Muungano huu lazima ujadiliwe


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 09 May 2012

Printer-friendly version

DUNIA nzima ilifuatilia kuanzia tarehe 9-15 Januari 2011 ilivyoendeshwa kura ya maoni ili kuamua kama eneo la kusini libaki kuwa sehemu ya Sudan au lijitenge.

Umoja wa Mataifa ndio uliosimamia kura hiyo ya maoni iliyoitishwa kufuatia makubaliano yaliyotiwa saini mwaka 2005 baina ya serikali yenye makao makuu jijini Khartoum na chama cha SPLA yaliyojulikana kama Makubaliano ya Naivasha.

Tarehe 7 Februari 2011, Tume ya Kuratibu Kura ya Maoni, ilichapisha matokeo ya mwisho yaliyoonyesha asilimia 98.83 ya waliopiga kura walitaka uhuru. Kwa matokeo hayo Sudan iliyokuwa moja kwa miaka mingi ilipasuliwa na kuwa nchi mbili tofauti kila moja ikiwa na mamlaka kamili.

Marais na wakuu wengi wa nchi Afrika, akiwemo Rais Jakaya Kikwete walihudhuria sherehe za uhuru wa Sudan Kusini tarehe 9 Julai 2011. Leo nchi hiyo imeomba kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Lakini Rais Kikwete aliyefurahi Sudan kupasuliwa kuwa nchi mbili, na akahudhuria sherehe za taifa jipya la Sudan Kusini, ‘ameuma meno’ akiapa muungano wa Tanganyika na Zanzibar hauwezi kujadiliwa tofauti na ulivyo sasa.

Tofauti ya Tanzania na Sudan ni nini? Kimsingi Sudan ilikuwa nchi moja, lakini tofauti za kiitikadi, mgawanyo mbaya wa mapato na utamaduni zilichangia mvutano, vita na hatimaye Sudan Kusini kupachuliwa.

Lakini Zanzibar na Tanganyika kwa asili ni nchi mbili tofauti. Zanzibar ni dola kwa vile kuna mamlaka iliyowekwa na katiba zote mbili, yaani ya muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye madaraka yasiyoweza kuingiliwa na chombo chochote kingine katika mambo yasiyokuwa ya muungano katika nchi ya Zanzibar.

Zanzibar ina vyombo vya ulinzi kama vile KMKM, mafunzo na JKU ambavyo vilianzishwa kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar.

Suala la mambo ya nje liko chini ya muungano, lakini suala la mahusiano ya kimataifa halijawahi kuingizwa katika orodha ya mambo ya muungano. Zanzibar ina uwezo kamili wa kushirikiana na mataifa na mashirika ya kimataifa katika kuwaletea maendeleo Wazanzibari.

Wazanzibari au Watanzania wanajua historia, malengo na faida za muungano uliofanyika 26 Aprili 1964, lakini sasa wanataka ujadiliwe kwa uwazi ili wasifike hatua ya Sudan, kupachuliwa baada ya vita vya muda mrefu.

Jambo lililowazi, Zanzibar hawakubaliani na muundo wa muungano. Wanaona wanabanwa, hawana uhuru, hawana haki sawa katika vyombo vya maamuzi na wanachukizwa na hatua ya Rais wa Zanzibar kutokuwa na sauti kubwa katika Serikali ya Muungano wakati nchi yao ni moja ya zile mbili zilizoungana Aprili 1964.

Tofauti na miaka iliyopita wakati sauti za kupinga aina ya muungano zilikuwa zinatolewa na wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF), sasa hata wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanalalamika. Tena waziwazi.

Katika nchi zote zilizowahi kuungana, kipindi cha kupitia upya au kurekebisha katiba huwa cha kutazama upya muungano wao. Njia hii ikizibwa kwa hila na mabavu, mapigano hutokea.

Baada ya Vita Kuu I ya Dunia mwaka 1918, mataifa mawili ya Jamhuri ya Czech na Jamhuri ya Slovakia yaliungana kuwa taifa moja kubwa la  Czechoslovakia. Kadri muda ulivyopita muungano huo ulipata nyufa.

Upepo wa demokrasia ulipovuma mwishoni mwa miaka ya 1980 ulilikumba taifa hilo. Pande mbili za taifa hilo ziliamua kukutana kujadili matatizo na mwaka 1991 zikaafikiana kutengana kwa amani zikarudi Czech na Slovakia.

Yugoslavia, chini ya Rais Josip Broz Tito miaka ya 1970, ilikuwa madhubuti na championi wa Umoja wa Nchi zisizofungamana upande wowote.

Lakini hivi karibuni haikutaka utaratibu wa kidemokrasia utumike kutoa haki kwa majimbo kujiondoa na kujitegemea. Matokeo ya ukaidi ule, vita viliibuka na Yugoslavia ikavunjika vipande vipande.

Muungano wa Tanzania unaoshikiliwa kwa mabavu na hila za kikatiba ulizivutia Senegal na Gambia mwanzoni mwa miaka ya 1980 ambazo ziliungana kwa lengo la kuimarisha usalama mipaka yao.

Katika makubaliano yaliyotiwa saini tarehe 12 Desemba 1981, nchi hizo ziliungana na kuwa Shirikisho la Senegambia 1 Februari 1982.

Miaka saba baadaye, kuta za muungano huo zilipigwa dhoruba, Gambia ambayo kijiografia imezungukwa kwa sehemu kubwa na Senegal, ikaomba kujiondoa ikawa hivyo.

Taifa jingine kubwa katika historia ya dunia hii ni Soviet lililounganisha nchi 15. Soviet ambayo ilijulikana kwa kifupi kama USSR iliimarika mwaka 1922 wakati nchi kadhaa zilipojiunga kwa masuala ya ulinzi, usalama na kiuchumi.

Baada ya Vladimir Lenin, kiongozi wake wa kwanza, kufariki dunia mwaka 1924, taifa la Kisovieti liliongozwa na Joseph Stalin katika vita ya miaka minne na kumshinda mvamizi Ujerumani kisha akaingiza katika vita baridi na Marekani.

Hata hivyo, baadhi ya nchi ambazo zilikuwa eneo la Baltic kama vile Lithuania, Latvia na Estonia, zilikuwa zikilalamika kutawaliwa na Soviet kinyume cha sheria kwa kutumia mkataba batili wa mwaka 1939.

Baada ya Soviet kukumbwa na matatizo ya kiuchumi na kisiasa, kiongozi wake, Mikhail Gorbachev, alijaribu kuinasua kwa mikakati tofauti. Mwaka 1991  ilielemewa ikaanza kuachia majimbo yaliyokuwa nchi kamili yajitawale.

Russia ikabaki kuchukua majukumu ya iliyokuwa Soviet hasa hifadhi ya hazina kubwa ya silaha za nyuklia.

Wataalamu wa masuala ya katiba wanasema kwamba muungano wa Tanzania umefuata ule wa Uingereza (United Kingdom). UK haijavunjika, lakini muungano wao ulipata msukosuko mkubwa Ireland Kaskazini ilipokumbwa na mgawanyiko wa kiitikadi.

Baadhi ya wananchi wake wenye itikadi ya utaifa zaidi, wengi wao wakiwa Wakatoliki, walitaka kujitoa UK ili wajiunge na Jamhuri ya Ireland, wakati wenye itikadi ya umoja, wengi wakiwa Waprotestanti wakitaka wabaki UK.

Mkataba ulifikiwa mwaka 1998 ukamaliza mapigano baina yao nchi ikabaki kuwa sehemu ya England lakini wakipewa haki zaidi. Nchi zote nne – England, Wales, Scotland, Ireland Kaskazini zina mamlaka yake.

Jambo la kujifunza katika mifano niliyoitaja, ni kwamba upande mmoja wa muungano unapoona kuna walakini upande wa pili unapaswa kupima hoja na kuridhia kupitiwa upya.

Muungano huu ndio uliosababisha kile kilichoitwa “kuchafuka kwa hali ya siasa Zanzibar” mwaka 1984 pale Rais wa awamu ya pili, Alhaji Aboud Jumbe, alipotaka muungano upitiwe upya ili uwe wa serikali tatu. Jumbe “alifukuzwa urais” baada ya Kamati Kuu ya CCM kushinikiza ajiuzulu.

Mwaka 1994 ikawa zamu ya Bara kuzimwa hoja ya serikali tatu pale wabunge wa kundi la G55 walipotaka irejeshwe serikali ya Tanganyika. Watawala wa Bara na SMZ wameng’ang’ania sheria hawataki ama wanaogopa muungano kujadiliwa kama kaa la moto. Wanapoziba njia hii ya kidemokrasia wanasubiri kuona dhoruba.

0789 383 979
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: