Mwacheni Dk. Slaa


editor's picture

Na editor - Imechapwa 28 April 2009

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

TANGU afichue dhambi ya mapato makubwa ya wabunge, Mbunge wa Karatu, Dk. Willibrod Slaa amekuwa akisakamwa na wabunge wenzake.

Dk. Slaa ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, ametaka mapato ya wabunge yatazamwe upya kwani hayaendani na hali halisi ya uwezo wa serikali.

Tunaona anachofanya Dk. Slaa ni kutoa kilio cha wengi. Anatoa kilio akisukumwa na uchungu na hali duni ya mishahara ya watumishi wa kada nyingine serikalini.

Inajulikana watumishi wengi wanafanya kazi ngumu zaidi ya wabunge, tena katika mazingira mabaya na kwa kutumia vitendeakazi duni mno. Bado malipo wanayopata hayatoshi kukidhi mahitaji yao ya lazima.

Kwa kutamka hayo tu, Dk. Slaa amekuwa midomoni mwa wabunge wenzake kwa kuanza kumsema hata kufikia kutajwa ndani ya bunge kuwa anapotosha mambo na anajitafutia tu umaarufu wa kisiasa kwa wananchi.

Mwenyewe anasema yeye tayari ni maarufu ndani ya chama, jimboni kwake na kwa umma wa Watanzania wanaopenda ukweli uwekwe bayana.

Hata sisi tunajua Dk. Slaa ni mwanasiasa maarufu kutokana na ukakamavu wake na staili yake ya kukosoa na kushauri serikali. Mwenendo huo ndio umempambanua na wabunge wengi wengine.

Kitu kibaya tunachokiona ni kwamba kwa kuzingatia ufichuaji wake wa dhambi ya malipo makubwa yasiyolingana na uwezo wa serikali na yasiyoonyesha uwiano na watumishi wengine wa umma, kumsakama ni mbinu ya wabunge kutaka “kufunika kombe ili mwanaharamu apite.”

Kwa kuwa hawawezi kuthubutu kusema kuwa Dk. Slaa amesema uongo, wanachojaribu kufanya ni jitihada za kumdhoofisha ili aache kuendeleza hoja ya umma mkuu.

Tunajua wabunge ni kama vile wameapa kutoweka wazi mapato yao. Yanapotajwa hadharani wanakuja juu. Lakini hawana budi kujua kuwa wanalipwa fedha za umma ambazo inabidi zijulikane matumizi yake hadi senti ya mwisho. Mapato yao yanapaswa kuwa wazi na kujadiliwa.

Wakati wenyewe wanalalamika miradi mingi ya maendeleo majimboni inakwama kutokana na kutopewa fedha, inashangaza hawaamini kuwa wao kulipwa zaidi ni dalili za matumizi mabaya ya fedha za umma.

Yapasa watambue kuwa wanapohimiza serikali iminye huku na kule ili kupata fedha nyingi za kupeleka kwenye bajeti ya maendeleo, basi pia wakubali kuwa sehemu ya mbinyo lazima iguse mapato yao makubwa.

Iwapo hawataki mtizamo huo lakini bado wanataka kila mradi wa maendeleo upewe fedha, hiyo ni sawa na kutaka kuvuna bila kupanda. Haiwezekani.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: