Mwalimu wa Nyerere ataka CCM iadhibiwe


George Marato's picture

Na George Marato - Imechapwa 20 October 2010

Printer-friendly version

MWALIMU aliyemfundisha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere katika shule ya msingi, amesema adhabu pekee ya kukipa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa kuendesha nchi katika mazingira ya rushwa na kutojali wazee, ni kukinyima kura katika uchaguzi wa mwishoni mwa mwezi huu.

Mwalimu huyo, James Irenge, mwenye umri unaokadiriwa kuwa miaka 120, anasema CCM imekumbatia rushwa na kwamba haijali hata wazee waliotumikia taifa kwa uadilifu.

“Kukinyima kura ndiyo itakuwa njia sahihi ya kumuenzi Nyerere," anasema Mwalimu Irenge alipohojiwa na mwandishi wa makala hii, nyumbani kwake mjini Musoma, huku akichuruzika machozi.

“Kwa vile dunia nzima sasa inatambua kuwa CCM si chama cha wakulima na wafanyakazi tena; kwamba hakijali watu wake; ni vema wanaojiita wazee wenye busara, ambao hawajapata doa la wizi wa mali za umma, wakajiondoa ndani yake mapema,” anasema Mzee Irenge.

Mzee Irenge alikuwa mwalimu wa Nyerere katika shule ya msingi Mwisenge ya mjini Musoma, mkoani Mara.

Anasema alimfahamu Nyerere mwaka 1934 wakati alipokwenda kuanza darasa la kwanza katika shule hiyo, na mwaka 1935 alimfundisha darasa la tatu ikiwa ni baada ya kuvukishwa darasa moja kutokana na ufahamu wake mzuri darasani.

“Alikuwa na ufahamu mkubwa sana, sema akili, mpaka wakamvusha darasa na mimi nikaanza kumfundisha darasa la tatu mwaka 1935," anakumbuka Mwalimu Irenge.

Mwalimu Irenge alistaafu mwaka 1970. Ana watoto 12 na wajukuu 27. Kwa sasa anaishi Mwisenge, mjini Musoma. Anasema serikali imeshindwa kumlipa kiinua mgongo stahiki kwani tangu alipostaafu, amekuwa akilipwa pensheni ya Sh. 200 kwa mwezi.

Mwaka 2005 pensheni yake ilipandishwa kufikia Sh. 20,000 na tangu Januari mwaka huu ameanza kupata Sh. 50,000 kwa miezi.

Amesema anashangaa kuona viongozi wa siku hizi hawathamini hata wazee wakati Baba wa Taifa alikuwa anapenda sana kuongea na wazee ili kujua matatizo yao na hata kuelewa ni wapi anakosea katika utawala wake.

“Viongozi wetu siku hizi wamekuwa na tamaa, tofauti na wakati wa Mwalimu Nyerere. Kwa mfano, wizi wa mamilioni ya shilingi uliotokea Benki Kuu na mikataba mibovu inayofanywa na serikali, ni kipimo tosha kuwa serikali haiko makini,” ameeleza.

Mzee Irenge anasema lengo la CCM lilikuwa kuwasaidia wakulima na wafanyakazi katika kuendeleza taifa lao; lakini kwa sasa chama hicho kimekuwa cha wafanyabiashara; kitu ambacho Mwalimu hakupenda.

Anasema kwa sasa hakitaki tena chama hicho kwani siyo chama alichokitaka Baba wa Taifa. “Enzi za Nyerere hakukuwa na matumizi ya fedha wakati wa kutafuta uongozi; lakini hivi sasa sifa kubwa ni fedha,” anasema kwa sauti ya kusikitika.

Wakati Nerere akiwa hai, anaeleza mzee Irenge kwamba alikuwa anamjali sana na kwamba kuna wakati alikuwa anakwenda Butiama na kukaa huko huku wakiongea masuala ya nchi.

Anasema mara nyingi Nyerere alimpa misaada midogo midogo, tofauti na sasa ambapo viongozi wameshindwa hata kwenda kumjulia hali.

Anasema kitendo hicho kinamuumiza sana kwani viongozi wa sasa wamekuwa tofauti na alivyokuwa Nyerere, kwani kiongozi pekee anayefika kumsalimia mara mojamoja nyumbani kwake ni mbunge wa jimbo la Musoma Vijijini Nimrod Mkono.

Katika maisha yake, anasema alifurahi sana siku ambayo Nyerere alikabidhiwa hati ya kuonyesha kuwa Tanganyika imekuwa huru. “Nilijiona mshindi; nimewashinda wakoloni; kwani uelewa wa Nyerere kuhusu mabaya ya ukoloni ulianzia shule ya Mwisenge nilipokuwa nikimfundisha.

Muda wote wa mahojiano na Irenge, unaona kuwa anaongea kwa taabu na mara kadhaa akisaidiwa na mtoto wake.

Anakumbuka kuwa hata kufikia kulipwa pensheni ya sasa ya Sh. 50,000 ambayo hata hivyo haitoshi katika mazingira haya, alihangaika sana.

Hadi anaidhinishiwa kiasi hicho, alikuwa tayari ameandika barua sehemu mbalimbali, kuanzia Ofisi ya Rais, haki za binadamu, wizara ya fedha na wizara ya kazi ambapo, barua ya wizara hiyo ilikabidhiwa kwa waziri Profesa Athuman Kapuya alipokwenda Musoma kwenye sikukuu ya wafanyakazi mwaka 2009.

"Kwa sasa maisha yangu si mazuri maana nalipwa kidogo wakati ni haki yangu. Nimeishaandika barua kila ofisi lakini hawajanisaidia; bali kama angekuwepo Kambarage (Julius Nyerere), ningesaidiwa haraka," anasema Mwalimu Irenge.

Anang’ang’ania kuwa kwa sasa serikali imewabagua sana wazee, kwani hata yeye alialikwa mwaka jana kwenye sherehe ya wafanyakazi mjini Musoma na kupewa blanketi; “lakini wameshindwa kusikiliza malalamiko yangu.”

Anasema hata mkuu wa mkoa wa Mara haendi kumtazama wakati anaishi jirani; kitu anachosema kinaonyesha viongozi wa siku hizi “hawana upendo kwa wazee;” ambayo ni tofauti kubwa kati ya uongozi wa sasa na ule wa Mwalimu Nyerere.

Akiongelea kifo cha Nyerere mwaka 1999, Mwalimu Irenge anasema Nyerere hakupenda kufia nje ya nchi yake, ingawa kuna watu ambao walilazimisha mauti yamkute nje kwa vile walikuwa na lengo lao. Hakutaja lengo hilo.

Anasema Nyerere alikuwa akitokwa machozi pale alipokuwa akiongea naye kabla ya kuondoka kwenda Uingereza. Anamnukuu akisema kuwa asingeweza kurudi mzima na kwamba anawaacha “watu wake.” Sasa baada ya kifo chake, nchi imekuwa ya kila mtu kufanya anavyotaka, anasema Irenge.

Akirejea maisha chini ya ukoloni, Mzee Irenge anasema alikuwa anachukia sana wakoloni kwa tabia yao ya kuwapiga viboko.

“Walikuwa wanatunyanyasa, wanatuibia mali zetu; hivyo nilikuwa siwapendi hata kidogo, ndio maana nilitumia muda wangu usiku kumsimulia Nyerere historia juu ya ukoloni na madhambi yake,” anasimulia.

Anasema Nyerere alimudu masomo darasani lakini alikuwa na shauku ya kujua mengine zaidi. Kwa mfano, anasema alikuwa akimuuliza jinsi wazungu walivyoingia nchini na jinsi walivyoshika utawala.

Kutokana na shauku ya Nyerere kutaka kujua mambo mengi; na kwa vile alionyesha nia ya kusoma mambo mengi kuliko wanafunzi wengine, Mwalimu Irene aliamua kuwa anamfundishia nyumbani kwake usiku ili ampe somo kamili juu ya utawala wa kikoloni.

Anasema Nyerere hakuwa na tabia ya kujisifu ingawa alikuwa na uwezo mkubwa darasani mpaka kufikia kuruka darasa la pili na kwenda darasa la tatu. Alikuwa akipenda haki kwa kila mtu na alichukia sana kuona mwenzake anaonewa.

Kitendo cha wakoloni kuwapiga wazee wao, anasimulia Mzee Irenge, kilikuwa kikimuumiza sana na ndiyo maana akaamua kutafuta mbinu ya kuwafundisha watoto, akiwemo Nyerere, na kwa siri, historia ya ujio wa wakoloni.

Mwalimu Irenge anawataja watu mashuhuri waliosomea shule ya msingi Mwisenge kuwa ni pamoja na Bhoke Munanka, Joseph Butiku na Joseph Warioba aliyewahi kuwa waziri mkuu.

Akiongea kutoka kitandani kwake, kwa sauti ya unyonge, mzee Irenge anasema anasikitika kuwa anaweza kuaga dunia kabla serikali haijamlipa mafao yake. Anadai kiinua mgongo ambacho amepigania tangu alipostaafu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: