Mvutano wazidi kati ya Mugabe, Tsvangirai


Hilal K. Sued's picture

Na Hilal K. Sued - Imechapwa 20 October 2010

Printer-friendly version

SERIKALI shirikishi baina ya vyama vya ZANU-PF na MDC iliyoundwa nchini Zimbabwe takriban miaka miwili iliyopita iko katika mtihani mkubwa.

Wachunguzi wa mambo wanashangaza kuona kwamba hadi leo bado inadumu madarakani.

Hata hivyo, kuendelea kudumu kwa serikali hiyo imeelezwa kunatokana na ukomavu wa kisiasa wa viongozi wa chama cha Movement for Democratic Change (MDC), hususan Rais wake Morgan Tsvangirai ambaye ni waziri mkuu katika serikali hiyo.

Tofauti zimeibuka kutokana na Rais Robert Mugabe kujiamulia mambo mengi peke yake bila kumshirikisha mwenzake, na labda kumfanya kiongozi yeyote wa upinzani kujitoa na hivyo kuipeleka nchi katika hali ya wasiwasi zaidi.

Tsvangirai hajakata tamaa, licha ya kuwapo mambo mengi anayochushwa nayo kutoka kwa mshirika wake mkuu ili asizue hofu na kuingiza nchi katika mfarakano mkubwa.

Wachunguzi wa mambo wanaona kwamba kuendelea kuwamo kwa Tsvangirai katika serikali ya pamoja kunaepusha shari kubwa.

Aidha wachunguzi wa masuala ya kisiasa wanasema, kwa kiasi kikubwa, Zimbabwe imefuata nyayo za Kenya ambayo pia ina serikali ya pamoja kufuatia mapatano yaliyofikiwa baina ya vyama vikuu vya PNU na ODM.

Mapatano hayo yalifanyika baada ya ghasia zilizotokea nchini humo baada ya uchaguzi wa Desemba 2007 ambao ulisababisha zaidi ya watu 1,500 kupoteza maisha yao.

Tofauti na Zimbabwe, Kenya sasa inaonekana kupiga hatua kubwa mbele, katika urekebishaji wa mfumo wa kisiasa hasa baada ya kukubaliwa na kuanza kutumika kwa katiba mpya ya nchi hiyo.

Na kama ilivyo kwa nchi nyingi za Afrika, si rahisi kwa chama kilicho madarakani kuachia madaraka kwa njia za kidemokrasia. Chama au kiongozi aliye madarakani, akigombea tena, basi hushinda.

Tangu mifumo ya chaguzi za demokrasia ya vyama vingi iingie barani Afrika mwanzoni mwa miaka ya 1990, ni Zambia, Malawi, Burundi, Ghana na Kenya ndiko kumetokea mabadiliko ya uongozi – yaani kwa chama tawala kuondolewa kwa njia ya kura – ingawa kwa Burundi, chama kilichoshinda cha FRODEBU chini ya kiongozi wake Melchior Ndadaye kilipinduliwa na Pierre Buyoya katika mapinduzi ambayo Ndadaye aliuawa.

Vinginevyo chaguzi zinazohusisha vyama vingi huwa ni kiini macho tu kwani ama viongozi wale wale walio madarakani ndio huendelea kutawala (mfano Uganda, Cameroon, Angola, Ethiopia n.k.) – au vyama vyao ndivyo huendelea kushinda chaguzi hizo (mfano Tanzania, Msumbiji, na Afrika ya Kusini).

Zimbabwe ni mojawapo ya huo mfano wa kwanza na wiki iliyopita kitengo cha wanawake cha ZANU-PF kilitoa wito kumtaka Mugabe agombee tena urais wa nchi hiyo katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwaka ujao. Aidha wanawake hao wamesema ni vyema tu Mugabe awe rais wa maisha wa nchi hiyo.

Menyekiti wa kitengo hicho Oppah Muchinguri, katika mkutano wa mwaka alisema: “Sisi wanawake wa Zimbabwe tunakutaka ugombee tena mwaka ujao na utawale milele, kwani kazi na jitihada zako haziwezi kulinganishwa na kiongozi yeyote humu nchini. Usituache.”

Akihutubia mkutano huo wa jumuia ya wanawake wa ZANU-PF wiki iliyopita, Mugabe (mwenye umri wa miaka 86 sasa) alisema ni lazima kwa serikali shirikishi ivunjwe mnamo miezi michache ijayo na uchaguzi mpya uitishwe mapema mwaka ujao.

Wito wa Mugabe umekuja pamoja na kukwama kwa jitihada za kuleta mabadiliko muhimu ya mfumo wa kisiasa nchini humo, kitu kilichotarajiwa kuletwa na serikali ya pamoja.

Alisema: “Hatutaki Juni 2011 ipite bila ya kufanyika uchaguzi. Kuhusu hili tunataka kasi iongezwe,” alisema Mugabe.

Hakuna tarehe iliyowekwa lakini viongozi wote wawili, Mugabe na Tsvangirai wametamka kwamba wako tayari kwa uchaguzi.

Tangu kuundwa kwake, serikali ya pamoja imekuwa ikikumbwa na mivutano mikubwa hususan katika uteuzi wa watendaji wake wakuu.

Wiki iliyopita Mugabe alionekana kuikoroga serikali hiyo alipoteua mabalozi katika sehemu muhimu; Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) na Afrika ya Kusini bila ya kushauriana na Tsvangirai.

Tsvangirai naye amejibu kwa kuzitaka UN na EU kutowatambua mabalozi hao. Amesema alipaswa kushauriwa kuhusu teuzi za maafisa wote wakuu kufuatana na kilichokubaliwa katika mapatano ya uundwaji wa serikali ya pamoja kati ya vyama hivyo viwili.

Jumatano iliyopita EU ilitoa tamko la kushtushwa na hatua ya Mugabe ya kufanya uteuzi wa mabalozi kinyume cha makubaliano.

Katika taarifa yake, kupitia kwa mwanadiplomasia wake mkuu Catherine Ashton, EU ilisema: “Ni muhimu kwa mabalozi kuwa na madaraka ya kuongelea kwa niaba ya serikali yote ya Zimbabwe.” Aliongeza kwa kusema kwamba ukiukwaji wa makubaliano ni suala zito na linatakiwa ufafanuzi.

Aidha Tsvangirai aliandika barua kwa viongozi wa nchi za Italia, Sweden, Switzerland na Afrika ya Kusini kupinga kulalamikia suala hilo.

Misuguano kuhusu teuzi mbali mbali za maafisa na watendaji wakuu wa serikali imeidhoofisha sana serikali hiyo na wiki iliyopita Tsvangirai alitamka waziwazi kwamba Mugabe anakwenda kinyume cha makubaliano ya mkataba.

Katika kipindi cha takriban mwaka mmoja na nusu iliyopita, Tsvangirai amekwaruzana na Mugabe katika uteuzi wa magavana wa mikoa, majaji wapya watano, mabalozi, gavana wa Benki Kuu na mwanasheria mkuu wa serikali.

Tsvangirai aliwaambia waandishi wa habari mjini Harare Jumatano iliyopita kwamba Mugabe amekuwa akiwaahidi wakuu wa nchi za jirani na zile za SADC waliohusika katika kuleta serikali ya pamoja kwamba hatakwenda kinyume cha makubaliano, lakini kila mara yeye ndiyo mkiukwaji mkuu.

Na kwa upande wake, Mugabe anaonekana kulihusisha suala hili na uhasama uliopo kati yake na nchi za magharibi.

Wachunguzi wa mambo wanasema kwamba Mugabe anakataa kuwepo kwa maelewano kamili na mshirika wake Tsvangirai hadi hapo vikwazo dhidi yake binafsi na maswahiba wake wapatao 200, vilivyowekwa na nchi za magharibi vitakapoondolewa.

0
No votes yet