Mwaka 2011 ulikuwa wa taabu michezoni


Elius Kambili's picture

Na Elius Kambili - Imechapwa 28 December 2011

Printer-friendly version

KILIMANJARO Stars ilifunga mwaka 2010 kwa mafanikio ya kutwaa Kombe la Chalenji hivyo ikaanza mwaka 2011 ikijivunia ushindi huo.

Taifa Stars, ikiringia ushindi wa Kilimanjaro Stars, ilialikwa kushiriki michuano ya kirafiki ya Bobde la Nile iliyofanyika Cairo, Misri. Stars iliumbuka baada ya kukung’utwa mabao 5-1 na wenyeji Misri.

Kichapo hicho kilifungua mkosi kwa Taifa na Kilimanjaro Stars. Taifa Stars ikashindwa kufuzu kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa mwaka 2012, huku Kilimanjaro Stars na Mapinduzi Stars zikishindwa kufanya vizuri kwenye Kombe la Chalenji lililochezwa kwenye Uwanja wa Taifa mwezi uliopita.

Matokeo mabaya katika michuano hiyo, kwa kiasi kikubwa yameathiri hata kiwango cha ubora wa soka ya Tanzania, vinavyotolewa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa). Kiwango hicho ni cha chini tangu alipoondoka Kocha Marcio Maximo Julai mwaka jana.

Chini ya Jan Poulsen aliyechukua mikoba ya Maximo, hakuna mafanikio yaliyopatikana mwaka huu. Taifa Stars imeruhusu vipigo na sare kwenye Uwanja wa Taifa zilizozima ndoto ya kwenda Gabon na Equatorial Guinea 2012.

Maximo aliicha Tanzania nafasi ya 108 (Juni 2010), lakini Julai iliporomoka hadi kufikia nafasi 112. Januari mwaka huu, Tanzania ilishuka hadi nafasi ya 120.

Februari 2011 iliporomoka tena hadi nafasi ya 123, Machi ilipanda kwa nafasi mbili hadi ya 121 na hata Aprili ilipanda zaidi hadi kuwa ya 112.

Hata hivyo mambo yalianza kuharibika Juni mwaka huu iliposhika nafasi ya 127 japokuwa Agosti ilipanda hadi kuwa ya 125. Tangu Septemba Tanzania imekuwa ikishuka katika viwango vya ubora hadi sasa ipo katika nafasi ya 137.

Kikubwa kilichoonekana katika kuporomoka kwa soka ya Tanzania ni namna Poulsen anavyochagua wachezaji tofauti na mfumo wa mtangulizi wake, Maximo.

Maximo hakuwa anachagua idadi kubwa ya wachezaji kutoka klabu za Simba, Yanga na Azam, badala yake alijikita zaidi katika kutafuta chipukizi ambao wangetumika kwa muda mrefu na kuwa na timu bora ya taifa. Pia alikuwa mhamasishaji mzuri kwa mashabiki na wachezaji kujivunia timu ya taifa.

Poulsen iwe yeye mwenyewe au wasaidizi wake, anapenda zaidi kuchagua wachezaji kutoka klabu kubwa huku akipuuzia soka ya vijana ambayo ni msingi wa taifa. Hapendi kuita chipukizi kikosini.

Kipimo kizuri kwa Poulsen, kama amejifunza chochote kwa miezi 12 iliyopita, ni mechi ya kirafiki dhidi ya Mafarao wa Misri, Februari mwaka ujao.

Kikubwa cha kujivunia katika mpira wa miguu ni Yanga kutwaa ubingwa wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati ‘Kombe la Kagame’, Yanga ilitwaa ubingwa huo baada ya kuifunga Simba bao 1-0 katika fainali ya michuano hiyo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Haikuwa michuano rahisi, lakini timu hizo za Tanzania zilipambana hadi mwisho na kufika fainali. Kimataifa hakuna klabu iliyotamba.

Timu ya soka ya wanawake Taifa Queens ndiyo walau ilijitutumua kimataifa ilipofuzu kucheza Kombe la Mataifa ya Afrika na Michezo ya Afrika japo hawakufanya vizuri.

Netiboli ndio walipeperusha vema bendera ya taifa pale walipofuzu kucheza Michezo ya Afrika na wakarejea na medali ya fedha baada ya kushika nafasi ya pili. Michezo hiyo ilifanyika Septemba Maputo, Msumbiji.

Michezo mingine yote, ikiwemo ya riadha na ngumi, hakukuwa na mafanikio yoyote. Hali hiyo imezidi kuwafanya mabondia kutofikia ubora wa kimataifa utakaowawezesha kupata mapambano makali chini ya mapromota wa kimataifa.

Wachezaji

Pamoja na hali isiyoridhisha ya soka kimataifa, baadhi ya wachezaji wameweza kupata nafasi za kusajiliwa na wengine kujaribiwa na hata kushiriki michezo ya kimataifa ya kihistoria.

Mrisho Ngassa wa Azam FC, 20 Julai mwaka huu, aliweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza mechi dhidi ya Manchester United ya England mbele ya mashabiki 67,052 akiwa ndani ya jezi ya Seattle Sounders ya Marekani.

Baadaye klabu hiyo ilisema ingemwita ajiunge nayo ili akacheze soka ya kulipwa, lakini kimya kimetawala hadi leo.

Wachezaji wawili Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wameweza kusajiliwa na iliyokuwa Klabu Bingwa Afrika, TP Mazembe ya DR Congo baada ya kuonyesha uwezo mzuri. Samatta alisajiliwa akitokea Simba ya Dar es Salaam wakati Ulimwengu alisajiliwa baada ya kung’ara katika kikosi cha timu taifa, Taifa Stars.

Endapo juhudi zitawekwa ni wazi Tanzania inaweza kufanya vizuri kimataifa katika soka na michezo mingine. Nawatakiwa heri ya mwaka mpya 2012.

0713 801 699
0
No votes yet