa pale ofisi ndogo ya makoa makuu Lumumba.

Nitawakumbusha walau jambo moja dogo tu lakini lina maana kubwa sana kwa mustakabali wa taifa kwa sasa.

Wakati muswada wa sheria ya kuunda tume ya kuratibu mchakato wa kuandika katiba mpya unajadiliwa na wananchi katika makongamano mbalimbali mwaka jana, jijini Dar es Salaam mkutano ulifanyika ukumbi wa Karimjee.

Siku ya kwanza ya mkutano huo Tambwe Hiza wakati huo akiwa anasimamia kitengo propaganda cha makao makuu CCM Lumumba, alipata wakati mgumu sana wakati akitoa maoni yake hali iliyomlazimu kukatisha hotuba yake.

Kesho yake aliamua kuwakusanya watoto kutoka matawi ya CCM mkoa wa Dar es Salaam na kuwajaza ukumbi wa Karimjee kabla ya saa mbili, nia ikiwa ni kuuvuruga mkutano huo. Watoto hao walikuwa na kazi mbili katika mkutano huo, kwanza kuhakikisha wenye hoja hawapati pa kukaa na hivyo kutawala ukumbi, lakini pili hata wale wachache waliopata fursa ya kuingia na kuujadili muswada huo, walijikuta wakizomewa na hao watoto wa Tambwe. Huu ni uhuni ulioasisiwa kutoka makao makuu ya CCM Lumumba.

Kwa hiyo, kuibuka kwa Lusinde Arumeru na matusi yake, na kuungwa mkono na Mukama, si mambo yanayostahili tena kushangaza wengi, kwa sababu kidogo kidogo CCM imeamua kujirahisisha na kuamini katika siasa za kuahirisha kufikiri, kukataa kukabiliana na changamoto za nyakati hizi zinazokabilia taifa hili, matokeo yake ni kutumia matusi kama majibu ya hoja nzito zenye kuhitaji fikra pevu za kukidhi kiu ya nyakati za sasa. Niliamini Mukama ni tofauti na Makamba, kumbe ni wale wale.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: