Mwaka mmoja SUK, ‘nidhamu mbovu kazini’


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 09 November 2011

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

NIDHAMU mbaya kazini – uovu na sumu kali kwa maendeleo – inashamiri katika sekta ya utumishi wa umma. Ndio kilio kikuu wakati Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) inatimiza mwaka mmoja.

Bila ya kila mtumishi kutekeleza wajibu wake kwa kuzingatia nidhamu, sheria na kanuni, wananchi hawawezi kutarajia utendaji wenye ufanisi au tija yoyote.

Iwapo utovu wa nidhamu inakuwa ndiyo kawaida kwa watumishi wanaolipwa mishahara kwa fedha za walipa kodi – wananchi pamoja na wale wafanyabiashara aina mbalimbali – maendeleo tutayaota tu badala ya kuyafaidi.

Inasikitisha mwaka mmoja tangu iingie SUK, serikali inayoundwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF), kiongozi wake mkuu, Dk. Ali Mohamed Shein, anakemea utovu wa nidhamu kazini.

Siyo tu ni jambo la kusikitisha, bali pia utovu wa nidhamu kazini ni dhambi kubwa kwa mola muumba mbingu na ardhi. Ameumba mwanadamu na kumwelekeza kutafuta riziki ya halali.

Riziki halali hupatikana kwa mwanadamu kuhangaika; na mafanikio hupatikana pale ambapo mahangaiko hayo yanasimamiwa kwa nidhamu iliyotukuka.

Lakini, rais akihutubia taifa, kupitia Baraza la Idd el Haji, mjini Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, Jumapili iliyopita, anasema kuna watovu wa nidhamu serikalini.

Anasema, “Watoa huduma za aina zote lazima waongozwe na nidhamu katika kuwahudumia watu. Tukumbuke kila binadamu anastahiki heshima. Nidhamu katika sehemu ya kazi itafanikisha lengo la serikali kuwa na utumishi bora.”

Kauli yake inamaanisha wapo watumishi wa serikali wasiozingatia misingi ya utendaji kazi nidhamu ikiwa ni mojawapo ya misingi hiyo.

Ukosevu wa nidhamu kazini una maana kuwa watumishi wanachelewa kazini, wanaondoka kabla ya muda unaotakiwa, hawatumii vizuri muda wa kazi kufanya kazi walizopangiwa na ambazo kutokana nazo ndio hulipwa mishahara.

Ina maana watumishi wanaibia serikali, wanahujumu mali za umma walizokabidhiwa ziwasaidie kufanya kazi vizuri, wananyanyasa na kudhalilisha wataka huduma.

Yote hayo ni matendo ya kifisadi. Hakuna mahali popote duniani nchi imepata maendeleo kwa watumishi wake kuwa mafundi wa ufisadi. Hakuna – si Ulaya na Marekani, wala Afrika, Asia na Australia.

Tunaposikia kuna nchi za Mashariki ya Mbali ziitwazo (Tiger economies) zimepata maendeleo makubwa na katika kipindi kifupi cha uhuru au China iliyokuwa ovyo sasa inatishia uchumi wa Marekani na Ulaya, basi ni kwa sababu watumishi wake, serikalini na katika sekta binafsi, wanafanya kazi kwa kuzingatia nidhamu.

Mtumishi anajua kazi yake, anaiheshimu, ana hamu ya kuifanya, na kwa viwango, anaamini katika utendaji adili, anazingatia sheria na kanuni. Watumishi wanatenda kwa uzalendo wa kujenga nchi zao.

Kumbe ni nani aijenge Zanzibar kama si Mzanzibari mwenyewe? Mzanzibari ndiye utapokea mgeni anayetaka kutalii vivutio vya ufukweni au msituni (misitu ya asili) kama vile Jozani ili kuona kimapunju, au Kizimbani kuona miti ya viungo vya aina kwa aina; au Kijichi na Maruhubi kuona mafulio au makao ya starehe kwa ‘watukufu.’

Ni wewe utapokea mgeni anayetaka kujenga kiwanda kisiwani Unguja au Pemba; kupokea mgeni anayetaka kufungua duka la mitambo ya kujengea barabara na madaraja; mgeni anayetaka kununua karafuu na kuziongezea thamani akiwa Unguja au Pemba; mgeni anayetaka kufungua yadi ya matrekta madogo kwa ajili ya umwagiliaji.

Ni Mzanzibari wewe unatakiwa kupokea mzawa au mgeni aloleta bidhaa mbalimbali kwenye makontena na kutaka kuzishusha katika ile Bandari Huru.

Ni wewe unapokea mgeni anayetaka kujenga hoteli ya kitalii ya nyota tano au kujenga kiwanda cha chakula kinachotumiwa kwenye ndege. Ni wewe mtumishi Mzanzibari. Ni wewe.

Kumbe kuna kusinzia kazini; watumishi wanalala; wanapiga soga; wanashona ukili na kofia kazini; wauguzi wanashughulisha vidole vyao kwa kutuma meseji za simu kwa wapenzi wakati majeruhi wa ajali ya gari au meli anafikishwa wodini.

Karani wa benki amefunga dirisha la kutolea huduma ili aende sokoni au kununua urojo; ofisa amefunga ofisi kwa sababu yuko likizo; chumba cha kulipia fedha wizarani au katika shirika la umma kimefungwa maana watumishi wote wamekwenda kuzika mwenzao.

Ofisa msimamizi wa usalama bandarini anafinya macho kwa waendesha meli ambao wamejaza abiria kuliko uwezo wa chombo; muongoza meli anaruhusu meli iondoke huku akijua imejaza kupindukia.

Haya yanaendelea kila pembe ya ofisi ya serikali. Lakini kusema kweli yanaendelea kwa sababu wakuu wenyewe wa idara na vitengo wameoza kabisa kinidhamu.

Wanafanya kazi kwa mazoea yaleyale ya utumishi katika zama za ujima. Hawajui tuko karne ya milenia – sayansi na teknolojia ndio njia. Zanzibar nayo imo humo.

Hawajui tiger economies waliamua kutenda vema na kwa kuzingatia misingi ya utawala bora, watumishi wao wakatenda hivyo, na sasa nchi hizo zinavuna matunda mengi kutokana na kutumikia kwa nidhamu.

Si wakuu tu wa idara na vitengo, hata wakuu wa mikoa na wilaya, wamepimwaje katika utumishi wao? Mawaziri na Makatibu wakuu wanapimwaje? Wakuu wa mashirika na taasisi wanapimwa vipi?

Leo, tunasikia mawaziri waliokwenda Uchina kwa ajili ya mafunzo ya utumishi wa kisasa wametanua, wakatumia wanawake wachache waliokuwa katika mafunzo kutafuta ndoa nyingine.

Ovyo, waziri mzima atamani mke wa mtu ughaibuni alikokwenda kuhudhuria mafunzo ya utumishi wa kisasa. Anajiingiza katika uhuni kwa sababu ajua akirudi hakuna anayemgomba.

Nachukulia safari ya Uchina iliyogharamiwa na Jamhuri ya Watu wa China, rafiki wakubwa wa Zanzibar, ilikuwa ni ya mafunzo sawa na semina elekezi walizopata mawaziri pamoja na viongozi wengine waandamizi serikalini.

Walifundishwa nini kama mwaka mzima baadaye Rais Dk. Shein anaendelea kupigia kelele nidhamu mbovu kazini?

Walifundishwa nini vitendo vya ufisadi dhidi ya mali ya umma vinaendelea kwa ari mpya zaidi, nguvu mpya zaidi na kasi mpya zaidi?

Walifundishwa nini iwapo wanatokea watendaji katika Shirika la Taifa la Biashara (ZSTC) wanapunguza karafuu nzuri za mkulima na kuzigeuza milki yao huku wakichanganya na za kiwango cha chini? Ni ufisadi mtupu.

Wakulima wanalalamika wanasajili kilo 250 za karafuu kavu tena za daraja la kwanza, siku wanayotaka kuuza, zikipimwa zinakutwa pungufu. Ni ufisadi mtupu.

Wanafundishwa nini kama watendaji Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar wanathubutu kuidhinisha wasichana wasio na sifa wapelekwe nchini India ambako wafadhili wanagharamia masomo ya juu ya wasichana hodari (genius) katika masomo ya sayansi watokao familia fukara?

Haya yanatokea ndani ya mwaka mmoja wa SUK na bado hakuna uchunguzi badala yake wakuu wa bodi wanatafuta nani ametoa taarifa nje ya bodi. Ufisadi mtupu.

0
No votes yet