Muungano unahitaji kura ya maoni


editor's picture

Na editor - Imechapwa 29 July 2008

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

SI jambo la kujiuliza tena kama sasa ni wakati wa kuujadili Muungano wa Tanganyika na Zanzibar au la. Kuna kila dalili hatua zisipochukuliwa sasa, tunaweza kujitumbukiza katika matatizo makubwa huko mbele.

Awali suala la Muungano lilianza kama mzaha, juu ya hadhi ya Zanzibar. Watu wakitaka kujua ni nchi au la. Kauli ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ndani ya Bunge kwamba Zanzibar si nchi, ndiyo iliyozua taharuki.

Ndani ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar mambo yamekuwa ni magumu kidogo, wajumbe wamekataa hata kutii mamauzi ya Spika wa Baraza la kutokujadili hoja ya ama Zanzibar ni nchi au la. Wameendelea kuijadili hata kama alisema 'suala hili limefungwa.'

Kwa bahati mbaya, mjadala huu umechukua sura ya mvutano baina ya Tanzania Bara dhidi ya Tanzania Visiwani (Zanzibar). Jazba imekuwa juu mno, wapo wanaodiriki sasa kusema sasa wakati wa kuvunja Muungano umewadia.

Kwa vyovyote itakavyosemwa, sisi tunaamini kwamba kuna matatizo ya kimsingi katika muundo wa Muungano. Kila upande baina ya Zanzibar na Tanganyika wanadhani wanafaidika au wangefaidika zaidi.

Kuna suala la utaifa na utambulisho. Kuna suala la rasilimali za kila nchi na jinsi matunda ya pamoja ya Muungano yanavyostahili kunufaisha kila upande.

Kwa maneno mafupi kabisa, tunasema Muungano una matatizo makubwa kuliko viongozi wetu wanavyodhani. Sisi tunaamni na kuunga mkono kwa dhati kabisa kuendelea kwa Muungano wetu. Tunadhani Muungano una faida nyingi kuliko hasara na kwa hiyo kuwa nao ni kitu cha maana zaidi.

Lakini pamoja na msimamo huo, tunafikiri zile zama za kuficha na kukalia mambo sasa zimepitwa na wakati, wananchi sasa wapewe uhuru wa kuamua kama wanataka kuwa na Muungano wa namna gani.

Wapewe nafasi ya kutoa maoni yao, waeleze na kutoboa dukuduku zao juu ya aina ya muundo wa Muungano ambao wangependezwa nao.

Tunasema haya kwa sababu tabia iliyodumu kwa miaka 44 sasa ya kuona kwamba kuzungumzia Muungano ni sawa na uhaini, haitasaidia kujenga Muungano unaotokana na utashi wa Watanganyika na Wazanzibari.

Tungefarijika zaidi kama serikali sasa ingechukua maamuzi ya kijasiri kwa kuruhusu kupitisha kura ya maoni juu ya suala hili.

Tunaamini bila kufanya hivyo, Muungano wetu utakuwa ni wa kulazimisha na unaoendelea kuwepo kwa sababu unasaidiwa na nguvu za dola. Tunataka kuwa na Muungano ambao kila Mtanzania atasikia fahari kujitambulisha nao.

0
No votes yet