Mwalimu pokea ujumbe huu


Aristariko Konga's picture

Na Aristariko Konga - Imechapwa 23 December 2009

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

NIMEAMUA kukuletea ujumbe huu Mwalimu. Ninafanya hivyo huku nchi yetu ikiwa na ukame na njaa kwenye baadhi ya maeneo na sehemu nyingine zikiwa zimeathirika na mafuriko kwa kiasi fulani. Wananchi wa Same ni mashahidi wa janga hili.

Mwanzoni kulikuwa na malalamiko. Wana-Same walikuwa wanashangaa-yu wapi kiongozi wa nchi ambaye angeshuhudia maafa yaliyozima pumzi za watu 24 katika Kata ya Mamba, wilayani Same.

Hatimaye Rais Jakaya Kikwete amefanikiwa kuingia kwenye milima ya Same. Ametua katika kijiji cha Mamba Miamba. Amewafariji waliopoteza ndugu zao 24. Lakini kikubwa ametoa ahadi. Serikali itawajengea nyumba nane waathirika wa mafuriko yale. Si haba Mwalimu. Rais kajitahidi kuwaonea huruma wahanga wa mafuriko haya,na msaada huu si kitu kidogo kwao. Aslani.

Mwalimu, pia ninaandika ujumbe huu huku kukiwa na mjadala mkali kuhusu taasisi iliyochukua jina lako-Mwalimu Nyerere Foundation (MNF). Ninafahamu kuwa unaielewa vizuri taasisi hii, kwa kuwa uliiacha ikifanya kazi. Ukafanya hata harambee ya kuchangia fedha ili ifanye kazi kwa ufanisi.

Taasisi hii inashambuliwa. Inapigwa ‘mawe.’ Inabezwa. Inasakamwa. Inatishwa. Inang’ong’wa. Inasukwasukwa. Inabebeshwa kejeli. Inalaumiwa. Inashutumiwa. Inapuuzwa. Inasutwa na inatuhumiwa kwa mengi. Kisa?

Tarehe 30 Novemba hadi 2 Desemba, 2009, MNF iliandaa kongamano la kutathmini mwelekeo wa taifa miaka 10 tangu ututoke. Watu wengi walipata fursa ya kuzungumza. Walipaaza sauti ili kuonyesha hisia zao.

Kongamano lilikuwa chini ya mwenyekiti wa bodi ya wadhamini ya MNF, Dk Salim Ahmed Salim. Lilihudhuriwa na washiriki wapatao 200 kutoka sehemu mbalimbali nchini. Walikuwamo viongozi wa serikali, wa dini, wastaafu, asasi za kiraia, wasomi, wanaharakati wa maendeleo ya jamii, wanahabari na wengineo.

Mambo mengi yalizungumzwa kwenye kongamano, lakini nitakueleza jambo moja ambalo, ninadhani, lilichefua mitima ya baadhi ya wanasiasa wenye uvumilivu kidogo, kiasi cha kuibebesha MNF lawama, kejeli, shutuma, na kila aina ya uovu.

Wengi wamekugeuka. Kongamano lilikiri kwamba taifa limepungukiwa, kwa kiasi kikubwa, na maadili, hasa upande wa viongozi baada ya kifo chako. Kwamba, hali hiyo inatishia amani, utulivu, mshikamano, maendeleo na ustawi wa taifa.

Wengi wamekugeuka. Kongamano linasema mmomonyoko wa maadili unadhihirishwa na ongezeko kubwa la rushwa na ufisadi, uvunjaji wa haki za binadamu, tabia na hulka ya viongozi kushindana kwa kujilimbikizia mali, kutoheshimiana na kujengeka kwa mitandao isiyo rasmi.

Wakati wengi wamekugeuka, yupo aliyepigilia msumari ambao umesababisha mjadala huo wa siku tatu uendelee mpaka sasa (wiki mbili baadaye). Huyu ni Mateo Qares, waziri wa zamani.

Wakati wengi wamekugeuka, Mateo Qares anasema Rais Kikwete anawajibika kuchukua maamuzi magumu, katika mazingira ya ufisadi uliokithiri. Kwamba asipofanya hivyo, hakuna haja ya kumpa fursa ya kugombea kipindi cha pili cha miaka mitano hapo mwakani.

Kauli ya Qares ndiyo iliyofichua ni nani hasa kakugeuka na yupi bado anakuunga mkono, hata baada ya miaka kumi ya kutoweka kwako kimwili.

Wengi wamekugeuka Mwalimu. Wa kwanza kutoa kauli za kulipuka dhidi ya kongamano, alikuwa ni katibu mkuu wa chama ulichoasisi-CCM. Huyu ni Yusuf Makamba.

Wengi wamekugeuka. Makamba alikwenda mbali kweli kweli. Akawaita waliochangia kwenye kongamano hilo kuwa ni wehu. Yaani wale waliotaka Rais Kikwete achukue maamuzi magumu, kurejesha uongozi kwenye unyoofu, ni wehu. Hebu na tutazame kwenye kamusi, mwehu ni nani hasa:

Kamusi ya Kiswahili sanifu, iliyotolewa na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, Dar es Salaam, toleo la pili, iliyochapishwa na Oxford University Press, inamtafsiri mwehu kuwa ni: “Mtu aliyechanganyikiwa, ambaye vitendo vyake vinafanana na vya mwendawazimu.”

Mwalimu, wengi wamekugeuka. Hivi ni nani ana uelekeo wa kuchanganyikiwa kati ya Makamba na Dk. Salim wa MNF? Ni nani anaelekea kuchanganyikiwa kati ya Makamba na Joseph Butiku, mkurugenzi mtendaji wa MNF? Jibu liko wazi. Ni Makamba. Anaonyesha kila dalili kwa tathmini ya kauli zake.

Wengi wamekugeuka. Chama Cha Mapinduzi kimetoa tamko kwamba katika siku hizi za kuelekea uchaguzi kutakuwa na “hadithi na nyimbo” nyingi za kumchafua rais na serikali yake.

Kama nilivyosema, wengi wamekugeuka. Enzi zako kulikuwa na dhana ya “kujisahihisha” na “kukosoana.” Leo hii maneno hayo yanawakilishwa na neno jipya la “kuchafuana.” Leo hii kumwambia kiongozi achukue maamuzi magumu ili kuiokoa nchi ni kumpaka uchafu!

Wengi wamekugeuka Mwalimu. Iweje leo tujifanye vipofu hadi tusione kasoro zilizopo katika uongozi? Iweje tuchekelee na kushangilia wakati maghala yanabomolewa na akiba yetu kuchukuliwa? Kuna mushkeli Mwalimu. Hapa ndipo tunahitaji maamuzi magumu.

Wengi wamekugeuka. Mwalimu, nimelazimika kuleta ujumbe huu baada ya kukereketwa na kauli ya msomi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, mwenyekiti mwenza wa taasisi ya utafiti-REDET. Huyu anawabeza washiriki wa kongamano la MNF. Ni wale waliomtaka Rais Kikwete achukue maamuzi magumu katika kupambana na ufisadi.

Wengi wamekugeuka. Dk. Bana anatoa kauli mbovu, ya kufikirika tu. Ati, badala ya kumkosoa Rais Kikwete kwenye kongamano walipaswa waombe fursa ya kukutana naye faragha! Hii ni ajabu. Kwa mtaji huu kongamano lote lilipaswa kuombewa fursa ikulu, liwe la faragha! Warsha, semina, na makongamano mangapi yatahitaji faragha za aina hiyo? Hii ni hoja hewa.

Wengi wamekugeuka Mwalimu. Ninao wasiwasi kama kweli fikra za wasomi kama hawa ziko huru. Ninadhani fikra kama hizo zimevia. Hazikui tena, hata kama zitawekewa ‘mbolea.’ Watu kama akina Dk. Bana wanapaswa kupigwa msasa upya na wanamapinduzi kama akina Walter Rodney. Wanapaswa kuingia darasani upya.

Mwalimu pokea ujumbe huu. Tuombee tusafiri salama hadi Oktoba mwakani, ili tupate chekeche zuri la kuwapata viongozi wanaojali maslahi ya nchi na watu wake.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: