Mulee ameshinda anazomewa, tumfanyeje Maximo?


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 01 April 2008

Printer-friendly version
Miaka miwili hana First Eleven Stars!
Sasa tuhoji kazi ya Marcos Tinocco

KENYA kupitia timu yake ya taifa ya Harambee Stars, imeanza vyema kampeni za kuisaka tiketi ya fainali za kwanza za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za nyumbani, baada ya kuizamisha Tanzania kwa bao 1-0.

Harambee Stars itahitaji sare ya aina yoyote kuvuka, ingawa hilo ni suala la kusubiri kutokana na ari ya wachezaji wa Taifa Stars ya Tanzania.

Lakini kwa Wakenya, ushindi huo si lolote, wamechukia na kumporomoshea matusi kocha wao, Jacob "Ghost" Mulee, wakidai timu anayoifundisha, haikucheza vizuri.

Hawakubabaika na matokeo, bali soka maridadi yenye kuburudisha. Hawakuangalia pia muda ambao kocha alipewa kuiandaa timu.

Hawakuangalia mambo mengine kama mikasa ya kufungiwa kwa nchi hiyo katika medani ya kimataifa na hata kuvunjwa kwa ligi za ndani.

Wao walichokijali ni matokeo mazuri, soka nzuri, basi. Kwa hili, Mulee anayeinoa pia klabu ya Tusker, anastahili pole.

Swali linakuja, kama Mulee aliyekaa na timu kwa muda mfupi, lakini akaibuka na ushindi, anazomewa, akiwa amepata ushindi, vipi Watanzania na kocha wao, Marcio Maximo?

Tofauti na Mulee, Maximo amekaa na timu kwa takribani miaka miwili sasa, lakini tusidanganyane, hajapata kikosi cha kwanza, First Eleven.

Kila kukicha ni Stars mpya, kila mechi ni kikosi kipya na kila mashindano ni kikosi kipya, achilia mbali mechi za kirafiki kama inayokuja ya Yemen, nayo inakuwa na kikosi chake.

Pamoja na dhamira nzuri ya Maximo ya kujaribu kuangalia vipaji tofauti, dalili zinaonyesha sasa anaishi kwa matumaini na ameishiwa mbinu.

Na hili linajidhihirisha na jinsi timu inavyocheza bila ya mpangilio, labda ikitegemea tu juhudi binafsi za wachezaji, kila mmoja akijitoa mhanga kwa lengo la kujihakikishia kubaki kundini.

Lakini kwa soka ya kujipanga katika maana halisi ya kusaka ushindi, Stars imepoteza mwelekeo, na leo hatuwezi kuingia uwanjani wa kuwa na uhakika wa kuifunga hata Somalia, jambo lililokuwa linalonekana kuanza kuondoka kutokana na mwanzo mzuri aliokuwa nao Maximo wakati anaichukua timu.

Tujiulize, kutokana na kukaa na timu kwa muda mrefu, kila siku akishuhudia mechi za ligi kuu, Watanzania wachukie na kuanza kumzomea? Hapana, amerithi mfumo mbovu wa soka na nchi yetu.

Sawa, hicho ndicho kilichomleta, aifufue soka yetu, lakini anaonekana amekata tamaa, sasa akisubiri ratiba, anaita kikosi, tena wakati mwingine akiwaacha watu wakiguna, ili mradi aingize timu uwanjani.

Je, kwa staili hii, Maximo ataweza kukidhi kiu ya Rais Jakaya Kikwete na Watanzania wenye shauku ya kurudisha makali ya soka ya miaka ya 1970 na 1980?

Kwa muda inawezekana, lakini inatia shaka kwamba, pengine wakati Maximo akipata mwelekeo, anaweza kujikuta akibaki na wachezaji wazee zaidi.

Nasema Wazee zaidi kwa sababu baada ya mechi ya mwishoni mwa wiki jijini Nairobi, Mulee aliiponda Taifa Stars akidai anamshangaa Maximo kwa kujaza wachezaji wazee.

Alikaririwa akisema: "Kocha wenu (Maximo) amenishangaza kwa kuamua kuchagua wachezaji wazee sana, si wazuri na hawana muda mrefu wa kuitumikia timu.

"Angalia kikosi changu, ni vijana, wengi wenye umri wa chini ya miaka 23. Hawa ndio watakaokuwa warithi wa nyota wa Harambee Stars wa sasa."

Ni maneno ya kejeli, lakini yana ukweli, na ukweli huo ndio wanaouhisi wanazi wa soka nchini.

Yanapaswa kuwachoma kwa sababu, Rais Kikwete na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limehakikisha nchi inakuwa na mfumo mzuri wa soka kuanzia ngazi za chini kwa kumleta kocha wa vijana, Marco Tinocco.

Lakini inashangaza na kusikitisha. Tinocco tuliyetarajia angeichangamsha soka nchini, anaonekana hana la kufanya.

Kila kukicha ni kuzunguka na Maximo, hivyo kuwa asiye tija kwa kile kilichomleta nchini.

Alianza vyema kwa kuchagua kombaini ya Kombe la Coca Cola, umepita mwaka hatujasikia lolote, na mbaya zaidi, hata wachezaji wale walioonekana kuwa nyota zaidi kiasi cha kupewa ofa ya kwenda Brazil, hawajulikani waliko. Wamekufa kisoka na kupoteza makali yao.

Huku ni kukuza au kuua vipaji? Kocha wa vijana atakaaje mwaka mzima bila ya kuita kikosi chake angalau kuangalia vipaji kila baada ya muda fulani? Kocha huyo huyo anakaa mwaka mzima bila ya kuibua kipaji kipya!

Maswali ni mengi, lakini huu ni wakati mwafaka kuwasaidia (si kuwaingilia katika majukumu yao), Maximo na Tinocco angalau kwa ushauri, ili warudi katika mstari.

Vinginevyo, hisia za kumzomea kocha kama ilivyokuwa kwa Mulee hazitazuilika tena, kwani itafika siku uvumilivu utakoma, labda dalili za nyota njema zianze kufufuliwa sasa.

0
No votes yet