Mutungirehi: Mrema 'chui wa karatasi'


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 14 April 2009

Printer-friendly version
Ana kwa Ana
BENEDICTO  Mutachoka Mutungirehi

BENEDICTO Mutachoka Mutungirehi (42), amesema hana taarifa za kufukuzwa Tanzania Labor Party (TLP) na kwamba amesikia kupitia vyombo vya habari.

“Sina barua. Nimeona na kusikia kwenye vyombo vya habari,” anasema. Mutungirehi alikuwa amejitosa kumng’oa Augustine Lyatonga Mrema katika wadhifa wake wa mwenyekiti katika uchaguzi ambao unatarajiwa kufanyika Aprili 26.

Tayari Mrema ametangaza kumvua uwanachama Mutungirehi kwa madai ya utovu wa nidhamu na kumpotezea sifa.

Mutungirehi amesema Mrema ana mdomo hivyo hawezi kumzuia kuzungumza chochote. “ Lakini kwa jambo zito la chama kikubwa kama TLP, huwezi kuwa na uamuzi wa upande mmoja. Kuna taratibu za kufuatwa. Huwezi kuwa mlalamikaji, wakili na hakimu kwa wakati mmoja,” amesema.

“Chama si nyumba ya mtu na wanachama wakawa wapangaji. Hata nyumba ya kupanga, unapotaka kumfukuza mpangaji kuna taratibu, huwezi tu kukurupuka. Nasema chama si chake, si mwanzilishi na wala si koti lake analotaka kuwanyang’anya watu ili aendelee kulivaa,” alisema Mutungirehi.

Mutungirehi anadai kuwa mwenyekiti wake amekuwa akifanya siasa za ulaghai kwani amewatangazia wajumbe kuwa ruzuku anayopata kutokana na ubunge wa Phares Kabuye na madiwani  ni Sh. 2.4 milioni wakati nyaraka zinaonyesha kuwa TLP inalipwa Sh. 9 milioni.

Inadaiwa ya kuwa Mrema ndiye anayeidhinisha kuchukua fedha hizo na matumizi yake yote katika uongozi wake.

Mutungirehi anasema, “Uenyekiti wa chama chetu si ufalme. Ni nafasi ya kiuongozi wa kisiasa. Hivyo hakuna mwenye hati miliki na mwenye mamlaka ya kumzuia mwingine asigombee nafasi hii.”

Mwingine aliyetangaza kuwania nafasi hiyo, ni Mkurugenzi wa uchaguzi wa TLP, Joram Kinanda. Sasa Mrema anasema amekosa sifa za kugombea.

Katika mahojiano yake na MwanaHALISI kabla ya kutangazwa kutimuliwa, Mutungurehi amesema kilichomsukuma kuwania nafasi hiyo ni sifa alizonazo, kujiamini na uwezo wake wa kuongoza.
 
 “Uongozi wa Mrema una ukomo wake. Na wajumbe wa mkutano mkuu wanayo mamlaka na wanayo haki ya kuchagua mtu mwingine kushika nafasi ya uenyekiti, iwapo wataridhika kwamba Mrema ameshindwa kazi,” anasema Mutungirehi.

“Nina sera, vision (maono), mikakati ya kuweza kufanya chama kiimarike kimuundo kwa maana ya mtandao na mfumo,” anasema Mutungirehi.

Anasema kwamba chama hicho, chini ya Mrema, kimepoteza dira na mwelekeo baada ya kutathimini chaguzi mbili kuu za kitaifa zilizopita. Chaguzi hizo ni za mwaka 2000 na 2005.

“Mrema anajidanganya kwamba anapendwa, wakati rekodi zilizoko kwenye Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) zinaonyesha kwamba amepoteza mwelekeo na mvuto wa kisiasa,” anasema.

Takwimu hizo zinaonyesha kwamba, mwaka 2000, chama hicho kilipata kura 600,000 katika wapiga kura zaidi ya milioni tano; kilivuna wabunge wa kuchaguliwa watano na kuongoza Halmashauri ya Moshi baada ya kuvuna madiwani wa kutosha mbali na wenyeviti wa serikali za mitaa na vijiji.

Mwaka 2005, katika wapiga kura milioni 12, TLP ilipata kura 86,000, mbunge mmoja, kupoteza halmashauri, kupokwa madiwani na wenyeviti wa halmashauri na vijiji.

“Sasa yeye anasema anapendwa; anapendwa vipi? Kura za ubunge Tanzania nzima zilikuwa 500,000 lakini kwa upande wake katika urais alivuna 86,000 kama ilivyo kwa madiwani. Sasa huoni kuna tatizo hapo; halafu anasema anapendwa, eeeh!” anashangaa Mutungirehi.

Mutungirehi ambaye kwa sasa ni katibu mwenezi wa TLP anasema, “Sikujitosa kupima upepo. Nimejitosa ili kushinda uchaguzi na kukiokoa TLP na tishio la kupotea kisiasa.”

Anasema Mrema tayari amekufa kisiasa; amepoteza mwelekeo na dhana anayojenga kwamba bado anapendwa “ni potofu. Na kufikia tarehe hiyo (ya uchaguzi), nafasi hiyo itakuwa wazi kwa mujibu wa katiba.

Mrema amekuwa akiwabeza wapinzani wake kwamba amewafundisha siasa na mbali ya yote, ana uwezo wa kuwatimua kama hawatofuata taratibu na sera za chama ambacho ameongoza kwa miaka 10.

Alipoulizwa juu ya kile kinachodaiwa kuwa “uswahiba wake na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),” Mutungirehi alisema, “Mimi si mwasisi wa muungano wa vyama vya upinzani. Mrema anawafahamu alioasisi nao na kuwa nao karibu.”

Hata hivyo, Mrema siyo mmoja wa waasisi wa mageuzi nchini. Alikimbilia upinzani baada ya CCM kuonyesha kuwa haitamruhusu agombee urais kupitia chama hicho na kuweka vigezo vya mgombea kuwa na digrii ambayo hakuwa nayo.

Amesema katika siasa zake, hata siku moja hakurejea Chama Cha Mapinduzi (CCM) wala kuhama kwa dhana ya kuwa kiongozi kama ilivyotokea kwa Mrema, aliyetokea NCCR-Mageuzi na kutua TLP kwa wadhifa wa mwenyekiti.

“Ndiyo maana nimetokea katika uenezi na kwenda juu na hiyo ni rekodi yangu tangu nilipokuwa mwanafunzi wa shule ya msingi,” anasema Mutungirehi akibeza kauli ya Mrema kwamba alimwokota na kumfunza siasa.

Amesema haoni hatari kuwania nafasi hiyo ya juu kwa sababu hata katika CCM, Jakaya Kikwete alikuwa waziri wa kawaida kabla ya kuwania urais. Amemfananisha Mrema na “chui wa karatasi.”

Kutokana na hali hiyo, anasema katika uchaguzi kuna wagombea na wapigakura na anachosubiri yeye ni uamuzi wa wanachama. Anasema, “Wapiga kura wa TLP wanajua ukweli.”

 Amesema wanachama wataamua siku hiyo; wameona hali ya chama ilivyokuwa huko nyuma na sasa wanajua kuangalia mbele, hivyo watakuwa na uamuzi sahihi.

“Si suala langu mimi kuamua, ndiyo maana kuna jitihada zinafanyika ili kuwazuia walio wengi wasije kwenye mkutano,” anadai Mutungurehi ambaye anaponda madai ya Mrema kwamba akienguliwa chama kitafilisika.

“Hivi ni lini amewahi kukikopesha chama; ni  chama ambacho kimempa makazi pale Sinza. Kila anachotumia ni gharama za chama,” anasisitiza Mutungirehi na kuongeza, “Mrema amepitwa na wakati.”

Historia ya Mutungirehi katika uongozi, inaanzia mwaka 1980, alipokuwa mwanafunzi wa darasa la nne. Alichaguliwa kuwa kaka mkuu katika Shule ya Msingi Kitwe, iliyoko Karagwe, Kagera.

Mwaka 1985 alichaguliwa kuwa kiranja mkuu huku akiwa kidato cha pili katika sekondari ya Kahororo, Bukoba.

Akiwa Sekondari ya Milambo, Tabora alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu kabla ya kuwa katibu wa tawi la CCM katika kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Buhemba. Amewahi kuwa Rais wa Serikali ya Wanafunzi Chuo Kikuu Dar es Salaam.

Mwaka 1997 alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika Wilaya ya Karagwe kabla ya kujitosa katika mbio za ubunge mwaka 2000 na kushinda kupitia TLP katika Jimbo la Kyerwa.  

Amekuwa katibu wa kambi ya upinzani bungeni; cheo ambacho alikuwa nacho katika chama cha Wabunge Vijana katika bunge lililopita.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: