Mvinyo uleule wa Anjelina, sasa ni Josephine


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 08 September 2010

Printer-friendly version
Tafakuri

WAYAHUDI wana historia inayojulikana vizuri zaidi duniani pengine kuliko mataifa mengi kwa sababu nyingi za kimsingi, kubwa kuliko yote ni kuwa chimbuko la dini. Kwa Wakristo wanajua vilivyo kwamba chimbuko la Ukristo ni Uyahudini licha ya wenyewe, Wayahudi, kuukataa Ukristo mpaka leo.

Katika historia hiyo kuna mifano mingi ya maisha yao ambayo imechukuliwa kama kielelezo cha kuasa jamii, mmojawapo ni ule wa mwanamke mzinzi aliyekuwa amezingirwa na Wayahudi waliokuwa tayari kumpatia adhabu ya kifo.

Mwanamke huyo aliyefahamika kwa jina la Maria Magdalena, alikuwa ametiwa hatiani kwa kosa la kuzini, Wakati huo Yesu alikuwako na aliwaambia “asiyekuwa na dhambi awe wa kwanza kumpiga mawe mwanamke yule.”

Baada ya kauli hiyo, hakuna Myahudi aliyebaki, wote walitawanyika kila mmoja kwa njia yake, kwa sababu walijua ndani ya nafsi zao hawakuwa wasafi kiasi cha kujipa mamlaka ya kumhukumu mwanamke aliyezini.

Ukitazama kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu zinavyoendelea, kuna picha inajengwa inayofanana sana na ya Wayahudi wa wakati huo, kwamba hoja zinaelekezwa kutafutana juu ya usafi wa maisha ya ndoa. Kwamba nani anatembea na nani imekuwa ndiyo hoja, ndiyo sera, ndiyo mkakati wa kushughulikiana kisiasa.

CCM ina historia ya kutumia siasa za namna hii. Mwaka 1995, CCM iliutumia sana mtindo huo dhidi ya aliyekuwa mgombea urais wa NCCR-Mageuzi, Augustine Mrema. Kulikuwapo na mwana mama anayeitwa Anjelina.

Mwanamama huyu alitumiwa vibaya mno na CCM kiasi kwamba alifika hatua ya kuvua nguo hadharani na kupiga kambi mbele ya nyumba ya Mrema.

Kwa waliokuwa wanamlipa, haikuwa fedheha kumwona mwanamama mzima anachojoa kila kitu na kubaki uchi wa mnayama mbele ya nyumba ya Mrema maeneo ya Masaki.

Kwa CCM lolote unaweza kufanyiwa, kama utaonekana kuwa tishio. Rejea kashfa za kuvuliwa uraia kwa makada wake, na hata vifo vya kutatanisha kama vya akina Horace Kolimba.

Kwa hali hii, suala la mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibroad Slaa na mahusiano yake na mwanamke anayitwa Josephine Mushumbusi, anayeleezwa kuwa ni mke wa mtu lakini sasa Dk. Slaa amemtangaza kuwa ni mchumba wake, haliwezi kutazamwa nje ya mkakati wa Anjelina.

Vipo vyombo vya habari vimeikamata kama ajenda kuu, kila kukicha ni Dk. Slaa na Josephine kana kwamba hakuna hoja nyngine inayoweza kuandikwa. Wameshika bango hilo kwa staili ile ile ya mwaka 1995, nia ni kutaka kumwaibisha Dk. Slaa ili kumpunguzia kura kwenye uchaguzi ifikapo Oktoba 31, mwaka huu. Huu ni mkakati!

Bila kuingia kwenye ubishi wa uhalali au uharamu wa mahusiano hayo, mtu anaweza kujiuliza swali moja muhimu, hivi katika hao viongozi wa CCM yupi ni msafi kimaadili; kuhusu mahusiano yake ya ngono; kuhusu nyumba ndogo na vimada? Yupi? Yupi hasa?

Yu wapi huyo ili awe wa kwanza kuchukua jiwe na kumrushia Dk. Slaa? Ninauliza haya kwa sababu kuna watu wamekaa na kuanzisha mkakati wa kufanya siasa za kijinga ili watu wasijadili mambo ya msingi na kufanya maamuzi sahihi ya upigaji kura ifikapo Oktoba 31, mwaka huu.

Mkakati huu si wa bahati mbaya na unalenga kumwondoa Dk. Slaa kwenye mstari wa mambo ya kimsingi kuhusu mustakabali wa taifa hili; kuhusu mwelekeo mpya wa taifa, kuhusu makubaliano mapya ya Watanzania katika kutokomeza adui namba moja wa maendeleo yetu, ufisadi.

Ni kwa kutambua ukweli huu, pengine Dk. Slaa angekuwa anafanya jambo la maana kama angeachana na hoja hizo ambazo zinasukumwa kwake ili kumuondoa kwenye mstari wa hoja za msingi ambazo wananchi kwa ujumla wake wangetaka kusikia.

Kila inapokuja suala la kimsingi kuhusu taifa hili kujiponya kutoka kwenye minyororo ya mapaka shume yanayokula bila kunawa, yanayofyonza kila tone la maziwa na asali ya nchi hii, kumekuwa na kila mbinu chafu za kuvuruga hoja hizo.

Umma unakumbuka vilivyo mbinu kama hizo zilivyotumika kupora hoja ya mapambano dhidi ya ufisadi, jinsi baadaye ilitekwa nyara na baadhi ya wabunge wa CCM waliojitangaza kwamba ni wapambanaji dhidi ya ufisadi, lakini mwisho wa siku wakaiua kifo cha mende.

Ni mbinu kama hizo pia zilitumiwa na Ofisi ya Spika wa Bunge kuvuta miguu ili suala la EPA ambalo Dk. Slaa alikuwa ameliibua life kifo cha mende hadi pale alipoamua kuiondoa hoja yake na kuipeleka kwenye mahakama ya umma.

Ndiyo maana kabla Dk. Slaa hajasema kuwa ana mpango wa kuwania urais, hoja ya kuwa na uhusiano na Josephine haikuwa jambo la kusumbua; na wala kwa miaka 15 aliyokuwa mbunge machachari si wa jimbo la Karatu tu, bali wa taifa zima, dini yake na kuwahi kuwa padri wa Kanisa Katoliki havikupata kuwa suala la kumjadili. Lakini alipoibuka sasa kukabiliana na mapaka shume, wanaofyonza maziwa ya watoto wetu, ni lazima adhibitiwe kwa kila hila!

Ukitafakari kampeni hizi chafu dhidi ya Dk. Slaa inafika mahali unashindwa kujua kwamba wote wanaendeleza uzandiki huu wanaufanya ili kumtumikia nani? Je, wanaofanya hivyo, watoto wao, ndugu zao, baba na mama zao, wajomba na mashangazi na wote wanaowahusu kinasaba wanaishi maisha gani?

Je, nao hawataki ukombozi wa taifa, hawataki kuishi maisha ya staha kwa kunufaika na raslimali za taifa kwa haki sawa? Je, kutaka mapaka shume yanaotafuna vifaranga wa kuku, wanafyonza maziwa ya watoto wetu watokomezwe, kwao hakuwahakikishii neema?

Taifa hili linaweza kuwa na neema kama watu watakataa kuwa wazandiki na kubeba mabango yanayotaka kulea na kufunika uoza, ukombozi unawezekana kwa kujenga taifa linaloheshimu sheria, utu na kukwepa wakati wote udamaduni wa kujengeka matabaka yanayowajibika tofauti mbele ya sheria.

Utamaduni wa kulinda wahalifu (culture of impunity) ndiyo umeponza mataifa mengi ya Afrika. Tujifunze walau kutokana makosa ya watu wengine. Anjelina na Josephine hawatatuondolea mapaka shume wetu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: