Mwambungu, Kamhanda hawafai Songea


Nyaronyo Kicheere's picture

Na Nyaronyo Kicheere - Imechapwa 29 February 2012

Printer-friendly version

UBOVU wa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), uhuni wa viongozi wa Jeshi la Polisi, na unafiki wa wakuu wa wilaya na mikoa umedhihirika wiki iliyopita mjini Songea, Ruvuma kwa kuuawa raia wanne wasio na hatia yoyote.

Ushahidi wa ubovu wa serikali ni huu. Raia wasio na hatia waliuawa na Polisi eti kwa sababu walidiriki kuandamana kudai na kushinikiza serikali iwalinde wakati serikali haioni sababu ya kuwalinda!

Malalamiko ya wananchi ni kwamba watu wanauawa na kila anayeuawa maiti yake inakutwa imeondolewa ‘jembe na kengele’ zote kama ni mwanaume na kama ni mwanamke maiti yake inakutwa imeondolewa ‘bustani yote ya Eden’ kwenye bonde la Mesopotamia.

Pamoja na malalamiko hayo ya muda mrefu, si Jeshi la Polisi wala chama tawala mjini Songea walioshituka na kuchukua hatua. Je, wanafurahia?

Mauaji haya yametokea mfululizo kwa siku kadhaa bila Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Thabit Mwambungu, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Michael Kamhanda na Mkuu wa Wilaya ya Songea, Thomas ole Sabaya kuchukua hatua wala kusema chochote!

Hapo ndipo wananchi wakaamka, wakaamua kwenda kwa wakubwa hao wanaolipwa mishahara kwa posho kutokana na kodi zao wawalinde kwa sababu hiyo ndiyo kazi yao. Ghafla akaibuka Kamanda Kamhanda akisema waliouawa ni kutokana na wivu wa mapenzi!

Wivu wa mapenzi? Haya na tukubaliane na msanii huyu Kamhanda kuwa waliouawa wameuawa kwa sababu ya wivu wa mapenzi.

Maswali kwa Kamanda Kamhanda; walioua wenzao kwa sababu ya wivu wa mapenzi ni akina nani? Je, wamekamatwa wangapi na wamewekwa mahabusu ipi?

Kama Polisi wamechunguza na kugundua kuwa raia wanauawa kwa sababu ya wivu wa mapenzi kwanini polisi hao hawajamkamata hata mmoja, hawajamsweka korokoroni hata mmoja na hawajamfungulia mashtaka hata mmoja? Huu ni usanii na Jeshi la Polisi halitakiwi kuongozwa na wasanii.

Haiwezekani watu wauawe mitaani kama kuku, lakini wakiandamana kudai haki ya kulindwa wauawe tena na wale wanaotakiwa kuwalinda. Na kuhalalisha mauaji hayo eti wanadai “yanatokana na wivu wa kimapenzi!” Kamanda Kamhanda ni msanii, hafai afukuzwe kazi mara moja.

Baada ya wananchi kushindwa kuvumilia kuuawa bila Jeshi la Polisi kuchukua hatua, wameandamana kwenda kwa Mkuu wa Mkoa (RC) ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya ulinzi na usalama mkoani kutaka awaamuru Polisi watekeleze wajibu wao wa kuwalinda, badala yake RC anaamuru polisi waue waandamanaji kwa risasi za moto!

Mwambungu kanukuriwa akitoa amri ya kutotembea usiku na Polisi kuwasaka watuhumiwa wa maandamano hayo. Mtu anayetoa kauli ya namna hii badala ya kuhangaika kutafuta kisa au chanzo cha mauaji yaliyosababisha maandamano ya wananchi ndiye aliyetoa amri ya kuua waandamanaji.

“… Polisi wataendelea kuwasaka watuhumiwa (wa maandamano) usiku ili kuwabaini na kuwachukulia hatua za kisheria,” Mwambungu alinukuriwa na vyombo vya habari. Kwa hiyo, Mwambungu anaona wabaya ni watuhumiwa wa maandamano ya kudai walindwe na siyo wanaoua raia na kukata sehemu zao za siri.

Kwa maana nyingine huyu Mwambungu anakubaliana na usanii wa Kamanda Kamhanda anayedai wanaouawa ni kutokana na wivu wa mapenzi ndiyo maana hawakuchukua hatua zozote za kisheria dhidi ya hao wanaoua. Kwa maneno mengine, Kamnda Kamhanda na Mwambungu wanasema ni halali kisheria mtu kumuua mgoni wake.

Mkuu wa Mkoa anayependelea wauaji kwa sababu za wivu wa mapenzi hatufai na hivyo aondolewe kwenye wadhifa huo mara moja. Kwanza Mwambungu ni mnafiki maana kesho yake alionekana kwenye runinga akiwafariji hospitalini hao anaodai ni watuhumiwa wa maandamano. Hatutaki viongozi wanafiki.

Mkurugenzi wa Operesheni na Mafunzo, Kamishna Paul Chagonja ni kiboko cha njia. Huyu eti katumwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Said Mwema kuongoza maofisa kutoka Makao Makuu ya Polisi kwenda mjini Songea kufanya uchunguzi wa ghasia hizo.

Akiwa njiani kuelekea Songea, Kamishna Chagonja alihojiwa na vyombo vya habari na akajibu ifuatavyo: “Maandamano hayakuwa ya amani bali ya kihuni na yalilenga kuvamia ofisi za serikali, ikiwamo ikulu ndogo na ofisi ya mkuu wa mkoa wa Ruvuma.”

Akaendelea Kamishna wetu Chagonja, “Sijafika huko ndiko naelekea, lakini yale si maandamano ya amani. Yaani wahuni wanataka kuvuruga nchi waachiwe? Kuweni wazalendo, msiwe kama labda ninyi ni wandishi wa BBC kutoka Uingereza, hii ni nchi yenu.”

Kama hivi ndivyo, Chagonja anafuata nini Songea? Kama amekwishaamua kuwa walioandamana ni wahuni waliotaka kuvuruga nchi, anakwenda Songea kufanya nini?

Anakwenda kufanya uchunguzi wa kitu gani wakati tayari ameshapata majibu kuwa walioandamana ni wahuni na hawakuwa na sababu ya msingi kuandamana?

Nitawakumbusha ya Kamishna Chagonja. Alipokwenda Nyamongo wakati wa vurugu katika mgodi wa North Mara alimhoji Mwenyekiti wa kijiji ambaye alimweleza kinagaubaga kwamba wanaosababisha vurugu za kuvamiwa mgodi ni polisi.

Kesho yake Mwenyekiti alikamatwa na Polisi akapigwa mateke, ngumi, mikanda, vitako vya bunduki na kubaki hoi bin taaban. Akapelekwa hospitali ya Sungusungu ikashindwa, hospitali ya wilaya ya Tarime na mkoani Mara ikashindikana hadi Bugando alikolazwa miezi miwili.

Hapa hatuulizi kitu, tunafahamu Polisi wasingempiga Mwenyekiti hivihivi. Walimpiga kwa hasira kutokana na kile alichomweleza Kamishna Chagonja. Leo huyu Chagonja anakwenda Songea kuongoza uchunguzi, atachunguza nini? Atakachoambiwa na raia hatawaeleza Polisi wa Songea? Na watakachomweleza hawatapigwa kama alivyopigwa Mwenyekiti wa kijiji kule Nyamongo?

Halafu Mkuu wa Wilaya ya Songea nimeambiwa ni Thomas ole Sabaya aliyehamia huko akitokea Serengeti. Mimi sikumtarajia ole Sabaya atende mema Songea kwani hana historia ya kutenda mema. Mkuu huyu wa wilaya ndiye aliyewagombanisha kiaina Wanyamongo na Wangoreme.

Ole Sabaya aliwaamuru raia wa Serengeti pale Ngoreme kukamata watu na ng’ombe wao kutoka Nyamongo watakaovuka mto Mara kwenda kulisha ng’ombe wao wilayani humo.

Eti raia wengine warande Tanzania nzima kutafuta malisho lakini Wanyamongo wasiruhusiwe kuvuka mto kwenda Ngoreme kulisha mifugo yao. Matokeo ya amri ile vurugu zilitokea. Hatufai ole Sabaya naye ang’oke mara moja.

Mwambungu, RPC Kamhanda, ole Sabaya na Chagonja wameshindwa kutekeleza wajibu wao wa kulinda raia na kauli zao ni za watu waliolewa madaraka ndiyo maana raia wanaoandamana kudai haki kwao ni wahuni.

Pia si vibaya kwa Rais Jakaya Kikwete kuunda Tume huru kuchunguza vifo hivi. Mfano mzuri ni Tume huru chini ya jaji iliyofanya kazi nzuri kubainisha ukweli vijana watatu na dereva teksi mmoja walipouawa na polisi mwaka 2006. Rais aunde Tume kuchunguza tukio hilo la Songea.

0
No votes yet