MwanaHALISI laipa kiwewe CCM


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 17 November 2010

Printer-friendly version

GAZETI la MwanaHALISI linaandaliwa mikakati ya “kuzimwa” kwa madai kuwa ni moja ya vyombo vilivyokosesha Chama Cha Mapinduzi (CCM) ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu uliopita.

Mikakati hiyo ni pamoja na kuzuia gazeti hili kusomwa redioni wakati wowote kuanzia sasa.

Aidha, wahariri wa vyombo vya habari ambavyo vimeitwa “sugu” wamesukiwa mkakati wa kuwalainisha, ikiwa ni pamoja na kukutana nao kwa lengo la kujenga urafiki wa karibu na serikali na chama kilichopo madarakani.

Kwa mujibu wa waraka wenye jina la “kada” wa chama hicho, unaodaiwa kuandikwa na mmoja wa wanachama wake, John John Nchimbi, MwanaHALISI limekuwa mwiba kwa chama chake katika uchaguzi mkuu uliomalizika 31 Oktoba mwaka huu.

Mwandishi anataka gazeti hili lidhibitiwe kwa maslahi ya chama hicho. Waraka unaodaiwa kuandikwa na John Nchimbi unaonyesha kuandikwa siku nne baada ya uchaguzi mkuu kumalizika.

Waraka huo ambao umenaswa na gazeti hili unasema, “Tunaweza kuzuia magazeti pinzani kama MwanaHALISI yasisomwe kwenye Radio Free Africa (RFA) ambayo inasikilizwa sana kanda yote ya ziwa; na Radio One ambayo inasikilizwa sana kanda yote ya Mashariki na Kaskazini.

“Kwa kufanya hivi, tutakuwa tumezuia mzunguko wa taarifa zake kwa takribani asilimia 40. Hili lazima lifanywe na watu wachache na makini kwelikweli wenye mapenzi ya kweli na chama chetu,” unasema waraka huo.

Hata hivyo, John Nchimbi alipoulizwa kuhusu waraka huo, ambao umesambazwa kupitia mtandao wa intaneti – email, tarehe 4 Novemba 2010, alionyesha mshangao.

Akiongea kwa njia ya simu na MwanaHALISI, Nchimbi alihoji, “Huo waraka una jina langu? Una saini yangu? Kama una saini, naomba uje ofisini kwangu nikuonyeshe saini yangu uone kama inafanana na hiyo iliyopo kwenye huo waraka.

“Nataka pia kuamini kwamba kuna Nchimbi wengi sana. Mimi mwenyewe, kwa mfano, nina mtoto anaitwa John John Nchimbi. Kwa hiyo si lazima waraka huo uwe umetoka kwangu hata kama majina yanafanana,” alisema.

Nchimbi alisema yeye hawezi kupendekeza jambo baya kama la kudhibiti vyombo vya habari kwa vile yeye ni muumini wa uhuru wa vyombo vya habari.

“Vyombo vya habari vya Tanzania vimefanya kazi kubwa sana kwa serikali na CCM. Siwezi kuviangalia kwa mtazamo hasi namna hiyo. Pia nina marafiki wengi sana kwenye vyombo vya habari, ukiwamo wewe mwandishi, na hivyo sina matatizo navyo hata kidogo,” alisema.

Waraka huo ambao umesambazwa kwa viongozi wa serikali na watu wenye ushawishi ndani ya chama hicho, unachambua sababu zilizokifanya CCM kisifanye vizuri katika uchaguzi uliopita.

John John Nchimbi ni jina la mdogo wa aliyekuwa naibu waziri wa ulinzi na jeshi la kujenga taifa katika serikali iliyopita ya Rais Jakaya Kikwete, Emmanuel Nchimbi, na ni miongoni mwa makada vijana wa chama hicho.

Waraka unasema vyombo vya habari nchini, hususani gazeti hili, “limekuwa sawa na vyama vya upinzani; ingawa lenyenyewe limekuwa ikifanya kampeni bila kuchoka.”

“Vyombo vya habari vimekuwa mwiba mkubwa kwa CCM. Vyombo vya habari ni chama cha upinzani kinacho-operate - kinachofanya kazi bila kuchoka dhidi ya CCM,” anasema Nchimbi katika waraka wake huo.

Anasema, “Magazeti hasa ndio chachu ya ushawishi wa vyombo vya habari hapa nchini. Muda mwingi vinafanya mashambulizi dhidi ya chama au viongozi mbalimbali ambao ni muhimu kwa chama na hivyo kupelekea chama kuathirika pia na kujenga chuki ya wananchi dhidi ya chama chao.”

Nchimbi anasema, “Sehemu kubwa ya Watanzania wanasoma vichwa yva habari katika mbao za kuuzia magazeti na pia kusikiliza vichwa vya habari katika radio na televisheni Tanzania nzima. Hivyo athari za propaganda zao zinafika hata sehemu ambazo hakuna magazeti.”

Nchimbi anasema upinzani, hususani Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) umepata matokeo mazuri katika mikoa ya Kanda ya Ziwa Viktoria kwa sababu ya nguvu ya vyombo vya habari.

Hata hivyo, Nchimbi anajenga hoja kuwa magazeti ya aina ya MwanaHALISI yasingeweza kuwa na athari kubwa kwa CCM iwapo yasingekuwa yakisomwa kwenye redio na luninga ambako ndiko wananchi wengi wanakoyasomea.

“Hakuna gazeti hata moja linalouza nakala zaidi ya elfu 30 kwa siku. Kwa sasa gazeti la Mwananchi wanauza nakala elfu 23-24 kwa siku. Tanzania Daima nakala elfu 21 na Nipashe nakala elfu 18. Parapaganda za magazeti zinaenezwa na redio na televisheni,” anaeleza.

Katika kuweka udhibiti kwa vyombo vya habari, mwandishi wa waraka aliyejiita John John Nchimbi anapendekeza mambo mawili makubwa yafanyike kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Kwanza, chama chake kiwe na mfumo wa “mchanganyiko wa upole na ukali” kwa kile alichoita, “ili chama kisonge mbele.”

Kwenye upole, anapendekeza CCM kiwe na utaratibu wa kukutana na wahariri wa vyombo vya habari mara kwa mara na kupitia mikutano hiyo wajue nani ni mzuri kwao na nani ni mbaya.

Kupitia mikutano hiyo anasema, “Tutaweza kufanya uchunguzi wa kujua ni nani huwa anapeleka habari mbalimbali za chama katika vyombo hivyo.

“Kugundua habari zinazokaribia kutoka zenye kuathiri chama kutasaidia ku -pre-empty kabla habari husika haijatoka,” anaeleza.

Linapokuja katika ukali ndipo Nchimbi anapopendekeza kuhusu udhibiti wa magazeti kama MwanaHALISI, Tanzania Daima na Mwananchi kwenye matangazo ya redio.

Mbali na kudhibiti vyombo vya habari, mwandishi wa waraka ameeleza mtazamo wake kuhusu kilichochangia chama chake kuporomoka ambapo matokeo ya kura za rais yametoka asilimia 80 mpaka asilimia 61 na kupoteza majimbo 52 ya ubunge.

“Kushuka kwa asilimia 19 ni jambo la hatari sana . Hata sehemu tulizoshinda chaguzi bado kura zimekuwa za ushindani mkubwa na upinzani,” anaeleza.

Anasema viongozi na wanachama wa chama hicho wamekosa umoja na upendo wa kweli, na kwamba pale wanapokosana wanaona kuwa njia pekee ya kurekebishana ni kusaidia upande wa upinzani.

Mfano anaotoa ni kushindwa kwa chama hicho katika jimbo la Nyamagana na Ilemela. “Tufike mahali umoja na mshikamano vihubiriwe kuwa ni nguvu ya CCM,” anasema.

Sababu nyingine iliyochangia CCM kushindwa vibaya katika uchaguzi huu, ni viongozi wake “kufanya kampeni za kizamani wakati dunia inabadilika. Utaratibu wa kura za maoni umeleta matatizo na pia timu ya uenezi haikuwa makini.”

Anapendekeza kuwapo kwa viongozi mahili wa kampeni, hasa watu wanaoheshimika ndani na nje ya chama.

Anasema, “Mtu kama Tambwe Hiza hapaswi kuzungumza na vyombo vya Habari kwa niaba ya chama. Hawa ni watu ambao hawana heshima kubwa kiasi hicho katika jamii.”

Aidha, Nchimbi anasema, “Katibu mwenezi wa chama anaruhusu sana kufunikwa na watu ambao kimsingi alipaswa yeye ndio awe anawaongoza.”

Waraka huo pia umetaka mabadiliko makubwa katika utendaji kazi wa jumuiya za chama katika kipindi cha kampeni na kabla ya kipindi cha kampeni.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: