Muungano wetu haujatengemaa


Ibrahim Hussen's picture

Na Ibrahim Hussen - Imechapwa 12 May 2010

Printer-friendly version

MUUNGANO wa Tanganyika na Zanzibar bado una utata. Maamuzi mengi yanatolewa na upande mmoja – Tanzania Bara; hali ambayo imesababisha kuwapo kwa malalamiko, shutuma na lawama.

Hii ni kwa kuwa pia uanzishaji Muungano haukushirikisha wananchi na waasisi, Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume, hawakuruhusu mjadala wa wazi juu ya muungano.

Matokeo yake hoja za msingi za kisheria na hata zile za kitamaduni, kuhusiana na muungano hazikupatiwa fursa ya kujadiliwa.

Kwa vile Muungano umefanywa na viongozi wa vyombo vya dola, mambo yote yalikuwa yakiamuliwa na viongozi, badala ya wananchi.

Haitoshi tu kusema kuwa upo udhaifu au utatanishi kwenye Muungano na mambo hayo yakifichwa na kufanywa siri ya viongozi.

Ili kupatikana ufumbuzi wa kudumu, ni vizuri kuweka wazi kila kinachoathiri na kutishia uhai wa Muungano.

Kwa mfano, wasiwasi wa Mzee Karume ulikuwa kupoteza utaifa wa Wazanzibari na hatimaye kumezwa na Tanganyika, hasa pale Watanganyika watakapomiminika visiwani bila kizuizi.

Katika hili, Karume aliweka sharti la kutumika paspoti kwa mtu yeyote atakayekuja Zanzibar. Leo, hati hii muhimu kwa ajili ya kulinda haki za Wazanzibari imeondolewa na serikali ya CCM.

Suala lingine nyeti linaloleta utatanishi linahusu fedha za kigeni, sarafu na biashara. Katika utaratibu wa sasa wa masuala haya ya Muungano, sarafu, biashara na fedha za kigeni ni jambo la Muungano.

Lakini mara kadhaa Wazanzibari wamekuwa wakilalamikia jambo hili. Wanasema suala la fedha za kigeni na sarafu si mambo ya muungano kwa kuwa hayakuwemo katika mkataba wa kwanza wa Muungano – 1964 hadi 1966.

Wazanzibari wanaitetea nchi yao huru kwa kusema kwamba mfumo mzima wa serikali ya Muungano unainyima serekali ya Zanzibar madaraka ya kusanifu uchumi wa nchi yao.

Kutokana na hoja hizo chache, kuna haja ya kujiuliza kama kweli Muungano wetu unakidhi matarajio ya wananchi na iwapo wananchi bado wanautaka.

Ikiwa kweli Muungano huu ulikusudiwa uwe wa wananchi, basi wakati umefika kuwapa fursa wananchi kuujadili kwa kina ili kuondoa kasoro zilizopo.

Wala hakuna mashaka kwamba Muungano unazidi kudhoofika kila kukicha, na moja ya sababu ya msingi ni viongozi serikalini kufumbia macho makosa ya wazi yenye shabaha ya kudhoofisha mshikamano miongoni mwa wananchi.

Wapo wanaomini kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulikuwa na matatizo tangu ulipoundwa, kilichosaidia wakati huo ni usiri uliogubika matatizo hayo.

Mara kadhaa Karume alijikuta akikwama kuamua mambo mengi kuhusu Zanzibar kutokana na ukweli kuwa chini ya mkataba wa Muungano hakuwa na mamlaka ya kikatiba ya kufanya hivyo.

Hali hiyo ilisababishwa na tukio la 22 Aprili 1964 majira ya asubuhi ya siku hiyo wakati aliyekuwa rais wa Tanganyika, Julius Nyerere alipowasili Zanzibar na waraka ambao baadaye ulikuja kuitwa “Mkataba wa Muungano.”

Waraka huo ulikuwa umeandikwa kwa lugha ya Kiingereza ambayo Nyerere alikuwa anaifahamu vizuri huku mshirika mwenzake, Karume akidaiwa kutoijua vema.

Waraka ulitiwa saini harakaharaka na bila ya kushirikisha kikao cha Baraza la Mapinduzi au kutakiwa ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa wakati huo, Wolfgang Dourado.

Kilio cha Wazanzibar kwa muda mrefu sasa, ni kubanwa kufanya baadhi ya maamuzi ambayo mkataba wa Muungano umeyatunga kwa ajili ya serikali ya Muungano.

Mfano mzuri ni Zanzibar kutaka kujiunga na Jumuiya ya Kiislamu Duniani (OIC).

Tatizo jingine ni mgawanyo usio na uwiano wa madaraka kati ya serekali ya Muungano ambayo kwao ni kama serikali ya Tanganyika na serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Ipo hofu miongoni mwa Wazanzibari kuwa kuendelea kuwepo kwa serikali mbili kutaifanya Zanzibar, ambalo ni taifa lenye historia yake, kumezwa na hatimae kutoweka.

Japo kudumu au kuvunjika kwa Muungano hakutegemei sana kama kuna ridhaa ya wananchi au la, bali muundo wake haunabudi kuangalia mifano kadhaa.

Muungano wa Kisovieti ulilindwa kwa kwa kila hali na dola kwa madai ya kuhifadhi mfumo wa Kisoshalisti wa dunia. Ulisambaratika baada ya marekebisho ya uwazi.

Je, si bora zaidi kushughulikiwa matatizo ya Muungano kwa nguvu ya makubaliano ya hiari zaidi kuliko nguvu za dola?

0
No votes yet