MwanaHALISI linahujumiwa


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 12 March 2008

Printer-friendly version

JUZI, Jumatano, tarehe 5 Machi 2008, gazeti letu la MwanaHALISI, lilitimiza miezi miwili tangu livamiwe na watu wenye kemikali na panga ambapo mimi nilimwagiwa kemikali machoni, kujeruhiwa na kitu kikali usoni na mshauri wetu, Ndimara Tegambwage kukatwa kwa panga kichwani na mgongoni.

Kana kwamba hayo hayakuwa hujuma tosha, juzi usiku wa saa 5.10, siku ambayo tulikuwa tunatimiza siku 60 tangu ofisi zetu ivamiwe, mtu mmoja aliita kwenye simu yangu Na. 0784440073. Simu ya aliyeita haikuonyesha namba. Aliyeita alisema, ?"Sali sala yako ya mwisho.

Siku tano nyuma, hapo 29 Februari 2008, saa 6.12 mchana, nilikuwa nimepokea ujumbe wa simu uliosheheni matusi ambayo kamwe hayawezi kuwasilishwa kwenye vyombo vya habari, lakini mkitaka nitayasoma hapa. Bali sehemu ya ujumbe huo ilisema,

" ?hivi wewe umekosa habari za kuandika magazetini eeh! Ss bac kama umechoka kuishi tutakuondoa duniani kuanzia ss."

Hivi siyo vitisho vidogo kwa mtu yeyote yule. Huu ni mwendelezo wa vitisho kwa miezi sita hivi ambavyo ni pamoja na kugongwa na gari, kuchomewa gari, kusutwa na kutukanwa na kutishiwa kwa njia ya simu.

Rais alipokuja kuniona hospitalini Muhimbili, aliwaambia waandishi wa habari na aliofuatana nao kwamba waandishi waendelee kuandika, wasiwe na woga bali wakuchukue "tahadahari."

Tulimuelewa rais kuwa yeye binafsi hawezi kufanya vitendo vya kihuni lakini kwamba alikuwa alikuwa anajua kuna watu wenye "ujasiri" wa kufanya vitendo vichafu.

Hatuna shaka kwamba ni hao ambao rais alitaka tujihadhari nao ambao wanaendelea kututishia na labda wanaandaa mipango mikubwa ya kuteketeza gazeti la wananchi na hata kuteketeza maisha yetu.

Bali hatujui jinsi ya kujihadhari. Tunachojua ni kuandika habari za kweli na sahihi.

Tulitarajia kwamba kama atakuwepo mtu asiyeridhika na habari zinazoandikwa na gazeti letu, atatwambia kwa ustaraabu au atakwenda mahakamani. Huko sheria itachukua mkondo wake. Sivyo ilivyo sasa. Tunaona vitisho vinaendelea na tunaishi kwa woga mkubwa.

Nimewaita ndugu zangu waandishi wa habari, kuwaambia kwamba matukio yote ya hivi karibuni tayari nimeyafikisha kwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishena Alfred Tibaigana na kwa Inspekta Jenerali wa Polisi, Said Mwema. Ninataka ninyi mjue kwamba moja ya vyombo vyenu, MwanaHALISI, kinafanyiwa hila na watendaji wake wanatishiwa kuuawa.

Wanaotutishia sisi wanawatisha na ninyi pia. Hili siyo la MwanaHALISI pekee yake. Wanatishia haki yetu ya kukusanya na kusambaza habari. Wanatishia uhuru wa wananchi wa kutoa mawazo. Wanavunja haki zetu za msingi na za katiba.

Nina maombi mawili makuu kwenu kwa leo. Kwanza, tuwape wananchi taarifa kwamba chombo chao kinatishiwa na watumishi wake wanatishiwa kuangamizwa. Pili, tusimame pamoja kupinga vitisho hivi.

Katika hili, Jukwaa la Wahariri, TAMWA, MISA, MOAT, Baraza la Habari na baadhi ya waandishi mmoja, wameonyesha msimamo thabiti. Tunawaomba tupige mbiu kwa pamoja.

Aidha, tunaomba asasi za kijamii zisimame nasi, kwa njia mbalimbali, katika kupigania haki na uhuru wa wananchi wa kutoa mawazo, ikiwa ni pamoja na kukemea vitisho na hujuma dhidi ya gazeti letu.

Lakini pia tunaitaka serikali kutuhakikishia ulinzi. Watumishi wa MwanaHALISI ni raia wema wanaostahili kulindwa kama raia wengine.

Bali kwa upande mwingine, wanaotishia maisha yetu ni watenda jinai ambao wanapaswa kushughulikiwa kwa mkono wa serikali. Hatutarajii wahalifu kuendelea kuwika wakati serikali tuliyoichagua wenyewe iko madarakani.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: