Mwakyembe ametusononesha


Isango Josephat Ng’imba's picture

Na Isango Josephat... - Imechapwa 21 January 2009

Printer-friendly version
Dk. Harrison Mwakyembe

HUYU ndiye Dk. Harrison Mwakyembe au vyombo vya habari vimetudanganya? Soma kauli aliyonukuliwa akitoa na kukaririwa na gazeti la Mwananchi toleo la 14 Januari 2009:

"Ukitaka kufanya mambo yako vizuri, na unataka usikilizwe, uishi maisha marefu, bora ubaki CCM kuliko ukawa kwenye upinzani na kupayuka mambo bila ya ushahidi wa kutosha.”

Tumesoma kuwa Mwakyembe alitoa kauli hiyo kwenye mkutano na wananchi wa jimbo lake uliofanyika viwanja vya Siasa, mjini Kyela ambako baadhi ya wananchi walimtaka kuhama CCM ili afanye kazi ya kufichua mafisadi kupitia kambi ya upinzani.

Akijibu hoja za wananchi hao, Dk. Mwakyembe alitumia maneno niliyonukuu hapo juu ambayo ndio chanzo cha hofu yetu kuhusu “mpiganaji huyu.” Kauli hii inalenga kutuambia nini?

Hii ina maana hakuna usawa? Kwamba katika CCM utasikilizwa lakini katika upinzani utapuuzwa? Kumbe madai ya upinzani kuwa utawala huu hauna usawa ni sahihi?

Kwamba “maisha marefu” yanapatikana CCM peke yake? Kwamba walioko upinzani maisha yao mafupi kwa kuwa hawaungi mkono CCM? Hii ni kwa kuwa ni masikini, hawana chakula au ni maadui na hivyo watauawa na CCM?

Nadhani Mwakyembe alisema haya bila kujua kutakuwa na mwandishi wa habari kunukuu kauli yake. Vinginevyo anajua uwezo mkubwa wa wabunge wa upinzani na umma mkuu ulioko nje ya bunge na nje ya vyama.

Mikataba ya ovyo kama ule wa Buzwagi; kashfa ya Richmond iliyomwangusha Edward Lowassa katika uwaziri mkuu; wizi mkubwa Benki Kuu na mengine, yameibuliwa na wabunge hawa. Kwanza yalibezwa, baadaye yakakumbatiwa; CCM ikayadandia kutafuta umaarufu.

Mwakyembe anataka kusema nini kwa wananchi wa jimbo la Kyela wasiokuwa CCM? Je, yeye alichaguliwa na wana-CCM peke yao? Je, maadili ya kujua mema na mabaya yanatofautishwa kwa kutumia misingi ya uanachama wa vyama vya siasa?

Kama ni lazima kuwa CCM au kubaki humo ili ufanikiwe, ina maana wasio wanachama wa chama hicho ni watu wa kulaaniwa? Mwakyembe anatufundisha nini sisi tuliomwona mzalendo, aliyesimama bila kutetereka kutetea maslahi ya nchi katika sakata la Richmond?

Kama alivyonukuliwa ndivyo alivyo; kwa maana kwamba amekuwa akificha sura yake halisi, na kwamba anaona kuwa maisha nje ya CCM hayawezekani, basi amejipunguzia sana heshima tuliyowahi kumpa.

Ina maana uchungu wa mwana-CCM kwa nchi hii unatofautina na uchungu wa mwana wa chama kingine? Kwamba tatizo la mwana-CCM ni tatizo zaidi kuliko tatizo la raia mfuasi wa chama kingine? Tunawaweka wapi wale wasio wafuasi wa chama chochote?

Nakaribia kushawishika kwa kauli ya rafiki yangu kuwa raia wa Tanzania si “Watanzania” maana “Watanzania” wana maisha bora kama kauli mbiu ya “maisha bora” inavyosawiri kwao. Sisi tusio na maisha bora si Watanzania.

Nisingejisikia vibaya iwapo Mwakyembe angesema atafanyia kazi ilani ya CCM na kwamba hana mpango wa kuhama chama chake, kuliko kutoa kauli zinazolingana na vitisho.

Nimesadikishwa kuwa kwa mwanafalsafa hakuna tamko la bahati mbaya. Nami naona Mwakyembe alikusudia kusema hayo na ameyasema. Kwa kuwa kila kauli ina gharama, basi kauli ya Mwakyembe imemgharimu heshima.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: