Mv Victoria na ‘wadogo zake’


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 30 May 2012

Printer-friendly version
Ripoti Maalum

MELI ya mv Victoria ndiyo meli kongwe kuliko zote katika Ziwa Victoria. Ina umri wa miaka 52, anaeleza Kaimu Meneja Mkuu wa Marine Services Company (MSC) Projest Kaija mjini Mwanza.

Imekuwa ikifanyiwa matengenezo na ukarabati mkubwa na mdogo.

Mara ya mwisho ilifanyiwa ukarabati mkubwa (Major rehabilitation) mwaka 2008 ambako ilikaa miezi sita katika gati la Mwanza South bila kutoa huduma.

Meli hii ina uwezo wa kuchukua abiria 1,200 na tani 200 za mizigo; lakini kufuatia abiria kupungua siku hizi, inapata abiria wapatao 500 hadi 800 – chini ya uwezo wake. Inafanya safari zake kati ya Mwanza, Kemondo na Bukoba.

Kwa mujibu wa Kaija, meli nyingine za MSC zinazotoa huduma Ziwa Victoria, ni mv Butiama, Serengeti, Clarias ambazo hubeba abiria na mizigo kati ya Mwanza, Bukoba na hata Nansio, Ukerewe.

Meli za mizigo ni pamoja na mv Umoja na Nyangumi ambazo husafirisha mafuta kutoka Mwanza hadi Kisumu, Kenya na Jinja na Port Bell huko Uganda.

Meli nyingine ni mv Ukerewe, Wimbi na Malindi, ambazo husafirisha mizigo, wakati Tanganyika Sea Warrior ni boti mpya ya kusafirisha watu wapatao 15 kwa wakati mmoja.

Iwapo mv Victoria itashindwa kuendelea kubeba mizigo na wasafiri wachache waliopo sasa, wananchi watakimbilia kwenye boti na mitumbwi ambayo ina usalama haba.

(Soma hali ya usafiri katika baadhi ya meli hizo wiki ijayo).

Ushindani wa ziwa na barabara

TANGU barabara ya lami ya Mwanza hadi Musoma ikamilike mwaka 1985, hakuna tena abiria wengi wanaosafiri kwa meli kwenda Musoma, Shirati au hata Kisumu, Kenya.

Upungufu huu wa abiria wa meli ni wa takriban asilimia 50, anasema Kaimu Meneja Masoko na Biashara wa Kampuni ya Meli (MSC), Kapt. Obedi Nkongoki.

Anasema mwaka jana kampuni yake ilisafirisha jumla ya abiria 235,794 tu ambao ni chini ya uwezo wake kwa asilimia 50. Mizigo iliyosafirishwa ni tani 54,212 tu.

Akizungumzia ushindani wa kibiashara, ofisa huyo amesema, kuimarishwa kwa miundombinu ya barabara, hususan kutoka Mwanza hadi Musoma, Tarime na hata Kenya, kumesababisha abiria wengi kuacha kutumia usafiri wa meli.

0
No votes yet