Mukama anasahihisha na kupakazia


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 11 May 2011

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli

WAHARIRI kadhaa walihudhuria mkutano ulioitishwa na Katibu mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilson Mukama Mei 2, mwaka huu kwenye hoteli ya Peacock, Dar es Salaam.

Mwalimu huyo wa zamani wa Chuo cha Kivukoni na baadaye Taasisi ya Usimamizi wa Fedha (IFM), aligeuza mkutano huo, uliolenga kutambulisha sekretarieti mpya ya CCM kuwa “semina” ili asahihishe dhana, aelimishe chimbuko, na afafanue falsafa ya CCM kujivua gamba.

Katika “semina” hiyo, Mukama akijaribu kupangua maswali chokonozi dhidi ya chama chake, na mwishoni aligeuza vichwa vya wahariri kuwa majalada ya kutupia takataka za fikra za CCM ili wakachapishe.

Hata hivyo, hakutarajia kukumbana na swali lililodai CCM inakufa.

“Mwalimu Julius Nyerere amewahi kuikosoa CCM na pia aliyekuwa katibu mkuu Horace Kolimba amewahi kusema CCM imepoteza dira…na sasa mmeanzisha utaratibu wa kujivua gamba ambao unaua chama. Katibu huoni kwamba CCM inakufa?” aliuliza mhariri mmoja.

Mukama alijibu: "Ndugu yangu…CCM itaendelea kuwepo daima, kwani ni chama kilichoanzishwa kwa misingi imara, kina sera na ilani inayotumika kuongoza nchi.

“Huwezi kulinganisha na CHADEMA kilichoanzishwa kwa fedha za fedha za Shirika la Fedha Duniani (IMF) baada ya muasisi wake kutofautiana na Mwalimu Julius Nyerere. Ndiyo CHADEMA itakufa mara 100 kabla ya CCM. Haya mambo yamefanyika baada ya utafiti wa kina na kisayansi, hatukukurupuka hivi hivi...” alisema.

Majibu hayo ambayo yalionekana kukera vichwa vya wahariri yalisababisha wengi kuashiria mwisho wa “semina” ile.

Mukama anaweza awe aliwaita wahariri kuwaambia historia isiyojulikana kuhusua namna vyama vya siasa vilivyoanzishwa nchini. Maana kama kila mmoja anajua, uzushi huu wa nini?

Nguvu za IMF

Baada ya kumalizika vita dhidi ya nduli Idi Amin wa Uganda mwaka 1979, uchumi uliharibika sana. Nchi wafadhili, Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia (WB) walitoa maoni juu ya njia ambazo nchi ingeweza kujikwamua.

Njia hizo ni pamoja na kuruhusu uchumi huria wa ndani na kuachia thamani ya fedha ilingane na hali yake halisi. Kwa wakati ule IMF ilitaka thamani ya shilingi ishuke.

Waziri wa Fedha na Gavana wa kwanza wa Benki Kuu, wakati ule Edwin Mtei aliunga mkono lakini alipingwa na Mwalimu Nyerere. Mtei alidhani haeleweki, akafanya mpango kuwapeleka, nyumbani kwa Mwalimu, kule Msasani maofisa wa IMF ili wafafanue faida zake.

Katikati ya mazungumzo yao, Mwalimu Nyerere alitoka nje na kuwaacha wageni hao na pale Mtei alipomfuata kumwambia wageni wanaondoka aliawambiwa awatoe nchini haraka sana. Mtei aliandika barua ya kujiuzulu uwaziri mwaka 1979 ili ampe Rais fursa ya kuteua mtu mwingine.

Katika kipindi chote hicho nchi hii ilikuwa inatawaliwa na mfumo wa chama kimoja—CCM. Ulikuwa uhaini kuanzisha chama kingine cha siasa.

Ingawa Mwalimu Nyerere alikataa ushauri wa Mtei na IMF, hatua iliyosababisha wananchi kuandamana nchi nzima kuunga mkono, miezi michache baadaye, serikali ya CCM ilishusha thamani ya shilingi.

Isitoshe Mwalimu Nyerere hakumtupa Mtei moja kwa moja, aliendelea kumtumia alipohitajika, ndiyo maana aliafiki uteuzi wa Mtei kuwa mkurugenzi wa IMF kanda ya Afrika kwa nchi zinazozungumza Kiingereza.

Ajabu ni kwamba baada ya Mwalimu Nyerere kung’atuka mwaka 1985 serikali ileile ya CCM iliyokataa ushauri wa kuchepua haraka uchumi, ilikubali masharti yote ya IMF, WB na nchi nyingine wafadhili hadi sasa wanajiuzia nyumba za serikali.

Aidha, serikali ya CCM ikaanza kupokea misaada kutoka IMF/ WB kwa ajili ya kuendesha nchi chini ya masharti magumu yanayonyonga wananchi.

Vilevile, serikali ya CCM ambayo, kwa muda mrefu, imepuuza shinikizo kutoka kwa wasomi mbalimbali waliotaka mfumo wa chama kimoja uondolewe, ilitii masharti ya wafadhili, IMF na WB kwamba urejeshwe mfumo wa vyama vingi ili vifanye kazi ya kusimamia na kukemea serikali.

Hapo ndipo, ili kujenga uhalali wa kisheria, ililazimika kuandaa waraka kupata maoni ya wananchi uruhusiwe mfumo wa vyama vingi au la. Inadaiwa asilimia 80 ya waliohojiwa walitaka chama kimoja huku asilimia 20 wakitaka vyama vingi.

Serikali haikuwa na ujanja; ikaacha utaratibu wa wengi wape ikaruhusu vyama vingi kwa sheria mwaka 1992, mfumo ambao sasa unaihenyesha CCM.

Walionufaika na marekebisho hayo ya sheria, kwanza kabisa ni Kamati ya Mageuzi ya Ujenzi wa Taifa (NCCR) ambayo iligeuka kuwa chama cha siasa ambacho kilisajiliwa Januari 21, 1993 na kuitwa NCCR-Mageuzi. Siku tatu baadaye yaani Januari 23, 1993 CHADEMA kikasajiliwa na vyama vingine vikaendelea kupata usajili hadi leo.

Kundi la pili kunufaika na marekebisho hayo ya sheria ya vyama vingi ni la watu waliofungwa kwa madai ya uhaini. Waliachiwa huru kurudi uraiani.

Aidha, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na katibu mkuu wa TANU, Oscar Kambona aliyekimbilia Uingereza baada ya kutofautiana na Mwalimu Nyerere alirejea nchini na kuanzisha chama cha Tadea. Kwa hiyo ni hoja mfilisi ‘kufundisha’ CHADEMA ilianzishwa kwa fedha za IMF.

Mkanganyiko

Tangu CCM walipopitisha msimamo mmoja kwenye mkutano wa Halmashauri kuu mjini Dodoma mwezi mmoja uliopita, wameyumba na wamesigana; hawana tena msimamo mmoja kuhusu kinachopaswa kufanyika dhidi ya watuhumiwa wa ufisadi.

Mathalani, akirejea hotuba ya Rais Kikwete katika kikao hicho, Mukama alisisitiza kwamba chama hakitakuwa na ajizi kwa watuhumiwa hao lakini alidai hakuna mahali popote walipotajwa.

Lakini alipopewa nafasi Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alikiri kutaja watuhumiwa hao kuwa ni wale wanaotajwa katika kashfa za Richmond na rada.

Hapa Nape alimaanisha mfanyabiashara na mbunge wa Igunga Rostam Aziz na aliyekuwa Waziri mkuu, Edward Lowassa wanaotajwa katika Richmond, na katika kashfa ya rada ni Andrew Chenge aliyekuwa Waziri wa miundombinu.

Mwenyekiti wao, Rais Kikwete ana yake moyoni. Amekutana na wanachama hao kutuliza vumbi la ‘mikingamo’ ya Nape yanayotaja kuwa wao ndio magamba ya kuvuliwa.

0789 383 979
0
No votes yet