Mwakyembe na wapambanaji wenzake wangefanyaje


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 08 December 2010

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

KUNA mjadala umeibuka katika siku za karibuni tangu Rais Jakaya Kikwete alipowateua Samwel Sitta na Dk. Harrison Mwakyembe kwenye baraza la mawaziri.

Wapo wanaoamini kuwa wanasiasa hao wamefanya makosa kukubali uteuzi huo. Na inaonekana ni kundi kubwa tu linaloamini hivyo.

Kwa watu wa kundi hili, kukubali kwa Mwakyembe na Sitta kujiunga na serikali ya Kikwete ni usaliti dhidi ya wale waliowaamini ni wapambanaji wa ufisadi.

Kwamba ili kupambana na serikali ya Kikwete, kina Mwakyembe wangefanya vizuri tu iwapo wangebaki wabunge tu ili waichachafye serikali.

Wapo wengine, lakini katika kundi hilihili, wanaoamini kina Mwakyembe ni wasafi kuliko serikali ya Kikwete na hawastahili kufanya nao kazi kwani watachafuka.

Kabla sijaendelea kuchambua hoja hizi, mifano miwili inaweza kujenga msingi wa hoja yangu ya leo.

Nchini China, hasahasa katika miaka ya 1950 na 1960, Mwenyekiti Mao dze Dung alikuwa na tofauti kubwa ya kiitikadi na Deng Xiao Ping.

Mao aliamini katika ujamaa wa kikomunisti wakati Deng aliamini ubepari wa kijamaa. Mao alipoona inafaa, alimwingiza Deng serikalini na walipokorofishana, alimtosa.

Pamoja na tofauti zao kubwa, Mao na Deng walikuwa ndani ya chama kimoja na wakati mwingine ndani ya serikali moja.

Leo hii, China ni nchi yenye nguvu duniani kwa sababu, kwa kiasi kikubwa, ya mchango wa Deng. Hata hivyo, pamoja na tofauti zao za kimsingi, walikubali kufanya kazi pamoja.

Hali iko hivyohivyo kwa jirani zetu wa Kenya. Raila Odinga amehama vyama na kufanya kazi na wanasiasa tofauti.

Sasa yupo pamoja na Mwai Kibaki katika serikali. Wana historia na itikadi tofauti. Hata hivyo, leo wanafanya kazi katika serikali ya pamoja.

Ikumbukwe pia kwamba Odinga amewahi kufanya kazi na Daniel Arap Moi, rais mstaafu aliyekuwa kiongozi wa Chama cha KANU. Moi aliwahi kumfunga Odinga na kuisababishia familia yake mateso makubwa.

Upo mfano mzuri Tanzania. Seif Shariff Hamad alifukuzwa CCM na wenzake. Mfumo wa vyama vingi ulipoanzishwa, wakasajili chama chao – Chama cha Wananchi (CUF).

Mwaka 1988 alitungiwa kesi ya jinai na kufungwa jela hadi alipotolewa kwa shinikizo. Tangu hapo, Maalim Seif amekuwa adui mkubwa kwa CCM hususan upande wa Zanzibar.

Lakini leo, ni Makamu wa Kwanza wa Rais anayemsaidia kazi Dk. Ali Mohamed Shein ambaye anaongoza Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar.

Sijaona, ndani au nje ya CCM, mwanasiasa wa sasa ambaye anaweza kudai yeye binafsi au familia yake wamewahi kuteswa na Kikwete au na CCM kwa kiwango kile ambacho Deng, Raila na Maalim Seif waliteswa.

Iweje leo ionekane nongwa kwa Dk. John Magufuli, Mwakyembe, Sitta au Profesa Mark Mwandosya ambao wote ni wana wa CCM kukubali kufanya kazi na serikali ya Kikwete.

Ninaamini kazi yao kubwa ni kukitumikia chama chao katika nafasi yoyote ile watakayopewa.

Kikwete ni mwenyekiti wa chama wanachokiamini kina Mwakyembe. Ameona miongoni mwa wanachama, Mwakyembe anaweza kumsaidia akimteua serikalini. Na aliyeteuliwa amekubali kufanya kazi hiyo. Liko wapi tatizo?

Si mara ya kwanza kwa Kikwete kumteua Mwakyembe kuitumikia nchi. Aliwahi kumteua kwenye Kamati ya Madini aliyoiongoza Jaji Mark Bomani.

Ni chama hichohicho cha Kikwete kilichomteua Sitta kuwa mgombea uspika. Tatizo liko wapi wakati mwenyekiti wa chama hicho anapompa Sitta au Mwakyembe uwaziri?

Hivi, Mwakyembe na Sitta wameiendesha serikali ya Tanzania kwa kiwango kilekile ambacho Raila aliiendesha serikali ya Kenya, Maalim Seif alivyoiendesha serikali ya mapinduzi Zanzibar au Deng alivyomwendesha Mao na baadaye wale waliokuja kuitwa The Gang of Four?

Kama Raila na Maalim Seif hatimaye leo wanafanya kazi na vyama vilivyowahilikisha, vyereje kina Mwakyembe ambao hawajawahi kuwa na mgogoro binafsi na Kikwete au serikali yake?

Kuna haja ya kundi linalowapinga kina Mwakyembe kubadili mtazamo wao kuhusu nini hasa maana ya upinzani. Hakuna upinzani wa kudumu.

Niccolo Machiavelli, alilisema hili vizuri katika kitabu chake cha The Prince pale alipoandika; “The End Justify the Means.” Kwamba matokeo ya mwisho yanahalalisha njia iliyotumika.

Hatuwezi kuwazuia au kuwawekea nongwa kina Mwakyembe kwa sababu wamekubali kuitumikia serikali. Nani ajuaye kwamba pengine watakapoingia ‘jikoni’ watawafaidisha zaidi Watanzania kuliko kama wangeendelea kubaki bungeni kulalamika?

Je, si ingekuwa vema zaidi iwapo serikalini nchi ingekuwa na watu wenye uwezo wa kuyabaini matatizo mapema kabla ya kuundiwa tume au wabunge kulalamika bungeni.

Kwa lugha nyingine, nchi itahitaji watu wa aina ya Mwakyembe bungeni iwapo watu wa aina hiyo hawatakuwapo serikalini.

Huwa ninashangazwa na watu waliokuwa wakiwaona kina Mwakyembe kama watu wasio watiifu kwa CCM kwa sababu ya misimamo yao tofauti bungeni.

Wakati Sitta alipomfukuza Zitto Kabwe bungeni mara baada ya kuibuka kwa kashfa ya mgodi wa Buzwagi, ni mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Stella Manyanya pekee aliyeinuka kumtetea Zitto.

Hakunyanyuka Sitta, Mwakyembe wala Magufuli kumtetea. Kwao, huo ulikuwa ni uamuzi uliokuwa na maslahi kwa chama chao na si vinginevyo.

Magufuli alipozungumza wakati wa kampeni na kusema Kikwete ndiye bwana harusi na waliobaki ni wasindikizaji tu, hakuna aliyedhani mwanasiasa huyo amepotoka.

Lakini huyo aliyemsifia Kikwete anapochaguliwa kwenye baraza la mawaziri tunataraji vipi akatae? Ninashangaa wanaopinga.

Halafu kuna suala zima la maslahi. Wanasiasa wote walioteuliwa kwenye baraza la mawaziri wanachukuliwa kuwa ‘wameukata’. Wataishi vizuri kuliko asilimia 80 ya Watanzania wote.

Wataendesha au kuendeshwa kwenye magari ya kifahari. Watapata posho na mishahara mizuri. Na watapata fursa ya kuzunguka ndani na nje ya nchi kikazi na wakati mwingine kutalii tu.

Miaka miwili iliyopita, alikuwepo waziri aliyefanya ziara ya kujifunza iliyofadhiliwa na taasisi ya umma katika nchi za Trinidad and Tobaggo na Barbados.

Hizi ni nchi zinazofahamika zaidi kwa matanuzi kuliko watu kujifunza vitu. Lakini, utapata wapi fursa hizi bila ya kuwa waziri au mwanasiasa wa kaliba ya juu?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: