Mwakyembe aivuruga serikali


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 22 February 2012

Printer-friendly version

UGONJWA wa Dk. Harrison Mwakyembe, mbunge wa kyela (CCM) umeivuruga serikali.

Wakati Waziri wa Afya, Dk Hadji Mponda anadai kwamba hajaona ripoti ya ugonjwa huo, taarifa zinasema Rais Jakaya Kikwete alishatoa taarifa juu ya ugonjwa wa Mwakyembe ndani ya Baraza la Mawaziri.

Chanzo cha habari hii kinasema pamoja na kukana kupata taarifa za ugonjwa wa Mwakyembe, Waziri Mponda ameelezwa kuwepo ndani ya kikao cha baraza la mawaziri ambacho Rais Kikwete alifafanulia ugonjwa wa Mwakyembe.

Kwa miezi sita sasa, Dk Mwakyembe amekumbwa na ugonjwa wa mnyauko unaopukutisha ngozi yake hadi kufanya sura yake ya awali ipotee.

Mvurugano kuhusiana na ugonjwa wa mbunge wa Kyela ulikuzwa na taarifa ya polisi wiki iliyopita, iliyokanusha kauli za baadhi ya viongozi serikalini kwamba kinachomsibu Mwakyembe kinatokana na kulishwa sumu.

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Robert Manumba aliwaambia waandishi wa habari mjini Dar es salaam wiki iliyopita kwamba polisi ina uhakika kuwa ugonjwa wa Mwakyembe hautokani na kulishwa sumu.

Kauli ya Manumba ililenga moja kwa moja kukanusha madai ya Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta kwamba ugonjwa wa Mwakyembe unatokana na kulishwa sumu; madai ambayo ameshikia bango kwa miezi mitatu sasa.

Mtoa taarifa kutoka ndani ya serikali ambaye hakutaka jina lake kuwekwa hadharani, ameliambia MwanaHALISI kwamba ripoti ya ugonjwa wa Mwakyembe iko mikononi mwa serikali na kwamba wao wameipata kutoka wizara ya afya, ambayo waziri wake anakana kuiona.

Mbunge Mwakyembe tayari amerejea India kuendelea na matibabu. Wakati anaondoka Dar es Salaam Mwakyembe alikandia polisi kwa alichoita kuingilia matibabu yake, huku ikiwa bado kuthibitishwa ni kitu gani kinamsibu.

Hivi karibuni Mwakyembe alisema tatizo lake liko katika mchuzi wa mfupa na bado halijathibitishwa kiini chake. Hivyo kuingilia kwa polisi na kudai sio sumu ni upotoshaji wa kiwango cha juu.

Mtoa taarifa amesema, “Ripoti ya ugonjwa wa Mwakyembe ipo. Serikali inayo. Wizara ya afya wanayo. Jeshi la polisi wanayo. Hilo halina ubishi.”

Amesema, “Nakuhakikishia ripoti ipo na nakwambia imewahi kufikishwa hadi kwenye kikao kimoja cha baraza la mawaziri. Katika kikao kile, Rais Kikwete alisoma ripoti yote na alifafanua kwa mapana kinachomsibu waziri wake.”

Hata hivyo, haijafahamika iwapo taarifa iliyoko mikononi mwa serikali inataja waziwazi kwamba Mwakyembe alipewa, alilishwa au alishikishwa sumu.

Kumekuwa na madai kwamba chanzo cha ugonjwa wa mbunge wa Kyela ni maji aliyonawa ofisini kwake na baadaye kujipanguza kwenye kitambaa kilichokuwa maliwatoni.

Haijafahamika pia, iwapo taarifa ambayo serikali inadai kuwa nayo imetokana na juhudi zake za kuulizia moja kwa moja kutoka kwa uongozi wa Hospitali ya Apollo, iliyopo Hyderabad nchini India ambako anatibiwa.

Wachunguzi wa mambo wanasema pamoja na kwamba hospitali hutoa taarifa kwa serikali, juu ya watumishi wake (serikali) waliokwenda kutibiwa nje, sio rahisi kuweka waziwazi chanzo cha ugonjwa wa mhusika.

“Nina wasiwasi. Kama serikali itasema kwamba imepewa taarifa na watalaam wa hospitali juu ya siri ya mgonjwa wao, ili linaweza kuharibu hadhi ya hospitali ndani ya nchi husika na kimataifa,” ameeleza mchunguzi mmoja.

Amesema uchunguzi unaoweza kuthibitisha chanzo cha ugonjwa wa aina hiyo, ni ama ule wa uandishi wa uchunguzi au ulioamriwa moja kwa moja na chombo cha haki kama mahakama, hasa baada ya kutokea utata ambao chombo hicho kinaona utahatarisha maslahi ya taifa.

Mvurugano huu umefikia hatua hii mwaka mmoja tangu Mwakyembe amwandikie barua ya kurasa saba, Inspekta Jenerali wa Polisi nchini, Said Mwema kulalamikia tishio la kuondoa maisha yake.

Katika barua hiyo, Mwakyembe alisema tukio analolalamikia ni sehemu ya mlolongo wa matukio ambayo alikwishayalalamikia kwa jeshi hilo.

Aliwataja walengwa wa tishio lama lake kuwa ni pamoja na kiongozi mkuu wa upinzani nchini, Dk. Willibrod Slaa, Mfanyabiashara Reginald Mengi, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Mark Mwandosya na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kabla ya kuondoka kwenda India wiki iliyopita, Mwakyembe alimshtumu Manumba kwa alichoita kupotosha ripoti ya ugonjwa wake.

Alisema, “Napata taabu kuamini kama DCI Manumba na wenzake waliisoma taarifa halisi ya matibabu yangu au walisoma taarifa nyingine…kama waliisoma taarifa hiyo wenyewe au walisomewa.”

Alisema, “Nasema hivyo kwa kuwa alichokisema DCI Manumba kwa waandishi wa habari, hakifanani kabisa na picha iliyoko kwenye taarifa halisi ya Hospitali ya Apollo, inayotamka wazi kuwa kuna kitu kwenye bone marrow kinachochochea hali niliyonayo, kitu ambacho mabingwa wanahangaika kukijua, kukidhibiti au kukiondoa...”

Akijadili uwezekano wa sumu, Mwakyembe alisema, “siyo lazima unyweshwe ili ikudhuru, inaweza kudhuru hata kwa kugusishwa tu.”

Mwishoni mwa mwezi uliyopita, Mwakyembe alinukuliwa akisema kuwa waliomsababishia hali aliyomo, “Wameshindwa. Watashindwa na watalegea kwa jina la bwana – Amin.”

Alikuwa kwenye mahubili katika Kanisa la Ufufuo na Uzima la Kawe jiji Dar es Salaam.

Mahubili hayo yalikuwa maalum kwa ajili ya  kumuombea Dk. Mwakyembe kupitia kile kilichoitwa, “Neno la Hekima kutoka kwa kiongozi.”

MwanaHALISI lilipomuuliza Sitta juu ya uthibitisho wa madai yake kwamba Dk. Mwakyembe alisema, “Ushahidi nilionao ni wa kimazingira. Ripoti yenyewe aulizwe Waziri wa Afya na Dk Mwakyembe mwenyewe.”

0
Your rating: None Average: 3.5 (2 votes)
Soma zaidi kuhusu: