Muwafaka unawezekana


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 26 August 2008

Printer-friendly version

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) hakikiamini Chama cha Wananchi (CUF). Nacho CUF hakikiamini CCM. Hivyo ndivyo Rais Jakaya Kikwete alivyoliambia Bunge, Alhamisi, 21 Agosti 2008 mjini Dodoma.

Alikuwa akielezea mazungumzo kati ya vyama hivyo viwili yenye shabaha ya kuleta mwafaka mpya katika kile alichoita “kumaliza mpasuko” Zanzibar.

Alisema yeye, Rais Kikwete, ni mtu mzima; anajua kuna tatizo; anatafuta njia mwafaka ya kuhakikisha anafika anakokwenda.

Alisisitiza, “Bado sijakata tamaa. Najua lipo tatizo kubwa la kutoaminiana. Tutaangalia kama kura ya maoni au makubaliano ya vyama yanatosha.”

Mazungumzo ya kutafuta muwafaka kati ya CCM na CUF yamekwama tokea Machi mwaka huu, baada ya CCM kung’ang’ania kura ya maoni, badala ya makubaliano ya Kamati ya Mwafaka.

Katika kikao cha Halmashauri Kuu (NEC) kilichofanyika katika kitongoji cha Mwitongo, kijijini Butiama, mkoani Mara, kulikuwa na kutoleana macho kati ya wapinzani na watetezi wa muwafaka.

Baadhi ya wajumbe, hasa kutoka Zanzibar, walisema wazi kwamba hawako “tayari kuunda serikali shirikishi na CUF.”

Rais wa Zanzibar, Aman Abeid Karume ambaye ni mdau muhimu katika kufikiwa kwa mwafaka, kwa kutumia nafasi yake, alipenyeza hoja ya kura ya maoni katika taarifa ya Kamati ya Mwafaka hata kabla haijawasilishwa katika Kamati Kuu (CC).

Ni hatua hiyo iliyochafua hali ya kisiasa na kuzua mjadala mkali uliopelekea kukosekana kwa maelewano.

Karume alimwaga hadi machozi, kushawishi na kutoa tahadhari kuwa mwafaka wa kuunda serikali ya pamoja na CUF utaua maana halisi ya “mapinduzi Zanzibar.”

“Baba yangu alipigania jambo hili (Mapinduzi) na alikufa kwa kupigania jambo hili. Kwa kukubali CUF kuingia serikalini, mnataka kufuta historia,” Karume alisema.

Ilifikia hatua mmoja wa wajumbe wa mkutano huo akasema Maalim Seif Sharif Hamad, Katibu Mkuu wa CUF, ni gaidi.

Hoja ya Karume ilikuwa ni pamoja na kutaka serikali shirikishi, iwe baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 jambo ambalo CUF wamelikataa.

Je, kauli ya Kikwete inalenga wapi? Kwamba anakubaliana na hoja ya kura ya maoni au anataka kufanya maasi ndani ya CCM, hasa pale aliposema kuangalia kama makubaliano tu ya vyama yanatosha?

Inawezekana Kikwete akatofautiana na Karume ili afanikishe lengo lake? Hili ni swali gumu hata kwa wachunguzi wa masuala ya kisiasa nchini. Lakini ukichunguza kwa makini utaona kuwa ni vigumu kwa Kikwete kumtelekeza Karume.

Kwanza, urais wa Kikwete unasadikiwa kutokana na kundi la Karume, hasa kwa ufuasi Visiwani. Kwa upande mwingine, hata urais wa Karume ulitokana na nguvu ya Kikwete, wakati huo Bara wakishinikiza Karume awe chaguo la chama chake.

Kila mmoja anamhitaji mwenzake. Lakini inavyoonekana, Kikwete anamhitaji Karume zaidi kuliko upande mwingine. Hii ni kwa kuwa Karume anamaliza muda wake na hakika hana tena cha kupoteza.

Wakati Kikwete bado anataka kugombea katika uchaguzi ujao wa 2010, Karume hahitaji kupitia kwenye mnyukano huo tena labda kwa kusindikiza rafiki yake wa kisiasa.

Kutokana na hali hiyo, hata kama kura za Zanzibar haziwezi kumzuia kuwa mgombea urais kwa kipindi cha pili, kwa kuwa zitakuwa zimegawanyika, lakini bado anahitaji kuungwa mkono katika vikao vya uteuzi, hasa NEC ambako wajumbe wa Zanzibar ni karibu nusu ya wajumbe wa Bara.

Kizingiti kingine kwa Kikwete ni kwamba ndani ya CCM Zanzibar, kuna kinyang’anyiro cha urais.

Siyo siri kwamba kila mwanasiasa  anayetamani kugombea urais Zanzibar, anamhitaji Kikwete, lakini hakuna hata mmoja kati yao ambaye atakubali kuonekana yuko tayari “kukabidhi serikali kwa CUF.”

Kikwete analijua vema jambo hilo. Inawezakana anajua mahali pa kupenyea, ndiyo maana anasema, “Sijakata tamaa.”

Lakini Kikwete anafahamu kuwa ni rahisi kwa CUF kushirikiana na CCM kuliko CCM kukubali kushirikisha CUF. Hivyo ndivyo CUF imekuwa ikisisitiza.

Kutokana na hali hiyo, bado safari ya Kikwete katika hili ni ndefu. Hata hivyo, matumaini yameanza kujitokeza kwa Kikwete kuanza kuonyesha “kuhama kambi” kwa nia ya kutekeleza ahadi yake kwa taifa na dunia.

Hilo, bila shaka, ndilo lilimtuma Kikwete kuwambia wananchi kuwa viongozi wa CCM na CUF hawaaminiani. Hii ina maana kwamba Kikwete anataka wananchi wachukue hatua ya kuvirudi vyama hivyo.

Kikwete anataka CCM ijirekebishe ili kujenga imani kwa wananchi. Anataka pia  CUF wajirekebishe, kwani hata wananchi wamechoka chokochoko na malumbano ya mwaka hadi mwaka.

Hata hivyo, Kikwete hajasema iwapo CCM watakataa kumaliza mpasuko yeye atafanya nini? Je, yuko tayari kuasi chama chake? Ubavu huo kweli anao?

Hakika hoja hii haiwezi kumfanya Kikwete aasi CCM kwa kuikimbia. Lakini anaweza kuhama fikra mgando za baadhi ya viongozi na akaamua kutenda ili amalize mgogoro.

Lakini Kikwete hana sababu ya kutoelewa uwezekano na umuhimu wa kuungana katika serikali. Hili ni jambo ambalo anaweza kulieneza vema kwa Wazanzibari.

Tayari CCM na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) vimeonyesha jinsi serikali zinavyoweza kushirikiana katika uongozi. Mfano ni serikali ya Halmashauri ya wilaya ya Kigoma-Ujiji. Hii inaundwa na vyama hivi viwili.

CCM, iliyopewa ridhaa ya kuongoza nchi mzima, imekubali kushirikiana na Chadema kuongoza Halmsahauri.

Ushahidi mwingine uko katika Halmashauri za wilaya ya Karatu, na Tarime, zinaongozwa na Chadema.

Mfano mwingine ambao ni wazi hata kwa Rais Karume, ni ule wa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar. Ndani ya Baraza kuna wawakilishi kutoka vyama viwili wakifanya kazi kuu ya uwakilishi wa umma.

Inawezekana kwa Rais Karume kuteua wana-CUF kuwa miongoni mwa viongozi serikalini na bado nchi ikatawalika kama vile ambavyo inawezekana kwa Kikwete kuweka viongozi kutoka vyama vingine.

Mwaka 2002, rais mstaafu Benjamin Mkapa, alimteuwa Hamad Rashid (CUF) kuwa mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano. Hilo nalo ni funzo.

Vyovyote itakavyokuwa, hakuna ugumu katika kushirikisha wapinzani serikalini. Suala ni ukosefu wa utashi kisiasa. Kwa mfano, katika nafasi zake 10 anazopewa kikatiba, Kikwete ameshindwa kuteua hata mpinzani mmoja.

Nani atakubali kuwa Kikwete yuko tayari kuona Zanzibar inatawaliwa na serikali ya pamoja, wakati hata serikali ya halmashauri ambayo chama chake kinagawana na chama kingine inamuumisha kichwa?

Panahitajika ukomavu kisiasa – Bara na Visiwani. Kwamba mtu yumo katika chama kilichoko madarakani haina maana kwamba ndiye mwenye akili nyingi na hekima.

Kwa wanaothamini akili nje ya vyama vyao, huchota akili hizo na kuzitumia ndani ya serikali zao na kwa pamoja kutumikia wananchi wote bila ubaguzi.

Hili linawezekana Zanzibar. Linawezekana Tanzania Bara. Wakati wa mijadala mirefu umeisha. Wananchi wanasubiri matendo, na matendo hayahitaji fedha za kigeni.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: