Muungano wa Tanzania sasa umekuwa dhaifu zaidi


Tundu Lissu's picture

Na Tundu Lissu - Imechapwa 09 February 2011

Printer-friendly version
Rais Kikwete ameficha wananchi ukweli

MUUNGANO wa Tanzania siyo tena kitu kimoja, hasa baada ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), kufanya mabadiliko katika katiba yake kwa kunyofoa baadhi ya mamlaka ya Serikali ya Muungano.

Tunaweza kusema hatua hiyo imechochea mpasuko mwingine katika Muungano.

Katika hotuba yake ya kwanza mbele ya Bunge, 18 Novemba 2010, Rais Kikwete alisema, “Pamoja na changamoto za hapa na pale zinazoukumba Muungano, bado muungano huo ni imara.”

Hata hivyo, rais hakueleza alichoita “changamoto za hapa na pale” ni nini. Badala yake, rais aliishia kutufariji kuwa, “…pande zote mbili za Muungano zina dhamira ya dhati ya kutatua kero zilizopo.”

Hapa rais hajaeleza ukweli. Hakusema kwamba Muungano ulioasisiwa na viongozi wetu wawili – Baba wa taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume – umekuwa dhaifu kuliko ulivyokuwa wakati wa uhai wa waasisi wake.

Wala rais hajasema kwa mfano, Mabadiliko ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 2010 na Sheria Na. 9 ya 2010, pamoja na kuleta neema ya kuwapo kwa mwafaka kati ya chama chake – Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF), yamemong’onyoa misingi karibu yote ya Muungano.

Sheria hiyo iliyoanza kutumika 13 Agosti 2010, haikuishia kwenye kubadili sura ya kisiasa Zanzibar kwa kubadilisha muundo wa serikali, bali imebadili sura ya Muungano wenyewe, mipaka yake na muundo wake.

Pamoja na kwamba hali ya kisiasa visiwani Zanzibar imekuwa tete tangu mwaka 1984 ulipoibuka mjadala wa mabadiliko ya katiba uliosababisha kujiuzulu kwa rais wa wakati huo, Alhaji Aboud Jumbe Mwinyi, lakini gharama ya mwafaka, inaweza kuwa chanzo kikuu cha kubomoka kwa Muungano na hata tishio kwa usalama wa mipaka ya taifa.

Hii ni kwa sababu viongozi wakuu wa Zanzibar wametumia kivuli cha maridhiano ya CCM na CUF kufanyia marekebisho katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kwa kuingiza ndani ya katiba hiyo mambo ambayo awali yalikuwa chini ya serikali ya Muungano.

Kwa mfano, wakati makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964 yalifuta nchi mbili za Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ili kuunda nchi moja, Ibara ya 3 na 4 ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba zinarudisha kuwepo kwa nchi ya Zanzibar.

Sheria hiyo inasema, “Zanzibar ni nchi ambayo eneo la mipaka yake ni eneo lote la Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na visiwa vidogo vilivyoizunguka na bahari yake ambayo kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ikiitwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.”

Vilevile, Ibara ya 4 ya sheria ya mabadiliko ya katiba inasisitiza, “Zanzibar ni miongoni mwa nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”

Rais anajua kuwa mabadiliko haya ya katiba ya Zanzibar ni makubwa na yana athari za moja kwa moja kwa uhai wa Mungano. Lakini hilo hakulisema. 

Wala hakusema pia kuwa hatua ya viongozi wa Visiwani kuingiza vifungu vya katiba vilivyoitangaza Zanzibar kuwa “nchi yenye mipaka kamili,” tofauti na mipaka ya nchi nyingine iliyokuwa ikiitwa Tanganyika, ni kinyume cha katiba ya Muungano.

Rais anajua kuwa kabla ya mabadiliko hayo kufanyika, Zanzibar haikuwa nchi na wala mipaka yake haikutajwa. Katiba ilisema, “Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”

Lakini mabadiliko hayo ambayo rais ameyanyamazia, yameifanya Zanzibar kuwa nchi yenye uhuru kamili. Kwa mfano, Ibara mpya ya 26(1) inayounda “Afisi” ya rais wa Zanzibar inamtaja rais wa Zanzibar kama “… Mkuu wa nchi ya Zanzibar…”

Wakati Ibara ya 2(2) ya Katiba inatoa mamlaka kwa rais wa Jamhuri – kwa kushauriana kwanza na rais wa Zanzibar – mamlaka ya kuigawa Tanzania Zanzibar katika mikoa, wilaya na maeneo mengineyo, Ibara mpya ya 2A ya Katiba ya Zanzibar inampa rais wa visiwa hivyo mamlaka hayohayo kwa kufuata utaratibu wa sheria iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi.

Haya yote rais anayafahamu. Lakini hakuyasema.

Hata muundo wa mahakama za juu za Jamhuri, unaathiriwa na mabadiliko haya. Mathalani, Ibara ya 117(3) ya katiba inaipa mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano mamlaka ya kusikiliza rufaa kutokana na hukumu au maamuzi ya Mahakama Kuu ya Tanzania.

Neno “Mahakama Kuu” limetafsiriwa na Ibara ya 151(1) ya katiba kumaanisha “Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano au Mahakama Kuu ya Zanzibar.”

Kwa maana hiyo, mfumo wa kimahakama wa Zanzibar umeunganishwa na mfumo wa kimahakama wa Muungano katika ngazi ya Mahakama ya Rufani ya Tanzania kwa sababu rufaa dhidi ya maamuzi ya Mahakama Kuu ya Zanzibar zimekuwa zinasikilizwa na Mahakama ya Rufani ya Jamhuri.

Lakini sasa, sheria ya Mabadiliko ya Katiba imebadili mfumo huu. Ibara mpya ya 24(3) ya katiba ya Zanzibar inasema, kutokana na maombi yanayopelekwa mahakamani kuhusu masuala ya haki za binadamu, uamuzi wa mahakama Kuu ya Zanzibar “… utakuwa ni wa mwisho na hautokatiwa rufaa kwenye Mahakama ya Rufaa ya Tanzania.”

Ibara ya 25A ya katiba ya Zanzibar imebadilishwa kwa kusema, rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu ya Zanzibar katika masuala hayo zitasikilizwa kwa mujibu wa masharti ya ibara ya 24(3).” 

Ni ibara hiyo hiyo iliyofuta haki ya rufaa katika mahakama ya Rufani ya Tanzania.

Jingine ambalo rais hakulieleza, ni kwamba sheria ya Mabadiliko ya Katiba inajaribu kuficha, suala zima la kuwapo kwa majeshi ya ulinzi.

Ibara ya 54(2) ya katiba ya Zanzibar ilikuwa inatambua uwepo wa kilichokuwa kinaitwa, “Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar” –Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM), Chuo cha Mafunzo (Magereza) na Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU).

Kifungu hicho sasa kimebadilishwa na kinaitwa, “Idara Maalum.”

Vifungu hivi vipya vya katiba ya Zanzibar vinakiuka moja kwa moja Katiba ya Muungano ya mwaka 1977.

Kwanza, vifungu hivi vinahoji muundo wa Muungano na kutishia usalama wa mipaka ya Jamhuri ya Muungano kama vilivyoainishwa na katiba.

Hii ni kwa sababu, Ibara ya 1 ya Katiba inatangaza wazi wazi kuwa “Tanzania ni nchi moja na ni Jamhuri ya Muungano.”

Ibara ya 2(1) inatamka mipaka ya nchi hii kuwa ni “… eneo lote la Tanzania Bara na eneo lote la Tanzania Zanzibar, na ni pamoja na sehemu yake ya bahari ambayo Tanzania inapakana nayo.”

Pili, mabadiliko ya katiba yanapora pia matakwa ya katiba kwa kutwaa mamlaka ya Rais wa Muungano kwa mamlaka hayo kujitwisha rais wa Zanzibar.

Katiba inampa rais wa Jamhuri mamlaka ya kugawa mikoa, wilaya na maeneo mengine katika Jamhuri kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria iliyotungwa na Bunge la Jamhuri.

Utaratibu wa kugawa mikoa na wilaya katika Jamhuri umewekwa na Sheria ya Tawala za Mikoa ya mwaka 1997. 

Lakini mabadiliko ya katiba ya Zanzibar yamemnyang’anya rais wa Muungano mamlaka hayo na kumkabidhi rais wa Zanzibar ambaye sasa anaweza kugawa mikoa na wilaya za Zanzibar kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi.

Wakati Katiba inamtaka Rais wa Muungano kushauriana na rais wa Zanzibar katika ugawaji wa mikoa na wilaya kwa upande wa Zanzibar, chini ya sheria ya sasa, rais wa Zanzibar hapaswi kushauriana na mtu yeyote anapogawa mikoa na wilaya kwa upande wa Zanzibar. 

Tatu, mabadiliko ya katiba yaliyofanywa yamekiuka katiba kwa kuinyang’anya Mahakama ya Rufani ya Tanzania mamlaka ya kusikiliza rufaa zote zinazotoka katika Mahakama Kuu ya Zanzibar.

Chini ya mfumo mpya wa kimahakama unaopendekezwa na “Sheria ya Mabadiliko ya Katiba” hakuna tena muungano wa kimahakama ambao umewekwa na Ibara ya 117(3) ya Katiba.

Nne, kwa kuhalalisha uwepo wa vikosi vya kijeshi vya SMZ vinavyoitwa “Idara Maalum,” sheria ya mabadiliko ya katiba imekiuka moja kwa moja masharti ya Ibara ya 147(2) ya katiba inayoipa serikali ya Muungano mamlaka ya “… kuunda na kuweka Tanzania majeshi ya aina mbalimbali kwa ajili ya ulinzi na usalama wa nchi na wananchi wa Tanzania.” 

Katiba inasema wazi, kwamba “ni marufuku kwa mtu yeyote au shirika lolote au kikundi chochote cha watu, isipokuwa serikali kuunda au kuweka Tanzania jeshi la aina yoyote.”

Tano, sheria ya mabadiliko ya Katiba inaingiza mfumo wa uongozi wa Zanzibar ambao hautambuliwi na katiba. Kwa mfano vyeo vya “Makamo” wa Kwanza na Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar. Vyeo hivi havitambuliwi katika katiba ya Muungano.

Hivyo basi, mabadiliko ya katiba ya Zanzibar, siyo tu yanakiuka katiba, bali pia ni batili na hayana nguvu yoyote ya kisheria.

Kufuatana na Ibara ya 64(3) ya katiba, “endapo sheria yoyote iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi inahusu jambo lolote katika Tanzania Zanzibar ambalo liko chini ya mamlaka ya Bunge, sheria hiyo itakuwa batili na itatanguka….”

Zaidi ya hayo, kwa mujibu wa Ibara ya 64(5), “… Katiba hii itakuwa na nguvu ya sheria katika Jamhuri nzima ya Muungano na endapo sheria nyingine yoyote itakiuka masharti yaliyomo katika katiba hii, katiba ndiyo itakuwa na nguvu, na sheria hiyo nyingine, kwa kiasi inachokiuka katiba, itakuwa batili.”

Kutokana na hali hiyo, hicho rais anachosema mafanikio, ni bomu linaloweza kulipuka wakati wowote. Wala hakuna mashaka kwamba marekebisho haya yakifahamika vema kwa baadhi ya wabunge, yanaweza kugeuza maridhiano yaliyofikiwa kuwa balaa, badala ya neema.

Ilikuwa ni vema mabadiliko hayo ya katiba kufuata njia sahihi za kisheria. Yangefanyika kwanza mabadiliko katika katiba ya Muungano kabla ya mabadiliko hayo kufanyika katika katiba ya Zanzibar.

Hili, kwanza lingeondoa manung’uniko, lisingetikisa Muungano na lisingeleta tafsiri mbaya, kwamba kuna watu wanapinga Muungano au maridhiano yaliyofikiwa.

Lakini hicho hakikufanyika. Hivyo basi, maridhiano yaliyofanyika hayana uhalali kisheria, na hivyo hayawezi kukidhi matakwa ya wananchi. Yanaturudisha katika migogoro mingine na mivutano isiyokuwa na sababu kati ya Bara na Zanzibar.

Haya yasingefikiwa iwapo viongozi wetu wangekuwa wa kweli na wangetenda kazi zao kwa uwazi. Lakini hapa wanaonekana walitenda yote haya kwa njia ya kuviziana.

Mwandishi wa makala hii ni  mbunge wa Singida Mashariki kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)  na wakili wa Mahakama Kuu. Amejitambulisha kuwa msomaji wa siku nyingi wa  gazeti hili. Anapatikana kwa simu: 0784 511509.
0
Your rating: None Average: 4 (2 votes)