Muswada ni udikteta mtupu, haufai


Mabere Marando's picture

Na Mabere Marando - Imechapwa 13 April 2011

Printer-friendly version
Mabere Marando

MUSWADA unaitwa Constitutional Review Act, 2011. Hilo neno review limetumika siyo kwa bahati mbaya, ni kwa makusudi. 

Kwa wanasheria, Kiswahili cha neno reviewni marejeo. Ni kurejea maamuzi fulani kwa nia ya kusahihisha makosa fulani. Katika Kamusi ya TUKI, toleo la tatu, neno “review” limegawanyika katika maeneo mawili:

Kwanza, niangalia, fikiri, tafakari, pitia upya, chunguza, kukaguliwa.

Pili, nipitia maandishi, chambua, hakiki, tafakari, angalia upya.

Kwa hiyo kwa muswada huu, nia ya serikali siyo kuwezesha wananchi kujiandikia katiba yao mpya, bali ni kuangalia katiba hii iliyopo na kuongeza viraka hapa na pale.

Kwa mujibu wa muswada huu, mchakato mzima utasimamiwa na Rais wa Jamhuri ambaye ni mwanachama na mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Ndiye atakayeunda tume ya kukusanya maoninaatakayeandaa hadidu za rejea kadri atakavyoona itafaa kwa maslahi ya chama chake.

Katibu wa tume atateuliwa na rais na taarifa ya tume itawasilishwa kwake – mwenyekiti wa CCM. Hii maana yake ni kwamba ni rais wa muungano na yule wa Zanzibar watakaopewa taarifa ya tume.

Tume inaelekezwa kufanya kazi kwa kutumia viongozi wa Kata, Mtaa, Vijiji na Shehia tu, na siyo taasisi nyingine zozote. Viongozi wote hawa, kwa hali halisi, kote Tanzania Bara na Zanzibar, ni makada wa CCM.

Viongozi wengine wote wa vyama vingine hawataona taarifa hiyo katika hali yake ya asili (original); bali kwa upande wa CCM, makada wake wote, kuanzia mwenyekiti, mawaziri, ambao ni wabunge pia, wakuu wa mikoa na wilaya, wote wanahusishwa moja kwa moja.

Ukweli ni kwamba muswada huu umetungwa kwa maudhui ya utawala wa chama kimoja na madhumuni ya chama hicho – CCM.

Kifungu cha 20 ni cha mwelekeo wa ajabu kweli. Kifungu 20 (1) kinasema ni marufuku kuhoji matendo yoyote ya Tume mahakamani. Kifungu cha 20 (3) kinasema yeyote atayekwenda mahakamani kulalamikia Tume anatenda kosa la jinai na anaweza kufungwa jela miezi 12.

Hii ni mara ya kwanza kuona kifungu cha sheria kinachoharamisha kitendo cha kwenda mahakamani. Yaani ukienda kwa wakili, akuandikie malalamiko na kuyawasilisha mahakamani dhidi ya Tume, basi kufanya hivyo tu ni kutenda kosa la jinai (!)

Aidha, muswada huu unazuia wananchi kujadili mambo makuu na muhimu. Kwa mfano, hawaruhusiwi kujadili ofisi ya rais wala Serikali yaMapinduzi ya Zanzibar. Lakini wangekuwa na maoni juu ya kuendelea kuwepo taasisi hizo kama zilivyo au kwa kufanyiwa mabadiliko.

Tume itaandaa muswada wa Katiba chini ya Kifungu cha 19. Baada ya Rais kupewa taarifa ya Tume, ikiwa pamoja na muswada wa Katiba, anayo madaraka (kifungu cha 21) kutangaza Bunge hilihili, kuwa sasa Bunge la Kutunga Katiba (Constituent Assembly).

Hivindivyo Rais Julius Nyerere alifanya wakati wa mfumo wa chama kimoja. Ndivyo Rais Jakaya Kikwete anataka kufanya sasa kwa kutumia bunge hilihili, lenye wabunge wengi wa CCM, ili kupata katiba nyingine isiyo ya wananchi.

Viroja zaidi vinakuja katika vifungu vya 22 na 23. Muswada wa Katiba utapitishwa na hiyo Constituent Assemblyna Rais ataweka saini yake kwa mujibu wa Kifungu cha 97 cha Katiba hii iliyopo.

Hii maana yake ni nini? Ni kwamba Katiba hii ya sasa inatumika tena kuhalalisha hiyo katiba nyingine.Kifungu cha 97 cha Katiba ya sasa kinasema Rais akishatia saini muswada wowote, basi muswada huo unakuwa sheria kamili.

Hili lina maana gani? Kwamba tutapata Katiba hiyo kabla wananchi kuipigia kura. Baada ya Rais kutia saini ndipo inapelekwa kwenye kura ya maoni (!).

Kwa mujibu wa sehemu ya sita ya muswada huu, vifungu vya 26 hadi 28, kura ya maoni ni ya kuhalalisha Katiba ambayo Rais atakuwa ameishatia saini na ile Constituent Assembly itakuwa imeshavunjwa kwa mujibu wa kifungu cha 25. 

Hakuna kifungu kinachosema hali itakuwaje iwapo wananchi watakataa Katibahiyo. Hii ni kwa sababu watawala wameweka mfumo unaowapa uhakika kuwa maoni ya Watanzania yatakuwa “Yes” (ndiyo) na Siyo “No” (hapana). 

Kifungu cha 28(2) kinazuia vyama vya siasa kushiriki kampeni ya kura za maoni. Maana yake ni kuwa kampeni hiyo itasimamiwa na ile ya Tume ya kukusanya maoni kwa sababu itaendelea kuwepo mpaka matokeo ya kura ya maoni yatangazwe. 

Ile Tume ya Rais ndiyo itakuwa inaitisha mikutano ya hadhara kwa ajili ya kampeni. Makatibu Kata, wenyeviti wa mitaa, vitongoji, vijiji na shehia, ndiyo watakuwa wanafanya kampeni kwamba hiyo Katiba, ambayo imekwishawekwa saini na Rais, ipite au isipite.

Kifungu cha 28(3) kinasema kwamba mtu yeyote, anayehusika kwa vyovyote, na chama cha siasa, akijihusisha kwa namna yoyote katika hiyo kampeni ya kura ya maoni, atakuwa amefanya kosa la jinai, na akipatikana na hatia, atapelekwa jela kwa miaka isiyozidi miwili. Mahakama hairuhusiwi kumtoza faini, ni kifungo tu.

Hii maana yake ni kuwa akina Dk. Willibrod Slaa, Freeman Mbowe, Prof. Ibrahim Lipumba na James Mbatia, wote watakuwa Ukonga (gerezani) ifikapo mwaka 2015, wakati wa uchaguzi mkuu ujao.

Huo ndio muswada wa Katiba wa Rais Kikwete na serikali yake. oHhhhhhhHoja ilikuwa ya Watanzania kujitungia Katiba yao mpya. Kwa mtindo huu, jitihada zote za wananchi zimechakachuliwa kabla hata hawajaanza kazi.

Huu ni ulaghai wa dhahiri. Wananchi hawatarajiwi kuukubali.Najua wengi wenu hampendi vyama vya siasa. Lakini sitegemei kuwasikia kuunga mkono muswada unaovizuia vyama vingine kushiriki katika mchakato huu, na kuachia CCM peke yake kushiriki kwa kutumia vyombo vyake.

CCM wanasema hili kwa ulimi wao, lakini kivitendo wamedhamiria kuimarisha ubabe wao katika utawala wa nchi hii. Wanataka kusema mchakato huu ni wa kupata Katiba mpya, lakini kivitendo dhamira ya kujihakikishia kutawala milele, kwa ufisadi, bila kupata upinzani wa maana. 

Mimi nasema Watanzania tusibweteke.Tutambue jambo moja, kwamba haiwezekani CCM kiweke Katiba itakayozaa fursa ya kukiondoa madarakani.

Kwa hiyo basi, Katiba mpya iliyotungwa na wananchi na yenye faida kwa Watanzania, itapatikana chini ya utawala mwingine, mpya na hakika, siyo chini ya CCM.

*Mabere Marando ni wakili wa Mahakama Kuu, mmoja wa waanzilishi wa mageuzi nchini na Chama cha NCCR-Mageuzi.Kwa sasa ni mshauri wa kisheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo – CHADEMA. Makala hii ni sehemu tu ya mchango wake kwenye mjadala wa Katiba, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, 3 Aprili 2011.

0
Your rating: None Average: 3 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: