Mwalimu Nyerere na miaka 13 ya pensheni


Aristariko Konga's picture

Na Aristariko Konga - Imechapwa 01 November 2009

Printer-friendly version

ULIKUWA ni mwaka wa 13 tangu Mwalimu Julius kambarage Nyerere aache madaraka ya urais. Nilipata fursa ya kuwa mmoja wa watu waliokuwa wamemtembelea Aprili 1998 kijijini Butiama wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kuifutia madeni Tanzania.

Katika ziara hiyo, pamoja na mambo mengine, nilipata fursa ya kuona maisha ya Mwalimu wakati wa pensheni yake pamoja na mazingira yanayomzunguka.

Jambo la kwanza kutafakari ni jinsi alivyoondoka madarakani mwaka 1995 jijini Dar na kurejea moja kwa moja Butiama. Halikuwa jambo rahisi miongoni mwa Watanzania.

Maelfu ya wananchi tangu alfajiri walikuwa wamefurika kwenye uwanja wa zamani wa ndege wa Dar es Salaam. Hali ya wananchi hao ilikuwa ni vigumu kuielezea, maana wapo waliokuwa wakilia na wapo walioonekana wakiwa na furaha mioyoni mwao. Bila sha kila mmoja alikuwa na sababu yake kuwa na hali hiyo.

Kwenye uwanja huo, kulikuwa na ndege ambayo ni wachache walioweza kuiona. Wale ambao hawakubahatika kuiona waliambiwa kwamba ilikuwa inaitwa 5H CCM. Ni ndege iliyokuwa ikimilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake nyakati za mwisho za mwaka 1985.

Muda mfupi tu ulitokea msafara wa magari yasiyokuwa na idadi, yakiongozwa na vimulimuli vya polisi. Ndani ya gari aliteremka Mwalimu Nyerere, rais wa Jamhuri kwa miaka 24.

Wengine walioongozana naye alikuwa ni Mama Maria Nyerere, watoto na baadhi ya wajukuu. Baadhi ya wananchi walilia na kushangilia.

Walilia, ukiacha wale waliofanya hivyo kutokana na kubanwa na umati wa watu. Waliokuwamo pia wale waliojiuliza ni jinsi gani Tanzania ingeendelea kuwa nchi ya amani baada ya Mwalimu kuondoka.

Waliofurahi walifanya hivyo kwa kumtakia heri Mwalimu Nyerere katika maisha yake ya kustaafu na pia walikuwa wakifurahi kwa sababu walipata fursa ya kumwona Baba wa Taifa akiondoka salama baada ya kuacha madaraka kwa ridhaa yake, iliyopambwa na heshima kubwa.

Mara Mwalimu alionekana akipanda ngazi ya ndege huku akikimbia, jambo ambalo lilikuwa ni kawaida yake. Lakini alipofika ngazi ya mwisho, kabla ya kuingia kwenye ndege, alisimama, akageuka nyuma, akawapungua mkono wa kwaheri maelfu ya wananchi, waliokuwa wamejitokeza kumuaga mkongwe huyo wa siasa.

Ndege ikaondoka Dar es Salaam. Ikawasili uwanja wa ndege wa Musoma. Mapokezi yalikuwa makubwa mno. Watu waliokuwa kwenye msafara wake ilibidi wachelewe kuondoka baada ya kila aliyefika uwanjani kutaka kumwona Mwalimu kwa karibu.

Hatimaye msafara uliondoka na kukaribia kijiji cha Buswegwe, mpakani na kijiji cha Butiama. Hapo gari la polisi lililokuwa limewasha taa na kimulimuli likawa nyuma ya gari maalum, lililoandaliwa na ukoo wa Mwalimu, yaani ukoo wa marehemu Chifu Nyerere Burito.

Gari hilo aina ya Land Rover lilisheheni ngoma za kichifu, zilizotumika tangu enzi za Mzee Nyerere Burito, aliyefariki dunia mwaka 1942. Aliyeongoza upigaji ngoma ni Joseph Nyerere, mdogo wake Mwalimu, na kupambwa vilivyo na wanawake.

Mwalimu Nyerere alipoingia kijijini Butiama hakutaka kwenda nyumbani kwake moja kwa moja. Badala yake alikwenda nyumbani kwa kaka yake, Chifu Edward Wanzagi Nyerere.

Mwalimu alikuwa na kawaida ya kumuenzi kaka yake huyo kutokana na ukweli kuwa ndiye aliyemsomesha na kumtunza hadi alipoanza kujitegemea.

Tofauti na walivyo watu wengine waliopata kuwa katika nafasi kama yake, Mwalimu aliishi maisha ya kawaida sana, ambayo hayakumtofautisha na mwanakijiji wa Butiama.

Maisha yake kijijini yalikuwa na mpangilio maalum. Kila siku asubuhi na jioni, kabla ya kuendelea na kazi zake shambani, ilikuwa ni lazima kwake kwenda kusali kanisani.

Baada ya kutoka kanisani asubuhi alikuwa akipata kifungua kinywa, mara nyingi ikiwa ni chai au uji, vilivyochanganywa na karanga. Aghalabu vitafunio vyake vilikuwa ni mihogo au viazi vilivyochemshwa. Ilikuwa ni mara chache kula mkate au maandazi.

Haikuwahi kutokea Mwalimu akapata kifungua kinywa akiwa peke yake. Mara zote hushiriki na wajukuu, majirani au wageni.

Alikuwa ni mkulina na mfugaji, akiwa na mashamba yenye ukubwa zaidi ya eka 90. Alikuwa akilima mahindi, karanga, mihogo, pamba, nyonyo, mtama, ulezi, viazi na maharage. Alikuwa pia mfugaji, akifuga ng’ombe, mbuzi, kuku na nguruwe.

Kwa kawaida alikuwa akifanya kazi shambani hadi mchana, kisha hurejea nyumbani kupata chakula. Baada ya kula alikuwa akipumzika kidogo na kurudi shambani saa 10 au 11 jioni.

Nyumba yake ndogo ambayo, iliyojengwa kwa matofali ya zege na mawe, ipo juu ya mlima, mahali ambako aliishi baba yake, Chifu Brito.

Mazingira yanayoizunguka nyumba hiyo ni ya asili, ingawa waweza kuona vifaa vya teknolojia ya kisasa. Ni ya asili kwa sababu ni mahali ambapo wapo wanyama aina ya ngedere na pimbi, ambao hupanda kwenye nyumba na kusogea kwenye jiko ili kupata mabaki ya chakula.

Sehemu ya nje, ambako hupokelea wageni, kuna kibanda kilichojengwa juu yam awe. Hapo kuna meza yenye bao. Mwalimu alikuwa ni mpenzi wa mchezo wa bao. Alikuwa akicheza na wageni, ndugu, marafiki na jamaa zake wanaomtembelea.

Kusini na mashariki ya kibanda hicho kuna vihenge ambaho huhifadhi nafaka. Ilikuwa ni kawaida kuwakuta watu kwenye vihenge hivyo, ambao walikuwa na ukosefu wa chakula. Walikuwa wakipewa chakula kulingana na maelekezo ya Mwalimu au yeyoye aliyepewa dhamana hiyo.

Upande wa mashariki kuna makaburi ya ndugu zake. Kuna kaburi kubwa lililojengwa kwa saruji. Hilo ndilo kaburi la baba yake. Sambamba na kaburi hilo kuna kaburi la mama yake, Mugaya wa Nyang’ombe, ambaye alifariki dunia mwaka 1997, akiwa na umri unaokadiriwa kuzidi miaka 100.

Kwa hiyo, Mwalimu alikuwa akiishi katika mazingira ya kawaida, ya kijijini, akiwa amezungukwa na wananchi wengine wa kawaida. Bila shaka kuna mengi ambayo Watanzania wataendelea kujifunza kutokana na maisha yake ya kawaida.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: