Mwalimu anadhalilishwa, atafundishaje?


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 09 February 2011

Printer-friendly version

KUNA dhana iliyojengeka miongoni mwa wanasiasa na wenye pesa kuwa ualimu ni sawa na uyaya na kwamba mwalimu ni kama mtoto mkubwa anayeshinda kutwa nzima na wadogo zake.

Hiyo ndiyo sababu mwaka 2009 aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Bukoba Vijijini, Albert Mnali aliwadhalilisha walimu kwa kuwachapa viboko.

Baada ya kuitisha kikao cha tathmini juu ya matokeo mabovu ya mitihani ya darasa la saba mwaka 2008, Mnali ambaye alidhani alikuwa na mamlaka ya ‘kuumba’ walimu bora katika wilaya yake aliamuru mgambo na askari alioambatana nao kuwacharaza viboko walimu wapatao 32.

Hilo ni moja ya matukio ya walimu kudhalilishwa kwa namna moja au nyingine. Katika baadhi ya maeneo hata wenyeviti wa vijiji wamethubutu kuamuru sungusungu kuwachapa viboko walimu mbele ya hadhara.

Si hivyo tu, katika baadhi ya maeneo, wazazi huweza ‘kuwakata’ makofi walimu kwa kosa la kuwaadhibu watoto wao wapenzi. Wakishafanya hivyo huamua kuwahamishia watoto wao kwenye shule za msingi za binafsi.

Maofisa elimu ni wadhalilishaji wakubwa wa walimu. Hujiona miungu watu. Humpa ukuu wa shule mwalimu fulani Januari, matokeo yakiwa mabovu, Januari ya mwaka unaofuata humpokonya au mwalimu akikataa ‘ngono’ humhamishia kijijini.

Katika vikao vya tathmini vinavyofanyika miezi ya kwanza kila mwaka maofisa elimu huwatisha wakuu wa shule kwamba watawakomoa.

Vikao hivyo vinavyoandaliwa na wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri ili kujua kwa nini ufaulu umeshuka, wahudhuriaji huwa maofisa elimu, maofisa elimu taaluma, walimu wakuu wa shule, walimu wa taaluma, wazazi na wadau wa elimu.

Katika baadhi ya halmashauri vikao huwa na mijadala mikali huku wakurugenzi au maofisa elimu na maofisa taaluma wakipinga kubebeshwa lawama kwa kuhusika kwao katika matokeo mabaya.

MMEM

Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (Mmem), umemwacha mwalimu akidhalilika.

Mmem, ulioanzishwa kwa lengo la kuboresha elimu ya shule za msingi, ulilenga ongezeko la shule, vyumba vya madarasa na wanafunzi si mwalimu.

Baadhi ya shule, majengo yalitenganishwa ili kupata shule mbili na zikapewa majina tofauti, bado zote mbili zikawa zinachukua wanafunzi wa asubuhi na mchana.

Walimu walilazimishwa ‘kufanyafanya’ maarifa kumudu ongezeko hilo. Serikali ikabadili mbinu za ufundishaji, ikaandaa semina kwa walimu, lakini walioambulia ni wachache tu.

Katika kipindi hicho hicho cha Mmem, wakaunganisha masomo ili walimu hao wachache wamudu kufundisha na hata walimu tarajali walifundishwa kwa mfumo huo yaani kwa kuzingatia masomo yaliyounganishwa.

Mwaka 2006 serikali iliporudisha utaratibu wa zamani, uliathiri siyo mitaala tu, bali hata walimu kwani wale waliojifunza somo la Maarifa walitakiwa kufundisha ama Historia pekee au Jografia pekee au Uraia pekee.

Matatizo

Matatizo makuu kwa walimu na yanayochangia ufanisi mdogo, baadhi yao kufundisha chini ya kiwango, kuacha kazi, na kukosa ari ni mishahara midogo, ukosefu wa vifaa vya kufundishia na nyumba.

Walimu wengi hukaa kwenye nyumba zisizo na hadhi na zinazowapa mazingira magumu kuandaa masomo. Kuanzia mwaka 2006, serikali imekuwa ikiahidi kujenga nyumba za walimu nchi nzima, lakini hakuna lolote.

Mgomo baridi. Oktoba 2008, walimu wote waliitikia wito wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) kugoma ili kushinikiza walipwe malimbikizo ya stahili zao. Baadhi ya walimu walikuwa wanadai posho za safari, nauli, matibabu, kujikimu, uhamisho kutoka kituo kimoja hadi kingine.

Serikali ilijaribu kuhujumu mgomo ule lakini ulifanyika kwa mafanikio. Serikali ililazimika kufanyia kazi madai yao kwa kulipa taratibu.

Baadhi ya walimu waliopunjwa malipo yao na ukweli kwamba mishahara yao ni duni wamedai ari yao ya kazi imeshuka hali ambayo wanaamini itachangia matokeo mabaya ya mtihani wa Septemba mwaka huu.

Vitabu

Mabadiliko ya mara kwa mara ya mitaala yameathiri siyo tu ufundishaji bali hata vitabu vya kufundishia na vitendea kazi.

Mwaka 1991 serikali ilianzisha Mradi wa Vitabu vya Watoto na huo ukawa mwanzo wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kujitoa katika utunzi wa vitabu vya kiada na ziada, ikabaki na jukumu la usimamizi na ukuzaji mitaala.

Lakini mwaka 2008 serikali ikafuta mfumo wa vitabu vingi na kurejesha kazi ya utunzi na usambazaji kwa TET.

Baada ya uamuzi huo, wataalam wa vitabu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) waliandaa semina ya siku kadhaa mjini Kibaha, Pwani juu ya utunzi bora wa vitabu vya kiada kwa TET.

Wakala, wakanywa, wakalamba posho. Lakini wakuu wa shule za msingi wanalalamika vitabu vilivyopendekezwa na serikalihavijafika na wanahofia matokeo yanaweza kuwa sawa na ya kidato cha IV yaliyozua mtafaruku nchini.

Mwaka 2008 lilitolewa tamko jingine ambalo walimu wanahofu linaweza kusababisha matokeo mabaya katika mtihani wa darasa la saba Septemba mwaka huu.

Tamko hilo ni lile lililofuta mtihani wa mchujo kwa wanafunzi wa darasa la IV na kidato cha pili. Wakati unatolewa uamuzi wa kufuta mtihani wa darasa la IV, wanafunzi walioko darasa la saba sasa walikuwa darasa la IV, hivyo hawakufanya mtihani wa mchujo.

Walimu wa shule za msingi kutoka Dodoma, Iringa, Mbeya, Kigoma, Arusha wanasema hawatarajii matokeo mazuri katika mtihani utakaofanywa Septemba mwaka huu.

“Mwandishi utakumbuka kwamba mheshimiwa alifuta mtihani wa darasa la IV mwaka 2008. Hebu hesabu vijana waliokuwa darasa la IV mwaka huu wako la ngapi. Ndio hawa darasa la saba! Tusubiri matokeo yake,” alisema mkuu mmoja wa shule ya msingi mjini Iringa.

Kuhusu kitabu kimoja walimu wanasema mpaka leo hakuna vitabu vya masomo matatu ya Uraia, Historia na Jografia.

“Tunachofanya hapa shuleni, tunaangalia mada gani inatakiwa kufundishwa halafu tunatumia vitabu vya darasa la nne, la tano na sita na wakati mwingine vitabu vya ziada. Darasa la saba hakuna vitabu,” anasema mwalimu mkuu wa shule moja mkoani Arusha.

Madhara

Kuanzia mwaka 1991, vitabu vilivyotumika ni vile vilivyotungwa na watu binafsi lakini vilivyoainishwa na TET na kupewa ithibati (EMAC). Baadhi ya vitabu vilibainika kwamba vilikuwa hafifu na havikuwa na mazoezi ya kutosha.

Uamuzi wa kurejesha utunzi na usambazaji kwa TET siyo tu umezima soko la vitabu vya kampuni binafsi bali umeondoa hata ushiriki wa kamati za shule kuamua aina ya vitabu vya kununua.

0
Your rating: None Average: 5 (2 votes)
Soma zaidi kuhusu: