Muswada huu haufai


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 06 April 2011

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

MUSWADA wa serikali wa “Sheria ya Marejeo ya Katiba” wa Mwaka 2011, haufai kuwasilishwa bungeni. Haufai kuwa sheria.

Kila tunavyousoma, kuuchambua na hata kusikia yanayosemwa na wachambuzi mahiri, tunathubutu kusema serikali ya CCM inakaribisha maafa nchini.

Ni kitu cha ajabu kuona katika zama hizi serikali iliyoko madarakani inaamini kutenda kwa staili ya kukandamiza fikra za wananchi. Mbona huko ni kuotesha udikteta?

Kwa mfano, wakati mjadala mkubwa sasa nchini ni haja ya Jamhuri kupata Katiba ya kwanza iliyotungwa na wananchi, serikali inapendekeza kuwafunga jela watakaohoji kinachokusudiwa kufanywa na tume yake ya kukusanya maoni.

Aidha, serikali inabainisha mambo ambayo haitaki yaguswe wakati wa tume hiyo kupokea maoni. Baadhi ya mambo haya ni Urais, Mahakama, Muungano, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Uchaguzi na Taasisi za Kidemokrasia, Ulinzi na Utetezi wa Haki za Binadamu.

Hivi serikali inapozuia yote haya kujadiliwa katika kile inachoita “Marejeo ya Katiba,” inataka wananchi wajadili nini kwa mustakbali wa taifa lao?

Kinachosikitisha ni kwamba yale ambayo serikali haitaki wananchi wajadili, ndiyo wananchi wanaona ni muhimu kwa maisha yao na mustakbali wa taifa lao.

Muswada wa serikali unaonyesha kuwa wahusika wakiwemo watokao Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, walijifungia chumbani, bila kushirikisha fikra za watu wengine.

Matokeo yake yamekuwa muswada unaomfunga mwananchi anayetafuta uhuru wa kauli na vitendo.

Ni maoni yetu kuwa serikali inataka kutunga Katiba badala ya kuacha wananchi kujitungia katiba yao waitakayo. Hata hiki chao walicholeta kinaonyesha hakikuwa shirikishi; ni dhaifu na hakifai.

Wito wetu ni kwamba serikali ikae pembeni na kusikiliza na kujifunza kutokana na mkondo wa kuandaa katiba ulioasisiwa na wanataaluma na asasi za kijamii.

Kwa serikali kuendeleza ubabe wa kutunga Katiba badala ya wananchi wenyewe, siyo tu inapokonya fursa na haki ya wananchi, bali inaanda mazingira hatari yasiyoweza kutulizwa kwa muwafaka wa aina yoyote ile.

Wananchi wanataka Katiba mpya. Serikali inataka marekebisho ya Katiba iliyopo. Huu ni mgongano mkubwa na wa aina yake.

Busara inataka serikali isikilize wananchi; hasa iwaache wajiandikie Katiba yao mpya na ya kwanza katika miaka 50 ya uhuru wa nchi hii. Serikali ikubali: Vitisho havijengi. Vitabomoa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: