Mungu awaambia Watanzania: Msiogope


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 22 September 2010

Printer-friendly version

NENO “usiogope” limeandikwa mara 365 katika Biblia Takatifu. Hii ina maana Mwenyezi Mungu amekuwa akiwaambia waja wake, kila siku, kwamba wasiogope.

Mungu leo anawaambia Watanzania,“msiogope;” Tanzania yenye neema inawezekana bila Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinachoongozwa na Mwenyekiti Jakaya Kikwete.

Mungu anasisitiza “msiogope, fungueni macho yenu na akili zenu mtazame” mageuzi na ufanisi uliofikiwa katika nchi za Afrika Mashariki na Kati baada ya kuviondosha vyama vilivyoleta uuhuru.

Katika nchi hizo maarufu kama Maziwa Makuu, vyama vikongwe, vilivyopigania uhuru, ambavyo leo hii vimechoka, vimeondolewa madarakani kwa amani – kwa njia ya kura – na nchi hizo zinasonga mbele kimaendeleo.

Hatua kwa hatua

Ingawa Dominique Mbonyumutwa aliiongoza Rwanda kama rais wa muda (Januari 28 hadi Oktoba 26, 1961), Grégoire Kayibanda ndiye alikuwa rais wa kwanza wa nchi hiyo akiongoza Chama cha Parti du Mouvement de l'Emancipation du Peuple Hutu (PARMEHUTU).

Lakini leo hii, tena baada ya ‘kuzichapa’ wenyewe kwa wenyewe mwaka 1994 kutokana na misingi ya ukabila, Rwanda chini ya Rais Paul Kagame wa chama cha Rwanda Patriotic Front (RPF), imepiga hatua kubwa ya kimaendeleo na ni mfano wa kuigwa.

Kazi kubwa iliyofanywa na Unity for National Progress (UPRONA) chini ya Prince Louis Rwagasore ilikuwa kupigania uhuru wa Burundi.

Lakini leo, baada ya miaka kadhaa ya vurugu za wenyewe kwa wenyewe kutokana na tofauti za kikabila, nchi hiyo inaongozwa kwa ‘amani’ na Pierre Nkurunziza wa National Council for the Defense of Democracy-Forces for the Defense of Democracy (CNDD-FDD).

Chama cha Kenya National Union (Kanu) kilicholeta uhuru nchini Kenya kikiongozwa na Jomo Kenyata, kiliachwa salama kwenye mikono ya Daniel arap Moi. Alipostaafu aliondoka nacho.

Kuanzia mwaka 2002 Kenya iliongozwa na NARC-Kenya (ushirikiano wa vyama vya siasa) chini ya Mwai Kibaki. Baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007, Kenya inaongozwa na Kibaki wa Party of National Unity (PNU) kwa ushirikiano na Orange Democratic Movement (ODM) cha Waziri mkuu, Laila Odinga.

Mafanikio makubwa waliyopata Kenya ni kutengeneza katiba mpya iliyoridhiwa na mamilioni ya wananchi.

Kenneth Kaunda aliwaongoza Wazambia kudai uhuru chini ya United National Independence Party (UNIP) na akawa rais wa kwanza.

Kutokana na mchoko, kujisahau au uzee, UNIP kilipoteza dira na kung’olewa mwaka 1991 na Frederick Chiluba aliyeunda Movement for Multiparty Democracy (MMD). Leo Zambia inaongozwa na Rupiah Banda.

Uganda ilipata uhuru wa kisiasa chini ya chama cha Uganda Peoples Congress (UPC) cha hayati Apolo Milton Obote (UPC).

Pamoja na athari kubwa kiuchumi iliyopata kutokana na vita dhidi ya Idd Amini na baadaye vita vya wenyewe kwa wenyewe, nchi hiyo imepata mafanikio makubwa ya kiuchumi chini ya National Resistance Movement (NRM) cha Yoweri Museveni tangu mwaka 1985.

Mabadiliko hayo, katika Nchi za Maziwa Makuu, ndiyo yanayovuma “vibaya” kwa CCM, kwamba kumbe vyama vilivyoleta uhuru vinaweza kuondolewa na nchi ikabaki salama. Madai kwamba nchi bila CCM itayumba, ni ghiliba za kisiasa na hazifai kusikilizwa.

Vyama vilivyoleta uhuru katika nchi hizo viliyumba na nchi zikayumba; hivyo viliondolewa kwa maslahi ya taifa. Kwa kuwa CCM imeyumba na nchi ikayumba, dawa pekee ni kuondoa chama madarakani.

Sera za CCM zimeyumba; mipango yake imetetereka, ubunifu wa viongozi umekwisha, upeo umeota ukungu na matumaini yamepotea. Katika hali hii, CCM na viongozi wake wakiondolewa, kamwe nchi haiwezi kuyumba.

Mtu yeyote atakayetoa mifano ya Burundi na Rwanda atakuwa mjinga. Ukabila ni moja vya viini vya mapigano katika nchi hizo; ukichochewa na utawala wa kikoloni uliotaka kuwagawa wananchi ili uwatawale kwa kuwaswaga kama kondoo.

Siyo siri kwamba pale walipoweka mguu, wakoloni walichagua wa kutumia ili kutawala; na kwa njia hiyo walikuza migongano midogo ikawa mikubwa; kupanda mbegu ya mgawanyiko na taswira za “mimi ni bora kuliko yule.”

Hali hiyo ndiyo inaiangamiza Somalia ya hayati Siad Bare tangu mwaka 1991 alipopinduliwa (dini moja, kabila moja lakini tofauti ni ukoo upi bora).

Mabadiliko ya Malawi ya Dk. Hastings Kamuzu Banda ambayo leo inaongozwa na Bingu wa Mutharika ni mfano mwingine kwamba CCM inaweza kuondolewa madarakani na nchi ikabaki na amani na utulivu.

Malawi ilitawaliwa kwa miaka mingi na Rais Banda chini ya chama cha Malawi Congress Party (MCP). Aliondolewa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1994; akaingia Bakili Muluzi wa United Democratic Party (UDP).

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2004 Muluzi aliamua kukaa kando, akapendekeza Mutharika awe mgombea urais. Lakini baada ya kupata ushindi wa kushindo, Mutharika alihitilafiana na mtangulizi wake katika masuala ya msingi. Alimfungulia Muluzi kesi ya ufisadi ambayo anahangaika nayo kortini hadi leo.

Mutharika alifanya mambo mengine mawili makubwa. Kwanza, alihama ikulu akidai imejaa mashetani. Pili, alianzisha chama cha Democratic Progressive Party (DPP), ambacho kinaongoza mapambano dhidi ya ufisadi. Malawi leo ina neema ya chakula na ustawi wa uchumi.

Ujumbe wa Mutharika
Watanzania wanaohudhuria mikutano ya kampeni za vyama vya siasa wanaweza kujifunza kutokana na somo la Bingu wa Mutharika.

• Kwamba kama kweli wanataka maendeleo waachane na CCM kwa sababu imeshindwa kupambana na ufisadi na badala yake imewaletea wananchi ugumu wa maisha.
• Mwenyekiti imara anaweza kukifanya chama kuwa imara na nchi imara. Kwa bahati mbaya, CCM ina mwenyekiti anayeonekana kuitika “hewala” kwa sauti za mafisadi na wawekezaji.
• Mutharika alihama ikulu akisema ina mashetani. Hii ni sababu nyingine ya kuihama CCM yenye mashetani kwa vile mwenyekiti wake amepewa ulinzi wa mashetani na mnajimu, Sheikh Yahaya Hussein. Kama mwenyekiti wa CCM analindwa na maruhani, chama chake kitakuwa kinalindwa na mitambo ya maruhani.
• Vyama vilivyoleta uhuru vimegeuka kuwa maficho ya viongozi mafisadi. CCM ya sasa imekuwa maficho ya waliokula rushwa ya ndege na rada, waliojiuzia mgodi wa Kiwira, waliovimbiwa kwa ukwapuaji wa mabilioni ya shilingi uliofanywa na makampuni ya Meremeta, EPA na Richmond.
• Mutharika anawaambia Watanzania kwamba ikiwa chama kitatekwa na mafisadi, basi hata serikali itatekwa na mafisadi na itatumikia mafisadi. Dawa ni kuhama. Dawa bora zaidi ni kukitosa.

Alichofanya Bingu wa Mutharika ni uthibitisho kuwa Tanzania bila CCM na bila Kikwete itakuwa na ufanisi wa hali ya juu.

Vyama vikongwe vilikuwa kwa ajili ya kuleta uhuru wa bendera. Jukumu hilo limetimizwa. Sasa vyama vipya vyenye fikra mpya, ndiyo nyenzo ya kufikia maendeleo endelevu.

0
No votes yet