Mwakyembe: Nitafyatuka


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 25 March 2009

Printer-friendly version
Lissu: Dharura ni kichaka cha ufisadi
Dk. Harisson Mwakyembe

MBUNGE wa Kyela (CCM), Dk. Harisson Mwakyembe amembwatukia mfanyabiashara Rostam Aziz na kumwonya kuwa “kuna siku tutafyatuka…tusiheshimiane kabisa.”

Mwakyembe alikuwa akijibu tuhuma zilizotolewa kupitia gazeti la Mtanzania linalomilikiwa na Rostam kwamba hajawahi kutangaza kuwa na maslahi katika tasnia ya nishati na kwamba ana mgogoro wa kimaslahi.

Aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Jumatano iliyopita, kwenye hoteli ya Durban, kuwa hana cha kutangaza na kwamba hana mgogoro wa kimaslahi.

Mwakyembe alisema ni kweli yeye ni mmoja wa waanzilishi wa kampuni ya Power Pull East Africa Limited ya kufua umeme unaotokana na upepo, lakini akasema kampuni bado ni mradi tu; haijaanza kazi na kwamba “haina hata koleo.”

Alifafanua kuwa kama kampuni haijaanza kuzalisha na haijapata hata vifaa, ina maana hakuna mapato na maslahi kifedha. Akasema ni upumbavu kusema una mgongano wa maslahi wakati huna maslahi.

Mwakyembe alidaiwa na gazeti la Rostam kuwa na maslahi katika tasnia ya umeme; kushindwa kutangaza maslahi yake; na kwamba ndiyo maana alikuwa anapinga kampuni ya Richmond na kununuliwa kwa mitambo ya Dowans.

Kwa sauti ya ukali, mbunge huyo aliwaambia waandishi, “Dowans hatuna mkataba nao. Dowans wametushitaki Mahakama ya Usuluhishi Ufaransa. Dowans mitambo yao ni chakavu, na ni kinyume cha sheria kununua mitambo chakavu.”
 
Alisema suala la Dowans liliisha zamani ndani ya Bunge lakini wanaotaka kulifufua wanaweza kulipeleka bungeni. “Dowans italetwa (bungeni), tutaikataa…wengine wanafikiri ni Mwakyembe peke yangu…sheria ipo.”

Mwakyembe alisema kinachogomba siyo Mwakyembe kuwa na kampuni wala maslahi, bali ni kuona waswahili wanaingia katika eneo ambalo lilidhaniwa kuwa la “akina Rostam” peke yao (Soma mahojiano uk. 7).

Naye Mkurugenzi wa Sheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambaye pia ni wakili wa Mahakama Kuu, Tundu Lissu amesema suala la Dowans liliisha zamani.

Ameliambia MwanaHALISI kuwa kilichohitajika ni kutaifisha mitambo yake kwa kuwa iliingizwa nchini kwa njia ya rushwa na kwa kuvunja sheria.

Amesema serikali inaweza kutumia sheria zilizopo kuchukua mitambo hiyo na kwamba kama wawekezaji wataamua kwenda mahakamani watashindwa kwa sababu “uwekezaji uliingia kwa rushwa.”

“Ni ujinga. Ni upuuzi mtupu kununua mitambo hii,” alisema Lissu. Alisema watu wanafanya mjadala uliofungwa tangu mwaka jana na wanaacha mambo ya msingi. “Nadhani chama changu kinapaswa kulitolea tamko jambo hili.”

“Mjadala unawapa mtaji watu waliofilisika. Tunamrudishia Lowassa taulo? Kama Dowans ni safi, basi Lowassa arudishiwe uwaziri wake na wote waliojiuzulu warudishwe serikalini,” amesema Lissu.

Kuhusu mipango ya dharura ya kudumu ya kuzalisha umeme, Lissu amesema kunapaswa kuwa na mipango ya muda mfupi, wa kati na mrefu na kwamba nchi haiwezi kuendeshwa kwa misngi ya “dharura dharura. Dharura ni kichaka cha ufisadi,” alisema.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: