Mwalimu Fatuma anahitaji huruma, msaada


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 05 October 2011

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli

HAJAOMBA msaada wala kuhurumiwa na jamii, lakini hivyo ndivyo jumuiya ya Shule ya Msingi ya Majengo katika halmashauri ya manispaa ya Mikindani, mkoani Mtwara itakavyopaswa kumfanyia Mwalimu Fatuma Mohamed Nendakutoha (55).

Siku moja mwaka 2007, Fatuma aliamka akisikia maumivu na ganzi miguuni. Akafanya mazoezi ya viungo ya hapa na pale kujiweka sawa kamav ile anavyofundisha na kuwasimamia wanafunzi wake wa darasa la I na II na shule nzima (vipindi vya PE).

Haikusaidia. Maumivu yalizidi kadri siku zilivyopita. Fatuma ambaye ni mwalimu mkuu msaidizi katika shule hiyo, akaanza kuishtaki miguu yake kwa madaktari wa kisayansi.

Alianzia hospitali ya Ligula ambako madaktari walimpima. Majibu ikawa ana kisukari. Tangu siku hiyo akajua ‘adui’ wa miguu yake ni kisukari. Mapambano yakaanza.

Mwaka 2008 akaona ukungu (fungus) umeota kwenye pacha za vidole vya miguu. Akatibiwa, akapona. Mwaka 2009 ukungu ukajirudia. Akatibiwa, akapona.

Mwaka 2010 malengelenge yakaibuka kwenye nyayo, vidole na sehemu ya juu ya nyayo. Akaishtaki tena Ligula, akapata nafuu. Baadaye mwaka huo, aliporudi safarini Tanga, alikuta miguu yote imevimba kama vile ana matende.

Juni mwaka 2011 miguu yake ikaanza kutoa majimaji sehemu za nyayo na vidole. Akatibiwa Ligula, akahamishiwa hospitali nyingine ya Ndanda ndogo. Julai 2011 hali ikazidi.

Mumewe, Soud Rashid, ambaye ni mwalimu mstaafu katika Chuo cha Ualimu Mtwara, akaongeza nguvu ya kumsaidia mkewe kutafuta tiba. Akatazama akaunti yake, akachungulia vijisenti vya kustaafu kwake. Akavikusanya vyote ili ampeleke mkewe mpenzi katika Hospitali ya Misheni ya Nyangao. Fatuma alipokewa, akalazwa.

Madaktari wakampima. Wakatoka na majibu mabaya: Bakteria wa kisukari wamekula miguu ya mkewe. Wakashauri ikatwe. Fatuma akajiuliza moyoni, ‘Nikatwe miguu?’ Ikawa kama kisa cha hadithi ya “The unwilling amputee” ya Agoro Anduru iliyochapwa katika gazeti la Sunday News miaka ya 1980.

Rashid akawaza: ‘Mke wangu akatwe mguu?’ Akasita. Rashid, Fatuma na watoto wao wakajibu, “Hapana”. Haoo, wakarudi tena hospitalini Ligula.

Wakapata wazo wakate rufaa katika Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam. Wakamwarifu mwajiri wake – Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Mikindani. Akawahurumia, akawaruhusu.

Tarehe 6 Agosti 2011, Fatuma alisafirishwa kwa gari la kubeba wagonjwa kutoka Mtwara hadi Muhimbili. Halmashauri ilibeba gharama za kumsafirisha mwalimu Fatuma, mumewe na watoto wawili na kulipa posho ya siku saba ya jumla ya Sh. 325,000.

Muhimbili wakapokewa vizuri. Madaktari wakasoma ripoti ya Ligula na Nyangao. Wakachukua vipimo upya. Wakatoa majibu: Ili kuokoa maisha yake (mwalimu Fatuma), inabidi akatwe miguu yote miwili; hatua hiyo ikichelewa kisukari kitapanda hadi kwenye nyonga!

Mtihani mkubwa ukawa kwa Rashid, mume mtu. Akamuonea huruma mkewe. Kwamba akikataa atampoteza, akikubali ina maana ameridhia mkewe kuwa mlemavu. Rashid akakumbuka alivyoishi na mkewe.

Fatuma akamuuliza mumewe, “Utakuwa radhi kuishi nami nikiwa sina miguu?” Mume baada ya kukumbuka kiapo cha ndoa yao , akajibu, “Ndivyo tulivyoapa, mimi na wewe hadi kufa katika shida na katika raha.” Rashid aliona heri kuwa na mke mwenye ulemavu kuliko kumpoteza.

Msimamo huu ulimpa nguvu mwalimu Fatuma. Akaongeza ujasiri, imani na amani moyoni. Madaktari waliporudi kumuuliza msimamo, akajibu kwa ujasiri, “Na iwe hivyo tiba inavyotaka.”

Tarehe 9 Agosti 2011, Fatuma alikatwa mguu wake wa kulia, juu kidogo ya goti. Huu ndio umeliwa zaidi na bakteria. Tarehe 30 Agosti mguu wa kushoto nao ukakatwa, chini kidogo ya goti.

Rashid akaanza kutafuta namna ya kurahisisha usafiri wa mkewe. Tarehe 19 Septemba akapiga hodi makao makuu ya Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kutoa taarifa ya hali ya mkewe, Fatuma, ambaye ni mwanachama wao. Aliomba msaada wa hali na mali .

Hakutembea bure. Alipewa palepale Sh. 125,000. haikutosha. Mkuu wa kitengo cha kushughulikia walimu, wafanyakazi na wanafunzi wenye ulemavu cha CWT, Peter Mlimahadala akahangaika kutafuta kiti au baiskeli ya magurudumu manne. Akapata msaada shirika la Erich Sharpen la Sweden .

Tarehe 1 Oktoba, Mlimahadala akamkabidhi mwalimu Fatuma msaada huo kwenye wodi ya Kibasila alikolazwa baada ya operesheni.

Mlimahadala: “CWT ina mpango endelevu wa kusaidia wanachama wake wenye ulemavu kwa kuwapa bure vitu kama fimbo nyeupe, magongo, baiskeli au viti pamoja na vifaa vya kuongeza usikivu. Mpango huu ulizinduliwa na Katibu Mkuu wa CWT, Alhaji Yahya Msulwa Juni 2010.

“Tangu Januari mwaka huu, huyu ni mwanachama wa 85 kusaidiwa na CWT,” alifafanua Mlimahadala.

Rashid sasa anasema, “Nimepokea kwa moyo mkunjufu. Yeye, watoto na mimi tulikubali na huo ndio mtihani mkubwa nilionao.”

Anashukuru kwamba Mfuko wa Bima ya Afya ndio unagharimia matibabu ya mkewe mpaka akipona lakini zaidi, “Familia yangu inaishukuru sana CWT kwa msaada huu tena wa haraka kiasi hiki.”

Mwaswali muhimu: Je, Fatuma ataweza kumudu kazi yake ya kufundisha na kuruka na watoto anaowapenda sana wa madarasa ya I na II?

Miundombinu iliyokuwa rafiki alipokuwa anatembea kwa miguu yake, haitakuwa kero sasa, kwenda jikoni kupika, kutembea barabarani, kuingia ofisini na darasani, kupita ili kukagua wanafunzi kwenye mistari? Vipi miundombinu ya vyoo vyetu?

Jambo lililo dhahiri ni kwamba Fatuma ataanza maisha mapya na magumu. Hataweza kutembea kwa miguu yake. Kukimbia. Hataweza kuingia darasani kufundisha na akimudu itakuwa kwa msaada wa wanafunzi wake, familia yake, walimu wenzake na jirani zake.

Kama wanafunzi walimpenda watamfuata nyumbani kwake. Watamsukuma hadi shule na kumwingiza ofisini. Muda wa vipindi ukifika, watamfuata ofisini na kumsukuma hadi darasani. Vipi kama wanafunzi walikuwa wanamchukia?

Fatuma alizaliwa mwaka 1956, Newala mkoani Mtwara akiwa mtoto wa tatu kati ya wanne kwa baba mmoja na mama. Baada ya kumaliza elimu ya msingi, alijiendeleza na akajiandikisha kama mtahiniwa binafsi. Akafaulu na kuchaguliwa kuingia Chuo cha Ualimu Mtwara.

Alipohitimu akapangiwa kufundisha shule ya msingi Chitoholi, Newala, baadaye alihamishiwa shule ya msingi Ligula na baadaye Chuno, zote za mkoani Mtwara.

Mwalimu Fatuma hakuridhika. Alienda kusomea Sayansi Kimu Chuo cha Mandaka. Alipomaliza, akapangwa shule ya msingi Majengo, anayofundisha sasa.

Nyumbani kwake kuna vyeti na tuzo kadhaa. Mwaka 1982 alitunukiwa cheti na wakaguzi wa Kanda ya Kusini baada ya kuteuliwa mwalimu bora wa darasa la I na II. Mwaka 1989 aliteuliwa mfanyakazi bora wa halmashauri ya manispaa ya Mikindani; akazawadiwa cheti na fedha taslimu Sh. 20,000.

Aliolewa mwaka 1972 na akajaaliwa watoto sita; wasichana wawili na wavulana wanne.

0789 383 979, jmwangul@yahoo.com
0
No votes yet