Mungu, wachawi na uchaguzi


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 27 October 2010

Printer-friendly version

NI mahojiano ya chapuchapu, kwenye kaunta ya M.S. Hotel jijini Mwanza, Jumatano 27 Oktoba 2010. Ndimara Tegambwage aliyeko hapa kwa ushauriano na waandishi wa habari wa kanda ya Ziwa Viktoria, anakutana na Fikiri Mabula na kwa muda mfupi anapata “fikra” za binti mdogo juu ya Mungu, uchawi na uchaguzi mkuu wa 31 Oktoba. Fuatilia.

Swali: Wewe unaonekana mdogo. Unafanya kazi hapa?

Jibu:  Hapana. Nimemfuata dada yangu. Kwa nini unauliza hivyo?

Swali:  Niliona kama mwenyeji vile; halafu nikaona kwa umri huo usingekuwa mfanyakazi.

Jibu:  Siyo mfanyakazi hapa lakini natafuta kazi.

Swali: Una umri gani?

Jibu:  Mimi? Miaka mingi.

Swali: Miaka mingi mingapi? Kama yangu?

Jibu:  Ehee! Miaka 22.

Swali: Una watoto wangapi?

Jibu:  Mimi? Mmoja tu.

Swali: Ungetaka kuwa na wangapi?

Jibu:  Wengi.

Swali: Wengi ni wangapi?

Jibu:  Watano.

Swali: Wote hao utaweza kuwatunza na kuwasomesha shule?

Jibu:  Eee, wewe vipi? Hivyo hivyo tu. Sasa nikizaa…kwani wewe ungetaka nizae wawili au watatu?

Swali: Unaniuliza mimi tena? Naona ungekuwa na watatu tu.

Jibu:  Watatu? Watatu tu?

Swali: Si ndiyo? Halafu urudishe mwili; utulie na kutafuta njia za kuwalea na kuwasomesha.

Jibu: Mimi naona nizae watoto watano.

Swali: Wote hao wa nini?

Jibu: Sikiliza. Nikizaa watano, Mungu atachukua mmoja; dunia itachukua mmoja na wachawi watachukua mmoja. Nitakuwa nimebakia na hutu tuwili (akionyesha kwenye vidole).

Swali: Kwani Mungu anahitaji mtoto wako?

Jibu:  Eee! Imeandikwa. Yeye akitaka anachukua wakati wowote.

Swali: Aache kuchukua mtu mzima kama mimi hapa achukue kifaranga chako?

Jibu:  Eee! Hata akichukua mtu mzima; atakuwa amechukua mtoto wangu. Yeye anaamua lini anataka kumchukua; uwe mdogo au mkubwa.

Swali: Na wachawi je? Wana sababu gani ya kuchukua mtoto wako?

Jibu:  Wewe! Wenye roho mbaya; hawapendi kuona mtu akipata kitoto chake kizuri.

Swali: Mbona watoto wazuri wako pote duniani. Hivi wachawi hawajawaona au wameelemewa kwa kuwa dunia ni kubwa?

Jibu:  Labda huko kwingine hakuna wachawi; lakini katika maeneo yetu haya, wapo na wana roho mbaya kweli.

Swali: Au dini ndiyo imepunguza wachawi?

Jibu:  Inaonekana wewe hujui mambo mengi. Hao wanaoonekana waumini wakuu ndio wanakamatwa kila siku wakifanya uchawi makaburini; lakini Jumapili au Ijumaa ndio wako mbele karibu na mchungaji au sheikh.

Swali: Wewe ni mwislamu au mkristo?

Jibu:  Mimi mwislamu.

Swali: Lakini kwa ulivyoelezea waumini wachawi, ina maana kuwa huendi msikitini kusali.

Jibu: Naenda. Mimi ni mwislamu lakini dada zangu wawili na baba, ni wakristo. Kila mmoja na madhehebu yake. Mimi nimekaa upande wa mama.

Swali: Hapo nyumbani hamgombani kwa kuwa na imani tofauti?

Jibu:  Tugombanie nini? Kila mtu anaamini vyake. Kuna mambo yanayofahamika kuwa ni mabaya, kama wizi, uchawi, hayo mmoja wetu akiyafanya lazima tutagombana.

Swali: Je, kama mnatofautiana kisiasa?

Jibu: Kisiasa? Hayo si mambo ya wanasiasa? Sisi kazi yetu kupiga kura tu.

Swali: Si mnaweza kugombania nani awe diwani, mbunge au rais?

Jibu:  Wewe unachekesha. Tugombanie chakula cha wengine? Kwa nini? Mimi kwa mfano, nitapiga kura kwa mara ya kwanza. Nitampigia Kikwete. Wengine wote pale nyumbani wanasema watampigia Dk. Slaa. Sasa ugomvi utatoka wapi? Kila mtu na chaguo lake.

Swali: Kwa nini unataka kumpigia Kikwete?

Jibu:  Wewe unataka niseme mengi. Kwanza nimeishatoa siri yangu ya nani nitampigia; na sasa unataka sababu za kumpigia kura ninayependa. Au wewe mwandishi wa habari?

Swali: Nadhani sababu za kupenda mgombea siyo siri. Kila  mmoja anasema… na hakuna siri, au vipi?

Jibu:  Mimi sina sababu kubwa. Ni kama wasemavyo “zimwi likujualo...” Kwa kuwa amekuwepo, basi naona aendelee huyohuyo. Halafu kuna maneno yanapita…mh, hayo tuyaache. Nitachagua huyo. Kwani wewe utachagua nani?

Swali: Unataka nami nitoe siri? Nitachagua mmoja wa wagombea (kicheko).

Jibu:  Sawa, lakini nimekuuliza, wewe ni mwandishi wa habari?

Swali: Napenda kuwa mwandishi wa habari. Kwani wewe unaona nafanana na mwandishi wa habari?

Jibu:  Huwa wanasema waandishi wa habari huuliza maswali mengi.

Swali: Kwani polisi hawaulizi maswali mengi?

Jibu:  Sijawahi kuhojiwa na polisi. Sijui (kicheko).

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: