Mwacheni Dk. Slaa, jibuni hoja


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 08 September 2010

Printer-friendly version

TUKIWA bado tunasoma ilani za vyama vinavyogombea uongozi katika uchaguzi mkuu ujao, gazeti la serikali, Habari Leo limeendelea kuandika habari zinazohusu maisha binafsi ya mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa.

Gazeti la serikali linatutaka tuache kuangalia hoja za wagombea, ilani zao na rekodi zao za utendaji, badala yake, tuanze kuangalia nani kati ya wagombea anajua kumfinya mkewe au mmewe vizuri.

Mgombe yupi anavaa vizuri; nani anavaa soksi zilizotoboka na kati ya wagombea waliojitokeza, yupi anayeendeshwa na mkewe.

Kwa gazeti la serikali kuziba masikio na kuteketeza maadili ya uandishi wa habari, ni mfano mbaya kwa magazeti mengine na hatari kwa mustakabali wa taifa.

Tukikubali kuangalia ubora wa wagombea kwa kuongozwa na kipengele cha ubora wa ndoa, tutaumizana na bila shaka siku ya mwisho, mchokozi atalazimika kushika filimbi ili awe mwamuzi, maana mchezo hatauweza.

Hii ni kwa sababu wagombea wetu wana mambo mengi, tena si ya kale, bali yanayowaandama hata baada ya kukabidhiwa dhamana kubwa ya uongozi. Wapo ambao hata ukiwauliza wana wake wangapi watashindwa kukujibu kutokana na kupoteza kumbukumbu kunakotokana na wingi wao.

Wapo watakaokujibu kwa kukuuliza, “una maana gani unaposema wake?” Wapo ambao hawajui kama wameoa au wameolewa. Wapo ambao watakuonyesha wake zao kumbe ni watoto wao.

Wapo wanaojua kuwa walioa, lakini wamesahau ni lini na walimwoa nani? Wapo watakaokujibu kutegemea ni nani anawasikiliza wakati huo; na wapo ambao watakuambia uwasiliane na wahasibu wao, maana ndiyo wanatunza idadi yao kwa sababu ndio wanaowalipa kila mwezi.

Wapo na tunawajua hata kwa majina ambao hawaaminiwi na wake zao kukaa karibu na mabinti zao wa kuzaa! Tunawajua wanaotunza watoto wanaodai ni wa mitaani, lakini mama zao wa mitaani wanasema “ni watoto wa hao wanaowatunza.”

Hali hii si njema kuichanganya na mjadala mzito wa kumchagua rais wa nchi. Ndiyo maana, Dk. Slaa mwenyewe anayetafutwa katika mchezo huu mchafu, amejibu kwa kifupi kuwa hagombei “uaskofu wala ushehe, bali nagombea urais wa Tanzania, yenye mila na desturi zake iliyosheheni dini mbalimbali na hata wale wasiokuwa na dini.”

Kumhukumu kwa kutumia itikadi fulani kuhusu suala la ndoa, si sahihi, licha ya kwamba suala lake linaeleweka na lina vielelezo kama alivyonukuliwa katika mahojiano na vyombo mbalimbali vikiwamo vile vinavyomilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake.

Nina uhakika kabisa, baadhi ya wagombea wa urais hawawezi kujibu maswali ya maisha binafsi aliyoulizwa Dk. Slaa: Wathubutu tuone.

Kama masuala ya maadili binafsi na hali za ndoa za wanasiasa wetu ndiyo yatakayoamua kinyanganyiro hiki, basi tujiandae kwa makubwa.

Hii ni kwa sababu baadhi ya wanasiasa, wanaishi maisha ya shaka kuhusu afya zao na afya za ndoa zao.

Wengi wanaishi kwa matumaini na ni suala la muda tu kusubiri tutangaziwe misiba ya kitaifa (Mola apishe mbali!) Baadhi yao imewachukua muda kuamua kama wagombee au waache kwa sababu ya migogoro mikubwa inayozikumba afya zao.

Nina maana ya kuugua kunakohusiana na mgogoro mkubwa wa maadili binafsi ya wagombea wetu. Tunawajua waliozimia waliposikia baadhi ya watu wamekufa kwa ukimwi!

Tunawajua hata wale waliolazimika kutumia nguvu ya dola ili kuzima zahama za kimaadili zilizokuwa zinaelekea kulipuka. Tunawajua ambao hata leo hawana amani ndani ya nyumba zao kwa sababu tu, wake zao wanajua wanachokifanya.

Wanajua kuwa wanakula sahani moja na mabinti wadogo walio katika nafasi nyeti na hata wake zao wamediriki kushinikiza mabinti hao kamwe wasionekane wanachaguliwa au kuteuliwa kuwa wabunge, wakuu wa wilaya na mikoa.

Nafuu ya Dk. Slaa anayedaiwa kuchukua mke wa mtu. Je, hao wanaojulikana mbona hawasemwi?

Hakuna linalofichika chini ya mbingu, na hata hatua chafu ya kuwatoa roho baadhi ya wasichana ili kuficha yasiyofichwa yanajulikana na baadhi ya wasichana wameonana na wanasheria kuandikisha maelezo ili likitokea la kutokea wauaji hao wajulikane.

Yarabi tupe salama! Baadhi ya mambo yanayoendelea ndani ya serikali ni ya kukalia matanga. Wapo wanaochekelea kwa kufikiri kwa kuwa wapenzi (nyumba ndogo) wao wametangulia mbele ya haki, basi siri yao itabaki ufichoni. Wanajidanganya! Wamwulize Monica Lewinski na Paula Jones kule Marekani.

Miaka ilipita, lakini siku ya nyani kufa ikafika na miti yote ikateleza ikiwamo mibuyu! Viapo vilikiukwa, amri za kutosema zilibatilishwa, viapo vya migongano ya maslahi vilivunjwa, viapo vya maslahi ya uteja viliondolewa ili kuujua ukweli kwa maslahi ya taifa.

Naam, wote tunajua kwa hakika kuwa kinachotafutwa hapa ni kupunguza nguvu ya Dk. Slaa kwa nguvu yoyote ile. Kinachowaogofya si kingine bali ni rekodi yake ya kutanguliza si mke wake, mtoto wake, chama chake, rafiki zake wala ndugu zake, bali taifa lake.

Inawashangaza wengi kusikia Dk. Slaa amediriki kumpigia kampeini mgombea wa NCCR-Mageuzi mahali fulani kudhihirisha hilo. Natamani kumsikia Kikwete akimnadi mgombea asiye wa CCM ikiwa anafika mahali pa kuhoji uwezo wa mgombea wa CCM. Nyerere alifanya hivyo na tungali tunakumbuka.

Umaskini wa Watanzania haukutokana na ndoa ya Dk. Slaa. Umetokana na ufisadi wa baadhi ya na viongozi CCM na serikali yake. Ufisadi unakihusu chama chao chote, familia zao, nyumba ndogo pamoja na zile kubwa.

Ninawashauri wana CCM wenzangu – mwili wangu uko CCM, lakini roho haiko huko, wajikite katika kujibu hoja za Dk. Slaa, na kuachana na mambo ya ndani ya suruali na sketi za watu.

Maana tulio na taarifa za kina kuhusu maisha binafsi ya vigogo wa CCM tutalazimika kuingia hadharani endapo gazeti la serikali na yale yanayomilikiwa na watuhumiwa wakuu wa ufisadi, yataendelea kutuchelewesha kwa kujadili “masuala” binafsi, badala ya maendeleo.

Nasema hivi kwa sababu wahuni walewale ndio wanaofanya ujinga huuhuu ndani ya chama wakati wa michakato yetu ya ndani na kusababisha mipasuko isiyoisha.

Sasa wamejipatia ajira kwa kushinda mitaani wakiandika habari za kuchafuana na kuwachafua wanaowaita “maadui” zao kisiasa. Huu ni wakati wa kujibu hoja si vinginevyo.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: